Tupo mwanzoni kabisa mwa mwaka 2020, mwaka ambao tumefika kwa neema ya Mungu. Wapo ambao walikuwa hawana matumaini ya kuufikia ila kwa neema ya Mungu wamefika.

Inawezekana hapo ulipo umeshajiwekea malengo yako makubwa ndani ya mwaka huu uwe umeshayafikia, ama baada ya miaka mitano ijayo uwe umeshayafikia malengo yako.

Hili Jambo la kupanga malengo yako inawezekana kabisa halijaanza mwaka huu, limeanza miaka mingi iliyopita.

Pamoja na kuanza kupanga miaka mingi iliyopita, umejikuta unapanga malengo ambayo kila unapoanza hatua ya kufanya Jambo hilo unajikuta unakwamia njiani.

Lakini ukitazama wengine wanafikia au wanafanikiwa katika hilo hilo unalokwama wewe.

Huenda hukuwahi kukaa chini ukatafakari hili na kujiuliza shida ipo wapi, kwanini wengine wanaweza ila wewe unashindwa.

Mfano, umejaribu mara nyingi juu ya kujijengea nidhamu ya kusoma neno la Mungu kila siku. Lakini kila ukianza unashiaga njiani.

Leo nataka kukufungua macho, tabia mpya unapotaka iwe kwako sio jambo la kuamka asubuhi, na kufikia jioni itakuwa imejengeka kama unavyotaka.

Tabia mpya inahitaji uweke mkakati wa kudumu, mkakati ambao utamtangulizi Mungu mbele kila hatua utakayopiga. Taratibu kadri unavyoweka bidii kidogo kidogo hiyo tabia ndio ijengeka kwako.

Kingine ni kuamua kuachana na mambo mengine, mambo ambayo ni kizuizi kwako. Ambayo yanakufanya yakuvute nyuma.

Pamoja na kuanza kujiwekea nidhamu ya kusoma neno la Mungu kila siku, vipo vitu unapaswa kuviacha, vipo vitu unapaswa kuviondoa kwenye maisha yako.

Sio hayo tu, wapo watu unapaswa kuvunja nao urafiki kabisa, ule ukaribu wenu wa kupitiliza unapaswa kuwekewa mipaka ambayo itawafanya muwe mbali nao.

Wapo watu bila kujiweka nao mbali, bila kukata mawasiliano nao, bila kuondoa ukaribu nao. Hao watu watakuwa sindano/mwiba wa kushindwa kufikia malengo yako.

Rejea: Lakini kama hamtaki kuwafukuza wenyeji wa nchi watoke mbele yenu; ndipo hao ambao mtakaowasaza watakuwa kama sindano machoni mwenu, na kama miiba ubavuni mwenu, nao watawasumbua katika hiyo nchi ambayo mwakaa. HES. 33:55 SUV.

Haya ni maelekezo ya Mungu wanapewa wana wa Israel, hata wewe leo unapewa. Hakikisha unaondoa miiba/sindano ambazo zitakufanya ushindwe kufikia LENGO lako la kusoma neno la Mungu kila siku.

Sindano yako ni marafiki ulionao, sasa jiweke nao mbali, kama ni mitandao ya kijamii angalia ni kitu gani huwa kinakupotezea muda mwingi alafu ukiondoe.

Mwaka 2020 uwe mwaka wako wa kusoma neno la Mungu kila siku, utaona kiwango chako cha ukuaji wa kiroho ukiongezeka.

Kama unasoma makala hii na bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku. Karibu sana uungane na wenzako wenye nia moja ya kusoma Biblia.

Namba yetu ya wasap ni +255759808081, tuma ujumbe wako kwa njia ya wasap tu. Usitume ujumbe wa kawaida hautapata msaada wa haraka.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.