Mtu anapokukemea kwa kawaida lazima utajisikia vibaya sana, tena inaweza kukusumbua sana ndani ya moyo wako na kuanza kufikiri labda hakupendi ndio maana amekukemea kwa namna ambayo hukuipenda sana.

Na wale ambao wanatusifia tu na kutuacha tuenende kama tupendavyo, huwa tunaona ni watu wazuri na ndio wanatupenda sana ndio maana hawatukemei sana kama wengine wanavyowakemea wao.

Kukemea imekuwa ikichukuliwa kwa sura mbaya, wengi huwa tunaona tofauti kabisa, kumbe haipo hivyo kwa jinsi ambavyo tumekuwa tukiambiwa au kwa vile ambavyo tumekuwa tukiaminishwa na watu au jamii.

Haijalishi tumekuwa na ufahamu wa siku nyingi kuhusu hili, huenda ulikuwa unaona mtu anayekukemea mtu huyo hakupendi, au mtu huyo hajui kuongea na watu vizuri, au mtu huyo hana utu kwa wengine.

Mawazo ni mengi sana kuhusu hili, lakini fahamu kwamba yule anayekukemea kwa nia njema ya kukufanya urudi kwenye mstari sahihi. Ujue huyo mtu anakupenda sana, haijalishi unamwona kwa sura mbaya ila fahamu upendo wa huyo mtu ni mkubwa sana kwako.

Sio kila wakati unaweza kuona ulipokosea, lakini wanaokupenda wanapoona umekosea, na wakachukua hatua nyingine ya kukemea juu ya tabia yako mbaya. Usije ukafikiri kuwa huyo mtu hana upendo na wewe, upendo wake kwako upo wa kutosha.

Kukemea ni tabia ya kiMungu, Mungu wetu huwa anatukemea pale tunapoenda kinyume na Neno lake, anaweza kukemea kupitia watumishi wake au anaweza kukemea kupitia Neno lake.

Rejea: Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. UFU. 3:19 SUV.

Ikiwa kuna mahali hasa eneo hili la kukemewa, ulikuwa unapata shida sana moyoni mwako, unapaswa kuelewa kwa mujibu wa Neno la Mungu. Upende usipende kukemewa ni tabia ya kiMungu, kama unakosea utakemewa tu.

Unaona kabisa hili linakupa shida kubwa au Unaona kukemewa huwa kunakupa wakati mgumu katika maisha yako ya wokovu, unapaswa kuelewa kuanzia sasa.

Usibaki unasononeka kuwa fulani anakukemea wakati anakuwekea mazingira yako vizuri na Mungu, cha msingi ni kutii na kuenenda sawasawa na mapenzi ya Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com