Unaweza usijue sana kibaya kilichopangwa juu yako, ukaendelea na maisha yako kama kawaida ila mbele yako ukawa umeandaliwa mpango mbaya juu ya maisha yako. Mpango ambao ni wa kuondoa uhai wako kabisa.

Wakati shetani anaandaa mabaya juu ya maisha, iwe anataka kuondoa uhai wako kwa ajali mbaya, au moto mbaya, na mengine mabaya yanayofanana na hayo.

Rejea: Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. UFU. 12:4 SUV.

Wakati joka hili linapanga kumla mtoto atakapozaliwa, lilikuwa halijui ulinzi wa Mungu uliokuwepo kwa mwanamke huyo na mtoto wake. Wakati joka linasubiri azaliwe mtoto amle, hilo suala halikuwezekana.

Rejea: Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi. UFU. 12:5 SUV.

Unaona kilichotokea kwa mwanamke huyu, baada ya kumzaa tu mtoto, mtoto alinyakuliwa na Mungu, maana yake ule mpango mbaya juu ya kumla mtoto haukufanikiwa kabisa.

Unaweza ukaona ni jinsi gani Mungu wetu alivyo mkuu, yapo mambo anatuepusha bila hata sisi kuona kile kilitopangwa juu ya maisha yako. Na mengine unaona vita vyake kabisa.

Mungu wetu ni mkuu sana, anaweza kufanya mambo ambayo kwa akili ya kawaida au kibinadamu ingekuwa ngumu sana kupata msaada wako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.