
Upo umhimu mkubwa wa kuwa na Roho Mtakatifu, ukiwa kama mkristo unapaswa kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu ndani yako. Hili ni la muhimu sana katika maisha yako ya wokovu, bila Roho Mtakatifu maisha yako hayatakuwa vizuri.
Roho Mtakatifu anakaa kwa mtu aliye safi, yule ambaye anaishi maisha ya utakatifu ndiye Roho Mtakatifu atakaa ndani yake siku zote za maisha yake.
Yapo mafundisho ambayo yanamkataa Roho Mtakatifu ila ukiwa mkristo mwaminifu mbele za Mungu, hili halitakuwa jambo gumu kwako. Ni mzigo ambao unabebeka katika maisha yako ya kiroho.
Roho Mtakatifu ni msaidizi wetu, kuna jambo gumu katika maisha yako au kuna jambo umekosa majibu yake, yeye ATAKUFUNDISHA. Tena atakufundisha hatua kwa hatua kuhakikisha umeelewa vizuri.
Yapo mambo yanatusumbua kupata majibu yake au hatuyaelewi kabisa, kwa sababu ya kukosa fundisho lake sahihi. Ndio maana unaona mambo yako hayaendi ni kwa kukosa Roho Mtakatifu.
Tumeona Roho Mtakatifu anafundisha, fahamu kwamba Roho Mtakatifu anao uwezo wa kukumbusha yote unayofundishwa na watumishi wa Mungu. Kile umesoma ndani ya biblia yako, utaona kikiendelea kuletwa kwenye kumbukumbu zako.
Rejea: Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. YN. 14:26 SUV.
Tamani sana kujazwa na Roho Mtakatifu, tumeona faida hizi kuu mbili anafundisha na kukumbusha yote uliyofundishwa. Hutabaki kama ulivyo, bali utaona mabadiliko mazuri katika maisha yako.
Muhimu sana kukumbuka haya, Roho Mtakatifu anafundisha na anakumbusha. Kama ni hivyo amua sasa kujazwa na Roho Mtakatifu kama siku ile ya pentecoste.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com