
Wazazi wetu wanaweza wakawa hawajafika viwango fulani vya mafanikio katika maisha yao, lakini baada ya kukuzaa wewe wakatamka neno la kinabii kwako. Neno ambalo litakuja kutimia katika maisha yako.
Wazazi wengine wanaweza wasijue sana hili na ikawa hawajatamka neno lolote kwa mtoto, inaweza kwa kutokujua au inawezekana wanaona wamezaa mtoto kama watoto wengine.
Pamoja na kutokujua kwao, makanisa mengi nimeona wana utaratibu wa mtoto kuwekewa mikono na wachungaji au watumishi wa Mungu. Watenda kazi hawa wa Mungu huwa wanatamka maneno mazuri kwa mtoto.
Usipoelewa unaweza ukaona ni maneno tu ya kawaida, lakini ukifuatilia kwa ukaribu huyo mtoto anakuja kuwa kama vile alivyotamkiwa na watumishi wa Mungu.
Sema hili linaweza likawa jambo gumu kwa wengi kutokana na kutoweka kumbukumbu za muda mrefu kwa kila mtoto tunayemzaa au kila mtoto anayetamkiwa maneno ya baraka na watumishi wa Mungu.
Unaweza ukahangaika kwa tabu nyingi sana kumlea na kumsomesha mtoto wako, lakini tabu zako zote ulizopata Mungu anakuja kuleta faraja kupitia kwa mtoto wako.
Unaweza ukanyanyaswa sana na watu mbalimbali au ndugu zako, lakini kupitia mtoto wako, anakuja kuwa faraja na ukasahau manyanyaso na dharau ulizokuwa ukipitia kipindi nyuma.
Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, Nuhu alipozaliwa moja kwa moja tunaona akionekana kuja kuwa faraja, kwa kuwa wazazi wake walifahamu hili hata malezi yake lazima yawe mazuri kiroho na kimwili.
Rejea: Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA. MWA. 5:29 SUV.
Haleluya, nimependa hii sentensi inayosema hivi; Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA.
Ukiwa kama mzazi au ukiwa kama mzazi mtarajiwa unapaswa kuelewa hili na kuwa mwangalifu kwa mtoto, unapaswa kumwombea na kumlea katika njia impasayo kuenenda.
Mtoto wako anaweza kuja kuwa mtumishi wa Mungu ambaye atarejesha ule uhusiano wa watu na Mungu uliopotea kwa miaka mingi, kule kuja kuhubiri injili ya kweli ndio kuwarejesha kwenyewe huko.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu kila siku, unapata maarifa ya kukusaidia katika maisha yako ya kimwili na kiroho, huwezi kuwa mtu wa kawaida kawaida tu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081