Tukiwa kama wazazi tuliopata neema ya kupata watoto wa kuwazaa, tunapaswa kuwa makini sana katika hili la kuonyesha upendo wa wazi kwa mtoto mmoja.

Bila kufanya hivyo tunaweza kujikuta tumesababisha madhara makubwa kwa mtoto ambaye tunaonyesha upendo wa wazi kwake.

Unapaswa kuelewa kuwa upendo kwa mtoto au watoto wako sio mbaya, isipokuwa unaweza kuleta shida pale unapoonekana unampanda sana mtoto wako mmoja.

Uzuri wa upendo huwa hujifichi, mzazi kuficha hisia zake za upendo kwa mwanaye linaweza likawa jambo gumu sana kwake.

Sifa mmoja wapo ya upendo huwa hujifichi, kwa kuwa hujifichi huwa unaambatana na matendo ya wazi.

Kwa kuwa unaambatana na matendo ya wazi, mtu atajikuta anamfanyia yule anayempenda vitu vya tofauti kabisa.

Kama mzazi ana watoto 5, na ikatokea mzazi akampenda mtoto wa mwisho. Upendo wake utaonekana kwenye kumnunulia vitu mbalimbali.

Kaka zake au dada zake wanapoona mdogo wao anapendwa zaidi na mama/baba yao, uwe na uhakika chuki itaingia. Labda wawe wameokoka na wamekomaa kiroho, na kama wameokoka kutakuwa na kitu hakipo sawa.

Ukiwa kama mzazi mwenye watoto au ukiwa kama mzazi mtarajiwa na unasoma hapa. Unapaswa kuwa makini na hili.

Kumpenda mtoto mmoja inaweza kutokea kutokana na matendo mazuri ya huyo mtoto, au kutokana na sifa njema za mtoto.

Huenda ni msikivu zaidi ya wenzake, au huenda anakusikiliza zaidi ya wenzake, na huenda ni mcha Mungu zaidi ya wenzake.

Hii inatosha kabisa mzazi kumpenda mtoto mwenye sifa hizi na zaidi ya hizi, tena ukute mtoto ni wa kwanza au wa mwisho. Hapo utajua kabisa huyu mtoto anapendwa na mzazi wake.

Hili tunajifunza kwa Yakobo/Israeli, alimpenda zaidi Yusuf kuliko watoto wake wengine.

Rejea: Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. MWA. 37:3 SUV.

Kama nilivyoanza kukuambia upendo huwa hujifichi, tunaona Israel akimtengenezea Yusuf kazu. Hili lilikuwa vazi la heshima kwa Yusuf.

Shida haikuwa kumpenda, shida ilikuja kwa ndugu zake, walimchukia sana Yusuf baada ya kuona anapendwa zaidi na baba yao.

Rejea: Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. MWA. 37:4 SUV.

Sijui kama unanielewa hapa, unaweza usielewe sana ila naomba Roho Mtakatifu awe mwalimu wako. Maana yeye anaweza kukusaidia kuelewa kwa njia rahisi zaidi.

Chuki hii tunaiona iliingia hadi kwa mambo ambayo yalikuwa mazuri, hata pale alipowashirikisha kuhusu ndoto yake. Walizidi kumchukia zaidi na kupanga njama za kumuua.

Rejea: Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. MWA. 37:19‭-‬20 SUV.

Chunga sana hii ukiwa mzazi, kumpenda mtoto mmoja kuliko wenzake tena kwa uwazi kabisa. Kama huwezi kujizuia kumpenda mtoto wako, mwombee sana mtoto wako.

Na mara nyingi watoto wa namna hiyo Mungu huwa ameweka kitu cha namna ya pekee kwa ajili ya utukufu wake.

Chuki kwa Yusuf haikuanza kwenye ndoto yake, ilianzia pale baba yake alipoonyesha kumpenda. Hapo ndipo kilipoanzia chanzo cha mambo yote.

Bila shaka kipo umejifunza kupitia ujumbe huu, nikualike katika usomaji wa neno la Mungu kila siku kama bado hujajiunga na kundi la chapeo ya wokovu. Wasiliana nasi kwa wasap namba hiyo chini.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
+255759808081