
Tunafanya mambo mengi sana mengine yanampendeza Mungu na mengine hayampendezi Mungu, yale yasiyompendeza Mungu ndio tatizo kwetu. Maana ni hatari katika maisha yetu, pamoja na kupuuza baadhi ya vitu kutokana na kutoona madhara yake.
Tunapaswa kujua kuwa ipo siku ya mwisho, hata kama tutaona haiwezi kuwepo hiyo siku tujue tu ipo siku ya mwisho, tukubali tukatae tuwe na uhakika ipo siku ya mwisho. Ile siku ya hukumu ya Mungu, siku ambayo itakuwa ya kutisha sana katika maisha ya mwanadamu.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali tunaweza kusema au tunaweza kuona siku ya mwisho haiwezi kuwepo, kama unaamini Neno la Mungu. Hili nalo lipo ndani ya biblia yako, na leo naenda kukushirikisha andiko linalotuthibitishia hili.
Kwa picha ya andiko hili inaonyesha wazi tukio hili la siku ya mwisho litakuwa ni la kutisha sana, ni kama haijulikani ni lini, na kama haijulikani kama hili jambo litaweza kutokea ama la.
Rejea: Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea. UFU. 8:7 SUV.
Hili ni tukio kubwa la kutisha sana kwetu sisi wanadamu, kama hutopata nafasi ya kuingia uzima wa milele, mateso yake yatakuwa makali sana.
Tunapaswa kuishi maisha yanayompendeza Mungu, na la msingi ni kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Maana yeye ni njia ya kweli na uzima, bila yeye hatuwezi kumwona Baba yetu mbinguni.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com