
Wakati mwingine tunaweza kubaki na maswali mengi sana juu ya wale ndugu zetu waliouawawa kikatili kwa ajili ya kutangaza habari njema za Yesu Kristo. Na wale waliokuwa na msimamo mkali juu ya imani yao kwa Yesu Kristo, ikawapelekea kuuwawa kinyama.
Huenda wengi wetu huwa tunapata wakati mgumu mahali ambapo wapo, na wengine hufikiri wangekuwa kweli wanatangaza habari njema za Yesu Kristo, au walikuwa wana shuhuda za yale Yesu Kristo aliwatendea. Wakakutwa na mauti iliyosababishwa na msimamo wao mkali juu ya imani ya Kristo.
Tunawaza labda njia zao hazikuwa vizuri ndio maana Yesu akaacha kuwatetea wakauwawa, maana tunajua kila mtumishi wa Mungu analindwa na Mungu mwenyewe. Iweje mtumishi wake auwawe kikatili wakati anayemtumikia yupo hai na anaona?
Maswali ni mengi sana na yana hoja zenye nguvu hasa ukiziangalia kibinadamu, lakini ukiangalia kwa jicho la rohoni na Neno la Mungu likawa ndani yako. Utakuwa umepunguza idadi kubwa sana ya maswali ambayo usingepata majibu ya uhakika kwa mtu ambaye hana Neno moyoni mwake.
Tunapaswa kujua ni kwamba wale waliouawawa kwa ajili ya jina la Yesu Kristo, roho zao zipo sehemu salama zinasubiri siku ya hukumu. Hupaswi kuwa na mashaka sana, unachopaswa kufahamu kuawawa kinyama kwa mtumishi wa Mungu sio kana kwamba alikuwa na dhambi mbele za Mungu.
Rejea: Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao. UFU. 6:9-11 SUV.
Ukisoma mistari hiyo niliyokushirikisha hapo unapata kitu kikubwa sana cha kutia moyo, hata kama ulikuwa na imani juu ya watumishi wa Mungu. Unapata mwanga zaidi kuhusu wale waliouawawa kwa ajili ya jina la Yesu Kristo.
Kuawawa kwao kinyama hakuwazui kuingia mbinguni, siku ile ya mwisho Bwana atawadhihirisha wazi, wala hupaswi kupata shida juu ya hili. Maana unaweza kuingiwa na hofu na unaacha kuwa jasiri, kwa kufikiri ukiuwawa hautakuwa sehemu salama.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, unafahamu mambo mengi ya kuweza kukusaidia katika maisha yako na kuwasaidia wengine katika jamii.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika,
Samson Ernest
www.chapeotz.com