Watu wote ni wa Mungu ila sio wote ni wana wa Mungu, wapo wanamkataa Mungu kwa kuabudu miungu mingine, wakifikiri wanamwabudu Mungu wa kweli. Kukataa kwao kumkiri Kristo kama Bwana na mwokozi wao huku wanadai wanamwabudu Mungu, huo ni uongo mkubwa sana.

Wale wanaomjua Mungu wa kweli wanasikilizana, mambo mengi wanaendana, tabia zao na tembea yao ni moja, maana wanayemwini ni Mungu mmoja.

Ukikuta watu wanayemjua Mungu wanasikilizana, hata kama watakutana wakiwa wageni wote, wanaweza kukaa mahali pamoja wakamwabudu Mungu pasipo shida yeyote ile.

Tofauti na wale ambao hawamjui Mungu wa kweli, kwanza hawezi kuwaelewa wanafanya nini wale wanaomjua Mungu, pili kuwasikia kile wanakisema na kukiamini ni ngumu kwao. Hapa ndipo wale waliomjua Mungu wa kweli wanapoweza kumjua Roho wa kweli, na roho wa upotevu.

Rejea: Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu. 1 YOH. 4:6 SUV.

Furahi kwa sababu unamjua Mungu, Kristo yumo ndani yako na wewe u ndani yake, umepata neema kubwa sana, maana wapo hawamjui kabisa Mungu japo wanaofikiri wanamjua.

Wangemjua Mungu wa kweli wasingeweza kusali mahali ambapo kuna roho ya udanganyifu, wala wasingeweza kukimbilia mahali ambapo kuna manabii au walimu wa uongo.

Tokana na Mungu rafiki, yaani kubali kuzaliwa mara ya pili, usiwe mtu mwenye dini tu, dini bila Yesu moyoni ni hasara tupu ndugu. Hakikisha imani yako msingi wake umejengwa katika Neno la Kristo, na si vinginevyo.

Imani iliyo kinyume na Neno la Mungu, hiyo ni Imani potovu, japo na hapa unapaswa kuwa makini, sio imani zote wanaotumia biblia unayoitumia wewe ni Imani sahihi. Zingine ni za uongo ila zinatumia kivuli cha maandiko matakatifu, ndio maana ni muhimu sana kusoma mwenyewe Neno la Mungu ukalijua.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com