
Unaweza kujitoa sana kwa Bwana kwa moyo wako wote, kujitoa kwako sio kutaka watu wakuona kuwa wewe ni mtu unayejitoa sana kwa mambo ya Mungu. Kujitoa kwako kunakuwa hakuna unafiki ndani yake, hata Mungu anapokutazama anabarikiwa na vile unavyojitoa kwake.
Inafika wakati Mungu anakubariki kwa utoaji wako wa muda kwa ajili ya jina lake, wale ambao mlikuwa nao pamoja katika huduma fulani. Kwa kuwa hawakuwa wakijitoa kwa moyo wa kumpendeza Mungu wao, Mungu anaamua kukubariki wewe kwa baraka za kukutosha.
Wale sasa uliokuwa nao pamoja alafu wakawa hawajabarikiwa kama wewe, au hawajapata kibali kutoka kwa Mungu kama wewe, wanaweza kukuchukia kiasi kwamba ukashindwa kuelewa ni nini kimetokea katika maisha yako.
Hili linaweza kukutokea mahali popote pale ukiwa umesimama vizuri na Mungu wako, inaweza ikawa ofisini unapofanyia kazi. Usifikiri utakapobandishwa daraja la juu zaidi kutokana na bidii yako, ukategemea marafiki zako wote mliokuwa nao daraja moja watafurahia hilo.
Kubarikiwa kwako au kuinuliwa kwako au kupata kwako kibali cha Mungu, kunaweza kukusababishia kifo, ndio kunaweza kuleta mauti kwako usipokuwa makini. Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, ni tukio lililompata Habili.
Rejea: Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake. MWA. 4:4 SUV.
Sadaka za Habili kupata kibali kwa Mungu, halikuwa jambo la kumfurahisha ndugu yake Kaini, hakupenda kabisa na kupelekea kukasirika sana, uso wake ulikuwa umeonyesha kukunjamana.
Rejea: Bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. MWA. 4:5 SUV.
Nataka utazame hapo nilipopakolezea wino, unaweza ukajiuliza Habili alimkosea nini haswa Kaini, hakuna kosa lolote isipokuwa sadaka ya Habili ilivyokuwa njema mbele za Mungu na kupokelewa ikaleta shida kwa ndugu yake.
Unaweza ukasoma usione uzito sana wa hili ila Roho Mtakatifu akikupitisha katika mazingira tunayoishi, unaweza ukapata somo kubwa sana la kukusaidia kujua mambo ambayo yangekuwa magumu mwanadamu kukupa majibu yake kirahisi.
Usije ukashangaa kuinuliwa kwako na Mungu ikakuletea mambo ambayo ni mabaya kwako, wala usije ukashangaa watu kutaka kukuangamiza kabisa maisha yako. Wapo akina Kaini wanatenda kazi hata leo, watu wasiopenda kuona tukibarikiwa au tukiinuliwa tulipokuwa kwenda hatua nyingine.
Mungu akusaidie kukabiliana na hali kama hizi zinapokukuta kwenye maisha yako ya kimwili na kiroho, maana wakati mwingine wanaweza wakawa ndugu wa kimwili na wakati mwingine wanaweza wakawa ndugu wa kiroho.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com