Tuna marafiki zetu ambao tunawaamini, hata wanapotuambia tuwafanyie jambo fulani huwa hatuna mashaka nao sana. Wakati mwingine wanaweza kutuomba fedha tukawapa bila kujiuliza maswali yeyote.

Tunawapa marafiki zetu kutokana na vile tunawafahamu walivyo, hata kama hatujawapa asilimia zote za uaminifu, kiasi fulani hatuna mashaka nao tunapofika maeneo ya kusaidiana kwa yale wametuomba na tuna uwezo nayo.

Tofauti kabisa na wale watu ambao hatuna imani nao au hatuna uhakika nao, wanaweza kutuagiza tuwafanyie jambo fulani badala ya kufanya maswali mengi yanaibuka ndani yetu. Badala ya kufanya tunabaki na maswali na kuona haina haja kufanya kile wametuagiza au wametuomba tufanye.

Vile tunamfahamu mtu, na vile mnakuwa na uhusiano mzuri na kushirikiana kwenye mambo mbalimbali katika maisha yenu, na ukawa na uhakika naye kutokana na matendo yake mazuri. Ni rahisi sana kutii kumfanyia jambo alilokuomba umfanyie.

Ndivyo ilivyo na kwa Mungu wetu, wengi tunashindwa kutii sauti ya Mungu pale anapotuagiza tumfanyie jambo fulani tunakuwa wagumu kufanya kutokana na uhusiano wetu kuwa mbali naye. Ule urafiki wetu na Mungu unakuwa wa kufifia, kama ni wa kufifia au kusuasua ni ngumu kufanya kile anatuagiza.

Tunajifunza jambo kubwa sana kupitia kwa Ibrahim, Ibrahim kutii maagizo ya Mungu ya kumtoa mwanaye mpendwa sadaka ya kuteketezwa. Halikuwa jambo rahisi kama tunavyoweza kusoma, tena ukizingatia alikuwa ni mtoto wake wa pekee kwa mke wake Sara.

Rejea: Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. MWA. 22:2 SUV.

Pamoja na huo upekee hatuoni kwenye biblia Ibrahim akimkatalia Mungu kumtolea mwanaye mpendwa sadaka ya kuteketezwa, ukisoma mwanzo 21 yote unaona kabisa Ibrahim hakuwa akionyesha kukataa au kulazimishwa.

Rejea: Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. MWA. 22:3 SUV.

Hapa hatuoni kusitasita kwa Ibrahim, kile Mungu alisema naye ndicho anaenda kukitekeleza, hakutafuta watumishi wengine wampe ushauri. Wala hakuanza kuwaambia watu wengine, maana hata wale ambao walikuwa wameambatana nao hakuwa wakijua kinachoenda kufanyika.

Hata Isaka mwenyewe hakuwa hakijua chochote kile, baba yake ndiye alikuwa anajua kinachoenda kufanyika eneo la tukio. Ndio maana tunaona kwenye mstari huu Isaka akimuuliza babaye;

Rejea: Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? MWA. 22:7 SUV.

Ndugu yangu tafuta sana kumjua Mungu kupitia Neno lake, hata pale anapotuagiza ufanye jambo fulani kwa ajili yake usiwe na shaka yeyote ile. Tena utafanya bila kutafuta ushauri kwa watu, maana utakuwa unajua aliyesema ni Baba yako wa mbinguni.

Napendezwa sana na utii wa Ibrahim, hadi anafika eneo maalum kwa ajili ya kumtoa Isaka sadaka, akamlaza mwanaye mpendwa tayari kwa kutekeleza agizo kwa hatua ya kumchinja.

Rejea: Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. MWA. 22:10 SUV.

Mungu atusaidie sana tufikie viwango vya namna hii, tutaona baraka za Mungu zikitujia kwa kasi sana kwa kutii tu sauti ya Roho Mtakatifu. Maana yapo mambo mengi tumeyaapuuza Roho Mtakatifu aliposema nasi, hicho ndicho kimepeperusha baraka zetu.

Tunaona Ibrahim akitamkiwa baraka nyingi sana baada ya kushinda mtihani aliopewa na Mungu mwenyewe, mtihani ambao wanaoweza kufaulu ni wale waliokubali kumfuata Yesu kwa miguu yote miwili.

Rejea: katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. MWA. 22:17‭-‬18 SUV.

Haleluya, sababu haswa ya baraka hizi za Ibrahim ilisababishwa na kutii kwake, hii inatuonyesha wazi zipo baraka za Mungu tunaweza kuzipata kwa kutii. Na zipo baraka kutoka kwa Mungu tunaweza kuzikosa kwa kutokutii Roho Mtakatifu.

Wewe usiwe miongoni mwa wasiomtii Roho Mtakatifu, ndio maana umepata nafasi ya kujifunza maarifa haya ya kukusaidia kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081