
Tunaweza kujenga mazoea ya jambo fulani au kila jambo, hata tunapopewa maelekezo juu hilo jambo wakati mwingine huwa hatuyapi uzito mkubwa sana. Zaidi huwa tunayachukulia kawaida kabisa au huwa tunayapuuza maelekezo tunayopewa.
Kwa kuwa tumejenga mazoea na kuchulia vitu kawaida, bila kujalisha yana madhara kwenye maisha yetu, wengi wetu tumejikuta tukipata madhara makubwa sana kwenye miili yetu.
Wengine hatujajenga tabia ya kupuuza maelekezo muhimu, isipokuwa hatujui madhara ya kutozangatia maelekezo muhimu tunayopewa na watu au na Mungu mwenyewe.
Wapo watu wamepuuza maelekezo muhimu kutoka kwa madaktari kuhusu dozi za dawa wanazopewa wameze, wapo imewapelekea kupoteza uhai wao, na wapo imewapelekea kuharibu afya zao.
Wapo watu wamepuuza maelekezo muhimu kutoka kwa Roho Mtakatifu na madhara yake waliyopata ni makubwa sana, hadi yamepelekea majuto katika maisha yao.
Kwa mfano mtu aliambiwa usifanye jambo hilo, sio sauti ya mwanadamu ambayo unaweza kusema ana wivu juu ya maisha yake. Bali ni sauti ya Roho Mtakatifu mwenyewe inayompa maelekezo au inayomwonya, ambapo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza na mtu kwa njia yeyote ile.
Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, tunaona wakwe za binti zake Lutu, wakiambiwa na Lutu mwenyewe waondoke mahali ambapo walikuwa wanaishi. Maana Bwana alikuwa anakuja kupaangamiza.
Rejea: Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze. MWA. 19:14 SUV.
Hawa wakweze walimwona Lutu anawatania, kwahiyo kile alichowaambia Lutu hawakujua ni ujumbe wao kutoka kwa Mungu, badala yake wakamwona kama mtu anayecheza mbele yao.
Madhara yaliyowapata ni kupoteza maisha yao au uhai wao, lakini walikuwa na nafasi nzuri ya kuepuka hicho kifo cha moto. Maana walipata fursa ya kujulishwa kile ambacho kinaenda kutokea mbele yao.
Rejea: Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. MWA. 19:24-25 SUV.
Mwingine aliyepuuza maelekezo muhimu aliyopewa ni mke wake na Lutu, walipewa maelekezo ya kutogeuka nyuma, na wasimame. Lutu na mke wake, na watoto wao wawili kila mmoja wao alipaswa kuzingatia maelekezo waliyopewa.
Rejea: Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. MWA. 19:17 SUV.
Kwa kutozingatia maelekezo waliyopewa, tunamsoma mke wake na Lutu akigeuka nyuma na kuwa nguzo ya chumvi. Sema “nguzo ya chumvi” hii ni kwa sababu alingeuka masharti aliyopewa.
Rejea: Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. MWA. 19:26 SUV.

Sijui kama unanielewa ninachokisema hapa, Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa vizuri haya, ukielewa vizuri itakusaidia sana katika maisha yako ya kimwili na kiroho.
Tumeona makundi mawili hapa, moja kuangamizwa kwa moto, na wa pili kuwa nguzo ya chumvi, kundi la kwanza lilikuwa na nafasi ya kupona na wa pili alikuwa na uwezo wa kutokuwa nguzo ya chumvi.
Na wewe unaweza kupona ikiwa utazingatia maelekezo muhimu unayopewa, sisemi kila maelekezo unayopewa utapaswa kuyafuata/kuyazingatia. Yapo maelekezo ukiyafuata utapotea njia, unapaswa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu ili uweze kuielewa sauti yake.
Ndio maana ya kujifunza kupitia neno lake, na ndio maana ninakukumbusha kila mara kusoma Neno la Mungu kila siku, hii inakusaidia kutoangamizwa kwa kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081