Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya mbele zetu, umefikia mpaka leo ujue Mungu  ana kusudi na wewe.

Napenda kuzungumza na wewe msomaji wa neno la Mungu, leo sina haja sana asiye msomaji wa neno, bali leo nasikia moyoni mwangu kuzungumza na wewe unayetoa muda wako kwa ajili ya kusoma NENO.

Nataka kuzungumza zaidi na wewe uliyeanza safari vizuri ya kujisomea NENO la MUNGU, ila umefikia wakati umechoka na huna hamu tena ya kusoma NENO.

Umejaribu kujitahidi ila unasikia uzito ndani yako, kila ukisema ushike biblia unasikia ndani yako subiri kwanza utasoma kesho, kila ukijaribu kufungua biblia yako kwenye smartphone/tablet unasikia kujipa muda zaidi.

Wakati huo unaendelea kuzunguka kwenye mitandao mbalimbali, wakati huo unaendelea kusoma jumbe mbalimbali za wengine.

Pamoja na kujipa kesho, hujawahi kuitimiza hiyo kesho, kila ukifikia hiyo kesho, unaongeza kesho nyingine.

Kuna wingu limekufunika na kukutia moyo na kujisemea, hata ukisoma huelewi bora utulie kwanza, kutulia hivyo ndivyo umezidi kupoa zaidi, na unapoelekea utasahau kabisa ratiba yako ya usomaji NENO.

Huenda hapo ulipofikia umeanza kuona wenzako mliokuwa mnasoma nao NENO, wanakukera sana wanavyojibidiisha kusoma NENO.

Hujaishangaa hiyo hali kwanini uanze kuchukia mtu anayejitoa kusoma NENO, hujishangai wewe ambaye kiu ya kusoma NENO imekata na kuhamishia chuki kwa wengine wanaosoma.

Hali hizi zipo, tena humtokea kila mtu, na lengo la hali hii ya kukuvuta uendelee kupeleka muda mbele wa kupumzika kusoma NENO. Nia yake ni wewe uache kujaza maneno ya Mungu ndani yako ambayo ni pumzi ya Mungu.

Kuacha kusoma NENO ni furaha kwa adui maana unaacha kujua mengi, na kutojua NENO utaendelea kuangamizwa na adui, kwa mambo madogo ambayo ungejua NENO yasingekupa tabu.

Mbona nakuambia tu maneno ya kuendelea kukuchoma?

Ama kweli nimejikuta nakwambia ukweli ili uelewe baadhi ya mambo, kujua huku kunakupa nafasi ya kujitathimini maamzi uliyochukua yana faida au yana hasara.

Kwa maelezo niliyokupa yanaonyesha maamzi yako yana hasara kubwa tena hasara yenyewe inakuua pande zote mbili, kiroho na kimwili.

Mpaka hapo utakuwa umeelewa vizuri na utakuwa umejua kosa lako lipo wapi, mimi nina ujasiri wa kukuambia ukiamua leo unaweza kuondokana na uvivu huo.

Haijalishi unapitia hali gani kwa sasa, kama unayo macho na umeweza kusoma ujumbe huu, una nafasi nyingine tena ya kuanza upya na Mungu katika kusoma NENO lake.

Katika NENO la MUNGU, kuna uponyaji wa moyo wako, kuna kuinuliwa upya moyo uliokosa tumaini, kuna tumaini jipya kwa nyakati unazopitia sasa.

Ninachokushauri badili usomaji wako, soma biblia kama unasoma barua ya majibu ya matatizo ya maisha yako.

Kwanini usome biblia kwa mtindo huo, barua ya majibu yako ina umakini wake wakati wa usomaji, nasema barua ya kupandishwa cheo kazi ina ladha ya kusoma na kurudiwarudiwa kwa furaha kuu.

Elewa hili ndugu yangu, nimeliona hili katika usomaji wangu wa NENO, wakati mwingine nilisoma NENO kwa kulipua. Ila nilisikia moyoni mwangu ukifanya hivyo utatoka mtupu, ilinibidi kurudia tena na tena ndipo nilipata kitu.

Suluhisho ni kutuliza akili zako kwenye NENO la MUNGU, wakati unasoma, hakikisha akili zako zipo ndani ya biblia, utasema haiwezekani, nakwambia inawezekana.

Shida ni kwamba hujajua umhimu wa NENO, labda nikukumbushe mfano huu; umewahi kuwa umechoka sana yaani huwezi hata kufungua macho ila ulivyopewa taarifa mbaya ulinyanyuka haraka sana na usingizi wote na uchovu wote kukata!

Umewahi kukaa ukiwa huna hamu na kitu chochote, zikaja habari njema kuhusu changamoto uliyokuwa unapitia. Ukasikia kuinuka tena kwa ujasiri na kubadilika uso wako.

Hapo umeona ni jinsi gani hali yeyote unaweza kuitengeneza, mwili wa nje huna nguvu wala ujanja pale utu wa ndani unapoinuka kwa ujasiri.

Kuanzia sasa ondoa takataka zote zinazokufanya ushindwe kusoma NENO, ziweke pembeni ziambie sasa ni muda wa NENO, ziambie sasa ni muda wa kuzungumza na BABA yako. Hakuna kitakacholetea ubishi maana unaenda kuongea na BWANA wa mabwana, MFALME wa wafalme, MUNGU wa miungu.

Kupata muda wa kusikiliza Mungu anasemaje kupitia NENO lake, ndio muda wako mzuri wa kumwambia BABA kupitia NENO lako naomba uniondolee hili, naomba uniepushe na hili, naomba unisaidie na hili.

Kilichoandikwa kwenye biblia ni kweli na hakika, una uwezo wa kudai hitaji lako kwa ujasiri ikiwa u mtakatifu mbele za MUNGU, kupitia NENO.

Amka sasa kama ulianze kulegeza kamba ya kusoma NENO, zikaze sasa kamba zako, anza upya safari yako ya usomaji NENO, ondoa chuki na uvivu wa kutopenda NENO.

Mungu akubariki kwa kuahidi kuanza upya, Mungu akutie nguvu kwa kuinuka tena, mtangulize Mungu kila hatua yako ya kujifunza NENO LAKE.

Nikukumbushe LEO tupo katika kitabu cha 1 Nyakati 18, nikualike tuwe pamoja katika kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii.

Samson Ernest.

+255759808081.