Zipo nyakati tunakuwa tunapitia katika maisha yetu, nyakati ambazo zinakuwa zinatukosesha raha kutokana na karaha tunazokutana nazo katika maisha yetu ya kila siku.

Inafika wakati mtu anaanza kuwaza labda Mungu alimtaka awe hivyo alivyo na asiwe kama vile anavyotamani kuwa kutokana na kuomba sana bila mafanikio. Japokuwa mtu ni mcha Mungu anafika mahali anaona kabisa jambo hilo haliwezekani tena kwake kutokana na umri wake kwenda sana.

Bila shaka umewahi kukutana na watu ambao umri wao umeenda sana, na bado hawajaolewa, wengi wao huwa wamejikatia tamaa kabisa. Hata unapomwambia Mungu bado anaweza kufanya jambo, anaweza asikuelewe kwa haraka.

Kuna hatua watu wamefika hawana tena matumaini na kile walichokuwa wanakitamani sana miaka mingi ya nyuma, wanaona uwezekano wa kukipata hicho kitu ni mdogo sana kwao.

Pamoja na hayo yote, yaani uwe umepoteza tumaini na kile ulichomwomba Mungu miaka mingi, haijalishi umri wako umeenda sana, wala haijalishi miaka mingi sana imepita. Elewa Mungu bado anaweza kufanya jambo lile lile ulilomwomba miaka mingi.

Mungu anaweza kukufanya uwe na kicheko kikuu kwenye maisha yako ya uzee, au kwenye maisha yako ya utu uzima wako. Ukimtukuza Mungu na kumshuhudia matendo yake makuu, na wale watu waliokuwa wanakufahamu wakatamani kumfahamu Mungu unayemwabudu.

Ndivyo ilivyomtokea Sara, baada ya miaka mingi sana kupita, yaani baada ya kupita usichana wake bila mtoto, mtoto alikuja kupatikana uzeeni. Tena ule uzee haswa, ambao kitaalamu ilikuwa haiwezekani kushika mimba na kuzaa mtoto.

Rejea: Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. MWA. 21:6‭-‬7 SUV.

Mungu aliyetenda kwa Sara na akamfanyia kicheko, hata kwako anaweza kutenda, yale yanayoonekana yameshindikana kibinadamu kwake hakuna mahali anasema haiwezekani. Kwa Mungu yote yanawezekana kwake.

Rejea: kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Luka 1:37 SUV.

Sijui kama unakubaliana na hili andiko linavyosema, hata kama hukubaliana nalo unapaswa kufahamu kwamba hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Ukubali au ukatae, hakuna lisilowezekana kwake.

Lipo jambo unatamani Mungu akutendee katika maisha yako, endelea kuwa na imani kwake ipo siku atakutendea, haijalishi umri wako, uwe na uhakika atakutendea katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com

Wasap: +255759808081