Kutengana sio mara zote ni kwa vibaya, kutengana kwingine huwa kunaletwa na mambo ya heri kabisa, mambo ambayo yanawafanya msiweze kukaa tena mahali pamoja.

Wengine wakisikia ndugu na ndugu wametengana wanaweza kuchukulia watakuwa wamefarakana wenyewe kwa wenyewe, sio kana kwamba ni jambo ambalo halipo. Hapana, mambo kama hayo yanakuwepo kabisa katika familia au katika jamii.

Watu kutengana hakupaswi kuchukuliwa kwa hasi, kunapaswa kuchukuliwa kwa chanya pia, ambapo leo tunaenda kujifunza hasa upande wa chanya. Ambapo ndugu au marafiki wanakuwa wametenganishwa kwa jambo la heri.

Katika maisha tunaweza tukawa pamoja, lakini kadri kila mmoja anavyozidi kufanikiwa katika maisha yake, itawazalimu kutengana, yaani kila mmoja wenu kuwa na sehemu yake ya kuishi.

Inawezekana mwanzo mlikuwa eneo moja la makazi na kila mmoja akawa na mali zake za kutosha tu, ile nafasi mliyokuwa nayo mwanzo inakuwa haitoshi tena na itambidi mmojawapo aondoke.

Hili tunajifunza kwa Esau na Yakobo, Esau baada ya kuona mifungo yake imekuwa mingi na ndugu yake Yakobo naye imekuwa mingi. Esau aliamua kukusanya kila kilicho chake kwenda nchi nyingine iliyo mbali na Yakobo.

Rejea: Esau akawatwaa wakeze, na wanawe, na binti zake, na watu wote wa nyumbani mwake, na ng’ombe zake, na wanyama wake wote, na mali yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani; akaenda mpaka nchi iliyo mbali na Yakobo nduguye. Maana mali yao yalikuwa mengi wasiweze kukaa pamoja, wala haikuweza nchi ya kusafiri kwao kuwachukua, kwa sababu ya wanyama wao. MWA. 36:6‭-‬7 SUV.

Hali kama hizi zinapowapata ndugu wengi huwa hawazikubali sana, na anapotokea mmojawapo anataka kuondoka huwa zinaibuka tafsiri mbovu juu ya huyo anayetaka kujitenga.

Kwa kuwa wewe unajifunza hapa unapaswa kuelewa kwamba utafika wakati mafanikio yenu makubwa yanaweza yakawagawa kwa nia njema kabisa. Usianze kumfikiri ndugu yako vibaya kwa kukupa taarifa ya kwenda kuishi mahali pengine.

Na wewe usianze kufikiri ndugu yako labda atakufikiriaje kwa kujitenga kwako na yeye, katika maisha hayo yapo. Kupeana nafasi inatufanya tukue zaidi ya tulivyokuwa mwanzo ila kuendelea kubanana inawafanya msikue zaidi.

Hili linaingia maeneo mengi sana katika maisha yetu, linaingia kwa mambo ya kiroho na kimwili, mnaweza mkawa pamoja katika huduma, lakini mnavyozidi kukua kihuduma itafika mahali ambapo mmoja wenu atataka akafanyie huduma eneo lingine tofauti.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, unapata maarifa sahihi ya kukusaidia kuishi maisha ambayo hayana maulizo mengi yasiyo na majibu yake sahihi. Lakini Neno la Mungu likiwa ndani ya moyo wako unakuwa huru kwenye maeneo mengi sana katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com