Kuna vitu kusikia kitafanyika kwako unaweza usiamini haraka sana kutokana na unavyofahamu kwa akili ya kibinadamu kuwa haiwezekani kutokea/kutendeka jambo kama hilo.

Yapo mambo mengine unaweza usiamini haraka hata kama umeokoka kutokana na uelewa wako wa shule, na kwa mjibu wa vipimo vinaonyesha kabisa haiwezekani kutokea jambo kama hilo.

Pamoja na madaktari wamesema kitaalamu haiwezekani, pamoja na ufahamu wako unakutuma kwamba jambo ulilolitamani muda mrefu halitaweza kutokea kabisa.

Kufikiri kwako hivyo hakuwezi kubadilisha Neno la Mungu, maana kwa Mungu hakuna jambo lolote lile lisilowezekana kwake. Japo tunaweza kubaki kusema kwa mazoea ila tunapaswa kuamini hakuna lisilowezekana kwake.

Ibrahim alikuwa haamini kama Sara anaweza kumzalia mtoto, kutokana na umri wake wa uzee wa miaka 90, miaka tisini unaweza kuitaja kishabiki au kawaida kabisa ila unapaswa kufahamu jambo lolote lile lisilowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu linawezekana.

Rejea: Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? MWA. 17:17 SUV.

Usimpe Mungu mipaka, ile mipaka tuliyojiwekea wenyewe ibaki kwetu sisi wanadamu ila kwa Mungu yeye hana umri umeenda sana, anaweza kufanya mambo ambayo mwanadamu hawezi kufanya.

Tunao mfano mzuri kabisa wa Ibrahim na Sara, japo Ibrahim alianza kumhoji Mungu baada ya kuahidiwa jambo ambalo aliona kama gumu. Lakini pamoja na hayo yote amini yote yanawezekana kwa Mungu wako.

Rejea: Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. MWA. 17:19 SUV.

Umekaa muda mrefu bila kupata majibu ya maombi yako, amini wakati wake ukifika Bwana atafanya mwenyewe bila kujalisha watu wamesema nini juu ya hitaji lako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com