
Nikitamka mnyama bila kutaja ni mnyama wa aina gani tayari kwenye akili yako utakuwa umepata picha ya wanyama kadhaa unaowafahamu kwenye kichwa chako.
Nikitamka ndege wa angani, kabla sijakutajia ni aina gani wa ndege tayari kwenye akili yako au ufahamu wako unakuwa una picha kadhaa za ndege wa angani.
Kila mnyama unayemfahamu wewe kwa jina lake, awe analiwa nyama au awe asiyeliwa nyama kabisa, unapaswa kuelewa kuwa kazi ya kuwaita majina yao. Haikuwa ya mnyama, bali ilikuwa ni kazi ya mwanadamu.
Ndege wote wa angani unaowafahamu na usiowafahamu wewe, kazi ya kuwaumba ilikuwa ya Mungu mwenyewe isipokuwa kazi ya kuwaita majina yao. Kazi hiyo ilikuwa ni mwanadamu.
Rejea: BWANA Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. MWA. 2:19 SUV.
Unapata picha gani katika hili? Ukiwa na utulivu na kulifanya hili kama tafakari yako, unaweza kuibua kitu chochote kikubwa sana. Kitu ambacho kitakuwa alama kizazi hadi kizazi.
Kwanini nakueleza haya yote, ninachoweza kukumbusha ni kwamba uwezo ulionao ni mkubwa sana na upo ndani yako, alichoweka Mungu ndani yako hakiwezi kufananishwa na mnyama wala hakiwezi kufanya kazi za kiwango cha chini.
Mungu ametupa uwezo mkubwa sana ndani yetu, uwezo ambao tukiutumia vizuri tunaweza kufanya mambo makubwa sana ya kumtukuza Yesu Kristo, mambo ambayo yatalifaa kanisa na jamii kwa ujumla.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com