Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari leo ndugu mpendwa katika Kristo YESU. Siku nyingine tena Bwana ametupa, nasi hatuna budi kuitumia vyema siku ya leo.
Naendelea kukushirikisha mambo mbalimbali kuhusu faida ya kujifunza NENO la MUNGU, kwa kutenga muda wako wa kusoma NENO la MUNGU. Vilevile naendelea kukupa mbinu mbalimbali za namna ya kuondokana na hali ya uvivu, ili uwe msomaji mzuri wa NENO.
Leo napenda kukupa tahadhari ya kitu kingine ambacho ukikielewa na kukishika, utavuka salama kabisa bila tatizo na utakuwa mwalimu mzuri kwa ndugu/rafiki yako.
Unaposoma NENO la MUNGU, unahitaji umakini mkubwa sana, unahitaji utulie ili upokee kile ambacho kimeandikwa ndani ya biblia.
Usipokuwa makini, ukasoma tu harakaharaka, kuna uwezekano wa kumeza NENO tofauti na vile ilivyotarajiwa.
Usipokuwa makini, unaweza kuwa na kumbukumbu tofauti na ile uliyopaswa kuwa nayo.
Ndio maana unashauri kuwa na muda wa kutafakari yale uliyojifunza, ikiwa kuna sehemu utagundua ulienda haraka bila kuelewa, upate muda mwingine wa kurudia kusoma na kuelewa.
Kwanini uwe makini katika kusoma NENO, unaweza kulisha watu matango pori pasipo wewe kujua kwa kushika NENO la MUNGU isivyo sahihi.
Mtu akikuambia hapa umekosea, unaweza kukasirika kwa kumfikiria vibaya kumbe umekosea kweli, ila umeshindwa kuelewa kwa kukosa umakini wako.
Nakueleza kitu ambacho kimenitokea mwenyewe, usiseme labda nasema watu wengine tu, nakueleza kitu ambacho ni halisi.
Kukosea kwangu sio nilishindwa kuelewa mstari, bali nilichanganya habari ya upande mwingine kuileta kwa upande usiohusika. Hii kwa mtu asiye msomaji wa neno hawezi kuelewa hata kidogo maana ilikuwa ni kosa lililojificha sana.
Kosa hilo lilinifanya niumie sana na kutubu mbele za MUNGU, baada ya kuona kwa kukosa kwangu umakini, nimesababisha mwingine kusoma habari ambayo haikuhusiana vizuri na kile nimekisema.
Sijakuambia kukosea hakupo, kupo sana ila unapaswa kuwa makini katika kusoma NENO, umakini wako unahusika sana katika hili.
Ukisoma biblia alafu unawaza mambo ya kazini, au unawaza mambo ya chuoni kuwa kuna kazi hujamaliza au unawaza changamoto za maisha, utakuwa unapita tu lakini akili haipo kabisa kwenye NENO.
Haya makosa nimeyaona kwa watumishi wengine pia, ila nimependa kujizungumzia mimi kwa sababu limenitokea. Maana inaweza kuwa rahisi kukueleza vizuri na kukusadia namna ya kuepukana na hili jambo.
Napenda kuwambia watu wanaoanza kusoma NENO la MUNGU, usisome biblia ili uonekane umemaliza kusoma biblia yote. Soma biblia kwa umakini uelewe kile unasoma, tena pata muda wa kutulia utafakari yale umesoma.
Kukimbia kwako utasoma sura 5 kwa siku moja, ila ukijiangalia unajiona kabisa huna kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya KIROHO.
Usikimbize upepo, usishindane na watu wengine waliokupita sana, najua kuna watu wamerudia biblia nzima zaidi ya mara mbili. Hii isikupe tabu kama umeamua kuanza na wewe, nenda taratibu.
Nakwambia kwenda kwako kwa umakini, unaweza kuwa vizuri zaidi ya mwingine, maana faida ya wewe kusoma NENO ni ili uishi sawa sawa na NENO linakuelekeza.
Wengine ni wasomaji wa neno ila si watendaji wa NENO, ndio wale tunasema wanasoma biblia kama gazeti fulani hivi. Wewe usikubali kuwa miongoni mwao, yale unajifunza kuwa sehemu ya kuyatenda, na kuyaishi.
Utaona mafanikio makubwa sana KIROHO na KIMWILI, tunashindwa kuelewa kuwa NENO la MUNGU linaweza kutuelekeza maeneo yote katika maisha yetu kwa sababu ya kutojua.
Uwe makini katika kusoma NENO, dini/dhehebu lako lisikufunge kiasi kwamba unaanza kubishana na maandiko Matakatifu.
Dini si WOKOVU, YESU Kristo hakuleta dini/dhehebu, dini ni mpango wa mwanadamu katika kumwendea Mungu. Sasa unaweza kufungwa na dini ukaikosa mbingu kabisa.
Narudia tena na tena, unaposoma NENO la MUNGU, jenga utulivu wa mawazo yako, ikiwezekana jikabidhi kwanza mbele za Mungu ndipo uanze kusoma NENO.
Usisome NENO huku umejaza matakataka kichwani, jifunze kuweka mambo mengine pembeni, yaani hata umekaa na mtu pembeni usihisi kuna mtu bali uone upo na biblia yako.
Najua umewahi kuwa sehemu yenye makelele mengi, alafu ukawa husikii kabisa yale makelele kutokana na jambo uliloweka umakini nalo.
Wengine wanaweza kuwa na msongo wa mawazo kiasi kwamba, yupo sehemu labda kwenye kusanyiko, wenzake wanajadili vitu vya msingi yeye hayupo kabisa eneo hilo kimawazo.
Usiwe hivyo, najua ukijua uzito wa NENO la MUNGU, huwezi kuruhusu wazo lingine likusumbue, utakuwa makini sana katika kusoma NENO.
Mpaka hapo utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika usomaji wako wa NENO la MUNGU.
Kwa wale ambao tupo pamoja katika usomaji wa NENO la Mungu wasap group, ambao tunaenda hatua kwa hatua, leo tupo katika kitabu cha 1 Nyakati 19.
Unapenda na wewe kuwa miongoni mwao, unakaribishwa sana, kikubwa uwe umejitoa kweli. Unaweza kuwasiliana nasi moja kwa moja kupitia wasap kwa namba hizo hapo chini, narudia tena uwe umeamua kweli kusoma NENO na sio uje ujaribishe kusoma.
Nakutakia siku njema yenye ulinzi wa Mungu.
Samson Ernest.
+255759808081.