Miongoni mwa mambo ya kuchunga sana kwenye safari yako ya maisha ya wokovu ni kujilinda sana usije ukarudia mambo mabaya yanayomkosea Mungu.

Ulikuwa mlevi ukaja kuokoka, hakikisha hurudii tena ulevi, ulikuwa mzinzi, muongo, mwizi, na mengine yanayofanana na hayo, hakikisha huyarudii tena. Bali endelea kumtumainia Mungu, maisha yako ya wokovu yaendelee kuwa safi zote.

Usipokuwa makini ukaacha tamaa za mwili zikutawale, ukarudi tena nyuma, alafu bahati mbaya ukashindwa kurudi kwa Yesu Kristo. Ukweli ulio wazi kuhusu hali yako ya wakati huo itakuwa mbaya kuliko ulivyokuwa mwanzo.

Kabla hujaokoka huenda watu walikuwa wanakuona mbaya sana kutokana na matendo yako hovyo, baada ya kuokoka ukaanza kuonekana wa maana. Uwe na uhakika siku ukijichanganya na kuamua kurudi nyuma kumtumikia shetani, uwe na uhakika hali yako itakuwa mbaya zaidi.

Rejea: Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. 2 PET. 2:20 SUV.

Kama ulishaamua kujitenga na mambo mabaya ya dunia na kuamua kuokoka, nakusihi sana uchunge sana mwenendo wako usije ukajichanganya ukarudi nyuma tena. Mbaya zaidi utakaporudi nyuma hali yako itakuwa mbaya zaidi ya mwanzo.

Kuishi maisha matakatifu ni gharama sana ila kinachohitajika ni kusimama vizuri na Mungu wako, bila kujalisha mazingira uliyonayo sasa. Unahitaji kujilinda sana usije ukajikwaa, ukayarudia yale mambo yasiyofaa mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com