
Jambo hili huwa linawasumbua vichwa baadhi ya watu, huwa wanafika mahali wanashindwa wachukue maamzi yapi wanapofika mahali wanapewa zawadi ya kitu walichonacho.
Mtu mwingine anaweza kuona haina haja kupokea zawadi ambayo tayari anayo, kufikiri hivyo wengi wamekuwa wakikataa zawadi nyingi.
Kwanza tunapaswa kuelewa kuwa hadi mtu akuletee zawadi kwako, sio suala ambalo amekurupuka. Amekaa akafikiri sana na kuona zawadi inayokufaa ni hiyo aliyokuletea.
Hili ni la kuheshimu sana, haijalishi una vitu vingi sana vinavyofanana na hivyo unavyopewa, unachopaswa kufanya ni kupokea.
Kukataa kupokea zawadi kwa kutoa sababu ya kuwa unavyo au unacho hicho unachotaka kupewa, huko ni kukosa maarifa sahihi ya kiMungu.
Hili tunajifunza kupitia kwa Yakobo, wakati amemwandalia ndugu yake zawadi nzuri aliyoona moyoni mwake itamfaa. Esau alikataa kuipokea hiyo zawadi na kumweleza kuwa anayo.
Rejea: Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. MWA. 33:9 SUV.
Sasa mara nyingi zawadi huwa zimebaba jambo fulani kwa mtoa zawadi, mtu anaweza akawa anataka kupokea baraka za Mungu kupitia kukupa wewe zawadi.
Mwingine anaweza kukupa zawadi kwa nia ovu, lakini Roho Mtakatifu akiwa ndani yako anaweza kukusaidia usipokee hiyo zawadi.
Zawadi wakati mwingine inaweza kukupa majibu ya maswali uliyokuwa unajiuliza kuhusu ndugu yako au rafiki yako au jirani yako.
Yakobo alimweleza wazi kabisa ndugu yake Esau, kama amekubalika machoni pake apokee zawadi yake aliyomletea. Na kama unakumbuka Esau alizikosa baraka za mzaliwa wa kwanza kwa baba yake Isaka kwa kuwahiwa na Yakobo.
Rejea: Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. MWA. 33:10 SUV.
Hapa inatufundisha pia tusiwe watu wa kukubali haraka kushindwa kwa jambo ambalo lina faida katika maisha yetu ya kiroho au kimwili.
Yakobo hakukubali haraka ndugu yake asichukue zawadi aliyomletea, alimpa hoja ya kumfanya athibitishe kuwa hana kinyongo na Yakobo.
Mwisho tunaona Esau alikubali kupokea zawadi aliyoletewa na ndugu yake Yakobo, hii ilikuwa ni hatua kubwa ya mafanikio kwa Yakobo.
Rejea: Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea. MWA. 33:11 SUV.
Vitu vingine utafanikiwa kwa kumshurutisha uliyemlenga, bila kumshurutisha unaweza usifanikishe kila ambacho ulitamani kiwe.
Hili tunajifunza kupitia maandiko ya biblia, tunaona Yakobo alimshurutisha ndugu yake Esau hadi akapokea zawadi yake aliyomletea. Bila kujalisha alidai anavyo vile alivyovitaka kumpa.
Kama hukuwahi kukutana na hili, elewa katika maisha yako unaweza kukutana na hili lisije likawa shida kwako, kuwa na maarifa sahihi kama haya itakusaidia kuamua vyema.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com