
Ni swali ambalo linaweza kuonekana geni kwako, au ni swali ambalo limekuwa likikusumbua wengi kwa muda mrefu bila kuwa na majibu yake. Kutokana na wakati ulionao alafu huoni mrithi wa jambo lako au huduma unayofanya.
Huenda hukuwahi kabisa kujiuliza swali kama hili, limekuwa ni swali geni kwako, hukujua kama unapaswa kuwa na mtu ambaye atakuwa mrithi wa kile ulikuwa nacho, au kwa kile ulikuwa unafanya katika maisha yako.
Inawezekana ni mali zako, unazo mali za kutosha ila huna mtoto wa kurithi mali zako, umesubiri sana mtoto ila umri wako umeenda sana bila mafanikio ya kupata mtoto.
Huenda wewe huna changamoto ya mtoto, unao watoto wa kutosha kabisa ila ukiangalia atakayekuwa mrithi wako na atakayeendeleza kile unatamani akiendeleze pindi upo na pindi utapokuwa haupo. Huoni kabisa mtoto wa kufiti kwenye nafasi ambayo unataka akae.
Jambo hili limekuwa likiumiza vichwa wengi sana, hasa wale ambao wamelitambua hili mapema kabla Mungu hajawachukua, limekuwa ni swali ambalo linahitaji majibu mazuri yenye kibali mbele za Mungu.
Wapo wengine hawajaokoka ila na wao wanatafuta mrithi wao, unaweza kuona ni jinsi gani hili jambo ni muhimu sana kulifikiri mapema na kulifanyia kazi mapema kabla hujaacha kile ulikuwa unafanya na ulitamani umkabidhi/umwachie mrithi wako.
Hili tunajifunza kupitia Ibrahim, alifika wakati akamuuliza Mungu kuhusu mrithi wake, linaonekana ni jambo ambalo lilikuwa linautesa moyo wake. Kama inavyoweza kuwa kwako au kwa mtu mwingine.
Rejea: Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? MWA. 15:2 SUV.
Wakati huu Abram hakuwa na mtoto, sasa anauliza mrithi wa nyumba yake atakuwa Eliezeri, Mdameski? Kwa maana nyingine halikuwa jambo linaloubariki moyo wake.
Tunakuja kuona kwenye mstari unaofuata Mungu akimjibu Ibrahim kuwa huyo Eliezeri hatakuwa mrithi wake, bali mtoto atakayetoka kwenye viuno vyake mwenyewe.
Rejea: Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. MWA. 15:4 SUV.
Hili ni somo kubwa sana kwetu wenye maswali kama haya ya Abramu, kwanini ni somo kubwa? Kwa sababu tunapojikuta tunatatizwa na jambo kama hili tunapaswa kumwendea Mungu kumuuliza.
Unaweza usiwe na shida na mtoto wa kimwili atakayekuwa mrithi wako, ukawa na shida na mtoto wa kiroho atakayerithi kundi ulilokuwa unaliongoza baada ya wewe kuondoka.
Tunapaswa kufuata njia ile ile aliyoipitia Abram wakati yupo kwenye kipindi kigumu cha kujiuliza kuhusu mrithi wake atakuwa nani, neno la BWANA likamjia kumpa jibu la swali lake.
Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku maana lina majibu ya maswali yako uliyonayo katika maisha yako, haijalishi unaona limekuwa ni swali ambalo limekosa majibu yake kwa muda mrefu. Amini majibu yake yapo kwenye Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081