Yapo mambo ambayo Mungu alitukukataza kufanya, tena ametupa tahadhari mapema kupitia neno lake. Lakini pamoja na kufahamu jambo fulani Mungu halitaki ulifanye, ndilo shetani anakutengenezea mazingira ya kulifanya.

Wale watu ambao shetani amekuwa akiwatumia kama mawakala wake, wamekuwa wanawadanganya watu wengi sana kutenda dhambi.

Tena lile unalolifahamu ni kosa mbele za Mungu, unaambiwa lifanye tu hakutakuwa na tatizo lolote katika hilo.

Mfano binti anaambiwa kwanini huna mwanaume, jibu anakuwa nalo kabisa la kuwa hapaswi kutembea na mwanaume hadi atakapoolewa. Lakini shetani atageuza kibao na kumwambia unakosa mambo mazuri sana.

Hiyo sauti ya unakosa mambo mengi na mazuri sana, tena inakukuta katikati ya changamoto fulani inayohitaji msaada wa wakati huo.

Haya tunajifunza kupitia Eva, nyoka anamgeuzia kibao upande wa pili kumwonyesha kile alichokatazwa na Mungu ni kitu kizuri sana kukitumia.

Rejea: Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. MWA. 3:4‭-‬5 SUV.

Ukishafika hatua kama hii, yaani kuanza kuona kufanya lile alilolikataza Mungu ni zuri sana kwako ujue umeshindwa na adui kwa uchanga wako wa kiroho.

Hawezekani Mungu kusema usiibe akiwa na maana ukiiba utafaidika na mambo mengi mazuri sana, huko ni kukosa maarifa sahihi ndio maana wakati mwingine tunafanya.

Mungu atusaidie sana tujue kuwa Mungu ameshaweka mambo yote kwenye mpangalio mzuri, mpangalio wenye kuleta uhai kiroho na kimwili.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com