Yapo mambo tunamwomba Mungu wetu na anajibu kwa wakati, na zipo ahadi za Mungu ambazo ametuahidia katika maisha yetu nazo tunaziona zikitimia kwa wakati wake, na tunaziona na kuzifurahia sana.

Yapo mambo mengine tunamwomba Mungu lakini majibu yake bado hatujayapokea, siku za mwanzo tulikuwa na moyo wa subira na kuona Mungu atatujibu tu kwa wakati wake. Badala yake muda unaonekana kwenda sana na ule moyo wa subira unakuwa haupo tena.

Kama binadamu hali kama hii inaweza kumtokea mtu yeyote yule, hata yule ambaye uhusiano wake na Mungu upo vizuri, kama hatakuwa na uvumilivu na kuendelea kumsubiri Bwana. Shetani anaweza kujitukuza kwa kumkosea Mungu wake.

Tunahitaji kuwa watulivu sana tunapofika wakati ambao tunaona muda wetu umeenda sana, sio muda tu, hata umri wetu unakuwa umeenda sana. Yale matarajio yetu kutoka kwa Mungu yanakuwa hayapo tena, hapa tunahitaji kumsikiliza sana Roho Mtakatifu.

Mungu kukuahidi jambo au kukuambia atakupa jambo fulani, sio wakati wote hilo jambo litapatikana kwa wakati unaoutamani/unaoutarajia wewe. Wakati mwingine majibu ya maombi yako au ahadi zako kutoka kwa Mungu huwa zinachelewa.

Hili liliwakumbuka akina Abram na Sarai, walifika wakati wakakata tamaa juu ya habari ya kupata mtoto, Sarai akaanza kumshawishi mume wake azae na kijakazi wake. Abram naye alimsikiliza mke wake, akakubali kulala na kijakazi ili wapate mtoto.

Rejea: Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. MWA. 16:2 SUV.

Sarai hili jambo lilikuja kuleta shida kwake, kijakazi wake alivyolala na mume wake Abram, dharau zilianza kwa kijakazi wake, hili halikuwa jambo jema kwa Sarai.

Rejea: Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. MWA. 16:3‭-‬4 SUV.

Unaona matokeo ya kuchukua maamzi yasiyofaa, kwa sababu ya kuchelewa kupata majibu ya maombi yake au matarajio yake? Hapa tunapaswa kumwomba Mungu sana atusaidie katika eneo hili tunapofika mahali tunaona haiwezekani tena.

Rejea: Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. MWA. 16:5 SUV.

Badala ya kuwa baraka katika nyumba ya Abram na Sarai pakawa na shida nyingine tena, afadhali wangekuwa vile vile. Wakasababisha mambo ambayo yasingetokea kama wangekuwa na subira.

Chunga sana majibu ya maombi yako yanapochelewa kujibiwa, kuchukua maamzi yasiyofaa mbele za Mungu yanaweza kukugharimu maisha yako yote. Ama yanaweza kugeuka majuto makubwa katika maisha yako ya kimwili na kiroho.

Ndio maana ni muhimu sana kuendelea kulisha moyo wako Neno la Mungu kila siku, kuna mahali bila kuwa na neno la Mungu hutaweza kuvuka. Unahitaji kujaa neno la Mungu usije ukamtenda Mungu wako dhambi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081