
Unapokuwa kwenye msimamo wa jambo lolote lile lenye manufaa, lenye kumletea Mungu wetu sifa na utukufu, sio wakati wote utakuwa salama sana bila kukutana na mambo mabaya yenye kukuvunja moyo.
Watu ambao wameamua kufuata tamaa mbaya za dunia hii, mara nyingi huwa wana maneno fulani ya kuwavunja moyo wengine walioamua kusimama na Yesu Kristo. Hugeuka na kuanza kuwapa maneno ya dhihaka juu ya imani yao.
Watu wa mambo ya dunia, wanaweza kuwaambia wale waliompa Yesu Kristo maisha yao kuwa hakuna siku ya mwisho, hii ni kutokana na tangu mababu zao hawajawahi kuona mwisho wa dunia ukifika.
Wengine wataenda mbali zaidi na kuanza kuwashawishi waliosimama vizuri na Mungu, kuwaambia wanajisumbua bure na kukosa mambo mazuri ya dunia hii. Wangefanya mambo ya dunia hii bila kuogopa kitu.
Dhihaka zipo nyingi sana, wakati mwingine zimekuwa kama mwiba kwetu kutokana na maneno tunayoambiwa na watu wasiomjua Yesu Kristo. Wanajiona wao ndio wanafanya vizuri zaidi kuliko wale wanaomjua Kristo.
Unapokutana na mambo kama hayo yenye kukudhihaki juu ya imani yako au juu ya kazi yako, inaweza kukuletea shida ndani yako na kuanza kujiona labda ulikosea mahali.
Unapaswa kufahamu unapokutana na dhihaka za watu juu ya wokovu wako, hupaswi kupata shida kiasi hicho, unachopaswa kujua ni kuwa ukiwa kama mkristo kukutana na dhihaka ni jambo ambalo lipo.
Rejea: Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. 2 PET. 3:3-4 SUV.
Hayo ni maandiko matakatifu yanasema hivyo, usifikiri unachokutana nacho kwenye maisha yako ya wokovu ni jambo jipya ambalo linaanza kwako. Haya yapo sana hasa hizi siku za mwisho.
Unapokutana na mtu ambaye amekamatwa ufahamu wake na shetani, anafanya mambo ambayo yapo kinyume na Neno la Mungu na mtu huyo anatoa maneno yasiyofaa. Ujue namna ya kukabiliana nao ili wasije wakakushinda.
Bila shaka umeshajifunza mambo ya msingi ya kukusaidia unapokutana na mtu mwenye dhihaka juu ya maisha yako ya wokovu. Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, nakusihi sana ujiwekee ratiba vizuri ya kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com