Kila mmoja wetu atakufa siku yake ikifika, inaweza isiwe kauli nzuri sana kwako ila kuogopa kufa au kujisikia vibaya unaposikia habari za kufa hakuwezi kubadilisha kitu. Wale watakaobahatika kukutwa hai ile siku ya mwisho napo hiyo ipo.

Lakini kwa ujumla kifo kinaweza kumpata mtu yeyote na muda wowote au siku yeyote, wala hakichagui mtu, awe masikini au awe tajiri njia ni ile ile. Hili tunapaswa kulijua na kuliweka kwenye fahamu zetu, tuwe tunapenda au tuwe hatupendi tunapaswa kuelewa hivyo.

Habari ya kifo inaweza isiwe habari nzito sana kwa wale ambao wamejiandaa kwa hilo au wamelifahamu vizuri, kufahamu kwao kunaweza kusiwasaidie sana ikiwa hawatakuwa na Yesu Kristo mioyoni mwao.

Unaweza ukajiuliza ndugu mbona unaongelea sana mambo ya kufa, acha tuyaongelee ili tuweze kukumbushana yale yanayotupasa kufanya mapema kabla tupo hai.

Kufa ukiwa na Yesu Kristo ni jambo la msingi sana, na ukawa mtu unayeishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu wako, siku itafika utaona ni heri ya wokovu wako.

Rejea: Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. UFU. 14:13 SUV.

Kama kuna jambo la kujivunia kama wakristo ni kumwamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako una heri nyingi sana. Maana Biblia inaeleza kwa uwazi kuhusu wale wanaokufa katika Kristo.

Maana wanaokufa katika Bwana wanaenda kupumzika baada ya tabu nyingi duniani, na yale matendo yao mazuri yatafuatana nao. Ni raha ilioje kufa katika Bwana, ni raha kubwa sana, tamani sana kufa katika Bwana.

Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com