Kupatwa na shida au mabaya kupo kwa mwanadamu, hilo hatuwezi kulikwepa tukiwa bado tupo duniani, tuwe tunapenda au hatupendi. Lazima tupitie kwenye mapito fulani magumu, inaweza ikawa kwenye familia yako.

Ama inaweza ikawa kwenye kazi yako, au inaweza ikawa kwenye biashara yako, au inaweza ikawa kwenye huduma yako, na mengine mengi ambayo sijayataja hapa. Yote hayo unaweza ukawa unapitia kwenye shida ngumu inayolenga eneo lako.

Tunapokuwa tunapitia katika nyakati kama hizo, wakati mwingine tunaweza kubaki na mawazo mengi yasiyo na majibu, au tunaweza kubaki kulaumu wengine kuwa wao ndio chanzo cha matatizo yote.

Badala ya kuendelea kuangalia nani ndio mwenye kusababisha mabaya yatupate, au badala ya kuendelea kulia na kunung’unika pasipo na utaratibu unaoeleweka. Ipo njia ambayo tunapaswa kuifuata wakati tunapitia katika nyakati fulani mabaya katika maisha yetu.

Cha muhimu sana na la kuzingatia siku zote tunapopatwa na shida yeyote ile, tunapaswa kumwomba Mungu wetu, bila kujalisha shida au mabaya yaliyokupata yanaonekana ni mazito kiasi gani. Unapaswa kumwomba Mungu wako.

Rejea: Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. YAK. 5:13 SUV.

Tena kama una uwezo wa kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, unaweza kuziimba vile unavyoweza, kumbuka hii ni wakati ule unapitia kwenye shida au umepatwa na shida au mabaya.

Huenda unajiuliza inakuwaje pale unapokuwa umepatwa na shida au mabaya alafu wakati huo unakuwa huna uwezo wa kuomba Mungu au huna uwezo wa kujiombea mwenyewe. Habari njema ni kwamba jibu lako lipo kabisa.

Kabla sijakupatia andiko lenye jibu lako, unapaswa kuelewa kuwa sio wakati wote utaweza kuomba Mungu unapopatwa na shida, au sio watu wote wanaweza kustahimili na kuweza kumwomba Mungu Wakati wamepatwa na shida.

Wale ambao hawezi kujiombea wenyewe au hawawezi kabisa wakati wa shida yao, wanapaswa kuomba msaada wa watu wengine waliokoka. Watu hao watasimama badala yao kuwaombea, kupitia maombi yao Mungu atasikia.

Rejea: Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. YAK. 5:14 SUV.

Vizuri kuwaita watumishi wa Mungu, wanaweza wasiwe wazee wako wa kanisa kutokana na eneo uliopo wakati huo. Unaweza kuwaita watumishi wa Mungu wa kweli, maana wapo wengi na wanapatikana ukiwatafuta.

Usikae kwenye shida inayokusumbua pasipo kuwashirikisha watumishi wa Mungu na wakati wewe mwenyewe huna uwezo wa kuomba, na ukijaribu kufanya hivyo unakuwa unashindwa. Usikae kimya ita wazee wako wa kanisa au mchungaji wako au kiongozi wako wa kanisani kwako akuombee.

Huwezi kuwaita mwenyewe usiwe na shaka, agiza mtu wa kwenu akawaite ili uje uombewe, huu ni utaratibu wa kiMungu. Na usifikiri kuwaita watumishi wa Mungu ni udhaifu, hapana ni utaratibu wa kiMungu kwa yule mtu ambaye hawezi.

Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku, kupitia usomaji wako unakutana na maarifa sahihi ya kiMungu ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu. Huwezi kusoma Neno la Mungu kila siku peke yako, ungana na kundi la wasap la Chapeo Ya Wokovu. Unaweza kuwasiliana nasi kwa wasap +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com