
Mtu anayesababisha mafarakano au yule ambaye ni mzushi, mtu huyo anaunawezo wa kuwafanya mvurugane kila wakati, tena anaweza kuwatoa jasho kweli na maneno yake tu.
Mara nyingi sana watu wanaosababisha mafarakano huwa wanajiona wanaelewa sana, huwezi kumwondoa haraka kwa kile anachoamini yeye ni sahihi kwake. Mnaweza kubishana naye sana na msifikie mwafaka.
Hili jambo limekuwa likiwaumiza watu kutokana na kushindwa kukabiliana na wazushi au watu wanaosababisha mafarakano wengi wao huona ni usumbufu.
Huenda umekutana na jambo kama hili kwenye maisha yako ya wokovu na umeshindwa umfanyaje huyo anayekuzushia mambo ambayo sio mazuri au anawafanya mfarakane kila wakati.
Kama umekuwa hujui ufanyaje kuhusu mtu wa namna hii, ondoa shaka tunaenda kujifunza hili kupitia maandiko matakatifu. Kuanzia leo utajua namna gani utaweza kukabiliana na mtu wa namna hiyo.
Maandiko matakatifu yanatupa njia ya kupita kuhusu hili jambo, kama ipo njia sahihi ya kuweza kukabiliana na watu wazushi au watu wanaosababisha mafarakano.
Jambo tunalopaswa kulifanya kwa mzushi ni kumwonya juu ya tabia yake, tunaambiwa tumwonye kwa mara ya kwanza, akikataa rudia mara ya pili kumwonya juu ya tabia yake.
Ukiona bado anaendelea na tabia yake ile ile na tayari umemwonya zaidi ya mara, epukana naye au mkatae kabisa huyu mtu. Usipomkataa utaendelea kujikwaa kwa Bwana Yesu.
Rejea: Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae. TIT. 3:10 SUV.
Umeona hilo andiko, unaweza kuona ni jinsi gani inakuwa rahisi kwako unapokutana na mtu wa namna hiyo unakuwa unajua unawezaje kuepukana naye.
Epukana na migogoro isiyo na maana kwa mtu ambaye ni mzushi, utaenda vizuri na hutomkosea Mungu wako kwenye eneo hilo tulilokuwa tunalishughulikia.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com