Hili tumeliona sana kwenye maisha yetu ya kila siku, mtu anakwambia atakufanyia jambo fulani. Lakini anakuja kushindwa kukufanyia kama alivyokuahidi.

Mtu huyu aliyekuahidi anaweza akawa aliongea tu kuepuka usumbufu aliokuwa anapata kwa aliyemwahidi atamfanyia jambo au kitu fulani. Lakini aliyeahidiwa anakuja kuona hakutendewa vile aliahidiwa, hajui kuwa kilichomfanya ahaidiwe ni ule usumbufu wake.

Wapo watu bado hawajajua kusema hapana au haiwezekani, wanaona kusema hivyo watamuumiza wanaomwaambia, kwahiyo wanaitikia tu bila kujalisha wanaweza kufanya ama hawawezi kufanya.

Pamoja na kuogopa kwetu kuwaumiza wengine kwa kushindwa kusema hapana au haiwezekani, tunapaswa kuwa na jibu moja ambalo ni ndio au hapana. Hii itasaidia sana kutoingia kwenye kundi la waongo.

Shida nyingine kwenye hili yule uliyemwahidi jambo fulani, hatakuelewa pale ambapo hujatimiza ahadi yako kwake, atakuona wewe ni muongo. Hataelewa mambo mengine kwa wakati huo zaidi ya umemdanganya.

Kwa kuwa kudanganywa imekuwa kama sehemu ya maisha yetu, imesababisha tusimwamini Mungu juu ya ahadi zake kwetu tuliofanyika watoto wake.

Ikiwa wanandoa wanaahidiana kupendana siku zote za maisha yao, na hawataachana, na wanatoa kiapo hicho madhabahuni, lakini inafika mahali waachana na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine. Bila kujalisha Mungu anachukia kuachana kwa wanandoa.

Uongo umekuwa kama jambo ambalo limezoeleka, sasa kwa mtu ambaye hajalijua Neno la Mungu au bado hajakomaa kiroho, anaweza asione kama Mungu anaweza kumtendea jambo.

Pamoja na kutoamini kwa watu au mtu, Mungu wetu hayupo kama mwanadamu hata aseme uongo, kile amekiahidi juu ya maisha yetu/yako lazima akitimilize.

Rejea: Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? HES. 23:19 SUV.

Mungu wetu hana ahadi za uongo, Mungu wetu hairishi kumtendea jambo mtoto wake, lakini mwanadamu anaweza kusema uongo. Lakini mwanadamu anaweza kuahirisha jambo aliloahidi kwa mwenzake, haya yapo katika maisha yetu tunayoishi.

Ukiwa mtoto wa Mungu, yaani umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, unapaswa kuelewa Mungu wetu hasemi uongo. Kile amekiahidi kwenye maisha yako, uwe na uhakika atakitimiza maana yeye huwa hasemi uongo.

Rejea: katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele; TIT. 1:2 SUV.

Unaona hapo, inasema Mungu wetu asiyeweza kusema uongo, hili linapaswa kutupa nguvu na imani mbele za Mungu tunapokuwa kwenye safari ya maisha yetu ya wokovu.

Ndio maana ni muhimu sana kusoma Neno la Mungu kila siku, hii inatupa mwanga mzuri na kutujengea imani mbele za Mungu, na kufahamu kuwa Mungu wetu hawezi kusema uongo kwetu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.