Inawezekana kabisa mtu aliyeokoka na kuenenda katika njia nzuri inayompendeza Mungu, siku akipatwa na shida fulani yenye kudhoofisha mwili wake. Huwa tunaona ametenda dhambi au uhusiano wake na Mungu haupo vizuri wakati huo kutokana na mateso anayopitia.

Mtu anaweza kuumwa sana na kufanyiwa huduma ya maombi, na maombi hayo yasitoe majibu kama waliyotarajia waombaji inaweza kugeuka habari tofauti kabisa. Wapo watakaoona mtu huyo atakuwa amemkosea Mungu mahali ndio maana ameshindwa kumjibu maombi yake.

Wakati mwingine tumefikiri tofauti kabisa, tumeona mtu kupita kwenye majaribu mazito kama mkristo haikupaswa kukutwa na mambo mabaya. Kwahiyo mtu akiwa anapita kwenye wakati fulani mgumu anaonekana kwa mtazamo usio sahihi kabisa.

Kutokujua neno la Mungu wakati mwingine imewafanya watu wengi kuongea au kuhalalisha vitu ambavyo sio vya ukweli, maana upo ukweli wenyewe ila unakwepeshwa pembeni au unashindwa kueleweka vizuri kutokana na mtu kutojua maandiko matakatifu.

Ukiwa kama mkristo ambaye anajisomea biblia kila siku, unao uwezo wa kutambua wakati ulionao sasa wa mateso makali. Amini kwamba wakati huo nao utapita.

Rejea: Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. 1 PET. 4:12 SUV.

Kujaribiwa sio kitu kigeni, kupitia kwenye mateso magumu sio kitu kigeni kwako, ukishajua hili katika maisha yako ya wokovu utaishi vizuri ukiwa na amani ya moyo kwa sehemu.

Usione kuwa ni mambo ya ajabu pale unapopitia kwenye majaribu, hesabu ni mambo ambayo yako na yana maumivu yake wakati unapitia. Pamoja na yana maumivu sana hupaswi kurudi nyuma, songa mbele.

Mungu akusaidie sana wewe ambaye unapitia kwenye shida fulani, kupitia kusoma unaweza kukutana na mambo mazuri ya kukujenga kiroho na kimwili.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
www.chapeotz.com
+255759808081