Zipo nyakati tunaweza kupita pagumu sana, nyakati ambazo zinakuwa ngumu hata kumwelezea mtu. Na kama unaweza kumwelezea anakuwa hana msaada sana kwako.

Wakati tunapitia nyakati kama hizo, mara nyingi huwa tunabaki na upweke fulani hivi wa kukosa usingizi, ama wa kukosa watu wa kuwa nao karibu.

Tunapobaki wenyewe, tunakuwa na Mungu pekee, muda mwingine tunaweza kubaki kumuuliza Mungu mbona watu hawapo pamoja nasi?

Kipindi kama hichi tunapopitia, ni kipindi ambacho ni kigumu kwetu ila kwa upande mwingine kinakuwa na mafunzo mengi sana katika maisha yetu ya kiroho na kimwili.

Unaweza usielewe sana wakati unapitia kwenye changamoto ngumu ila utafika wakati utaona faida yake.

Huenda upo kwenye kipindi cha majonzi makubwa sana, umekuwa mtu ambaye unaishi ilimradi siku ziende.

Ninachoweza kukuambia leo, amini upo wakati Mungu atakusahaulisha taabu zako zote, ndio Mungu atakusahaulisha taabu zako zote saa ikifika.

Rejea: Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu. MWA. 41:51 SUV.

Hili tunajifunza kupitia maandiko, baada ya mapito magumu ya Yusuf ilifika wakati Mungu akamsahaulisha taabu zake zote.

Ambapo hata wewe unayesoma ujumbe huu, itafika mahali ambapo utasahaulishwa taabu zako zote na kustarehe katika Bwana.

Usitishwe sana na hali unayopitia sasa, ipo siku Bwana atakafuta majonzi, endelea kuweka tumaini lako kwake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081.