Miongoni mwa njia ambazo zinaweza zikatupa majibu sahihi juu ya rafiki, mzazi, mke, mume, kaka, dada, ama ndugu yeyote yule ni kumtazama usoni.

Unapokutanisha macho yako na baba yako, mama yako, mume wako, mke wako yanaweza kukupa majibu ya maswali yako au yanaweza kukupa maswali mengi zaidi.

Nyuso zetu huwa zinazungumza kabisa kile kilichojaza mioyo yetu, kama mtu ana hasira/chuki na wewe unaweza kumtambua mnapokutanisha macho yenu. Wakati mwingine anaweza akashindwa kukutanisha macho yenu ila kwa kumtazama na kumsemesha unaweza ukatambua jambo.

Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, Yakobo alimtambua Labani kuwa hayupo sawa kwa kumtazama usoni, alimtambua sio yule wa jana na juzi.

Rejea: Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi. MWA. 31:2 SUV.

Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. MWA. 31:5 SUV.

Ukitaka kuthibitisha hili jaribu kuchunguza utaona hichi ninachokueleza hapa, hasa watu wako karibu mnaofahamiana nao, jenga utaratibu wa kuwatazama usoni wakati unazungumza nao.

Yapo mambo utagundua haraka, maana uso huwa hufichi kile kilichoujaza moyo wako, kama mtu ana hasira na wewe utamtambua kwenye uso kabla ya mambo mengine.

Ukitaka kujua uliyemwomba msamaha amekusamehe au bado hajakusamehe, usitafute mambo mengi wewe cha kufanya ni kumtazama usoni. Utajua umesamehewa au bado hujasamehewa.

Ukitaka kujua mchumba uliyenaye bado mpo pamoja au ameshakuacha mtazame usoni, utafahamu mambo mengi sana hata yale ambayo hukuyasikia akisema kwako.

Ukitaka kujua mume au mke wako mpo vizuri naye au hampo vizuri naye, jenga utamaduni wa kumtazama usoni, utagundua ana furaha na wewe au ana hasira na wewe.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu kila siku, mambo ambayo ulipaswa kukaa darasani miaka mingi, unayapata kwa njia ya kutenga muda wako wa kusoma Biblia na kutafakari kile umejifunza.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com