Kuna maeneo fulani tunakuwa wenyeji wa muda mrefu, tunakuwa tunaelewa taratibu zinavyoenda, tofauti kabisa na mtu ambaye ni mgeni.

Kama sio wenyeji tunakuwa tuna uzoefu nayo hayo maeneo au hiyo sehemu, uzoefu ambao watu wengine wanakuwa hawana kabisa. Lakini sisi tunakuwa nao.

Sasa wewe kama mgeni ni vizuri kusikiliza utaratibu wa mahali hapo pa ugeni kwa mwenyeji wako, ni vizuri kuuliza utaratibu wa hapo huwa ukoje.

Kuna mtu unajua kabisa huwezi kuzungumza naye, vizuri kumtumia yule ambaye unajua anaweza kuongea naye akakufikishia ujumbe wako.

Tunajifunza kwa Yusuf, familia yake ilipofika Misri, baada ya mapokezi na kufurahiana, aliwapa darasa namna ya kumjibu Farao atakapowauliza.

Rejea: Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri. MWA. 46:33‭-‬34 SUV.

Hii inaonyesha wazi kabisa hakutaka ndugu zake wakosee, pia alikuwa anaelewa swali kama hilo linaweza kujitokeza. Kwahiyo likijitokeza watakuwa na la kujibu mbele ya Farao.

Linaweza lisionekane jambo la muhimu sana kwako, ama linaweza ukaliona sio jambo la kiroho sana. Lakini unaweza ukafikiri, mambo mangapi uliwahi kukosea kujibu?

Unaweza kukumbuka ni mambo kadhaa, na ulivyokosea akatokea mtu anakuambia huyo mtu huwa haendewi hivyo ungemwendea hivi, au huyo mtu hukupaswa kumjibu hivyo ulipaswa kumjibu hivi.

Hii itatusaidia sana tunapotaka kuonana na viongozi wetu wa kiroho au kimwili, inatupa kujiandaa, na sio inatupa nafasi ya kudanganya, kumbuka hilo.

Una uzoefu mahali fulani, usiwe kimya, wape maelekezo muhimu wageni wako, utaratibu wa mahali husika ni muhimu sana ukafahamika.

Ukitaka kuelewa kuwa Yusuf alikuwa anaelewa vizuri kile ambacho ndugu zake wanaenda kukutana nacho kwa Farao, soma hapa;

Rejea: Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao. Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu. Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni. MWA. 47:2‭-‬4 SUV.

Hata leo tunapaswa kufanya kama Yusuf, itamsaidia sana yule anayeenda kwa kiongozi, akiulizwa ataenda moja kwa moja kwenye majibu yaliyo nyooka.

Hii ndio faida ya kupata maarifa kama haya, unakuwa unajua namna ya kufanya pale unapokutana na watu wanataka kumwona boss wako, na hautaki walikose lile wanalohitaji kwake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com