Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za leo, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa ili kuendelea kumzalia matunda mema, na nafasi kwao wale ambao hawajaacha matendo yao mabaya na kulikiri jina la Yesu Kristo.

Neno la Mungu ni ufunguo wa maisha yako KIROHO na KIMWILI, Neno linakupa mwanga na usahihi wa njia ya wokovu, ambayo unapaswa kuenenda siku zako zote za uhai wako.

Tunaweza kusimama kutetea sana dini zetu, lakini ukweli ukabaki palepale kuwa kuna maeneo tunayafuata hatupo sahihi. Tunapojua Neno la Mungu tunapata kuelewa tulipo ni sawa ama tulipo si sahihi.

Dini zetu zinaweza kuwa zimetujaza hofu nyingi ili tushindwe kumwona YESU Kristo akitenda makubwa katika maisha yetu. Badala yake tukawa tumefungwa fahamu zetu tushindwe hata kupokea ahadi za Neno la Mungu.

Tumeona dini nyingi zilishikilia msimamo wa jambo fulani kuwa ni sahihi, kumbe halikuwa sahihi, baada ya kuja kujua kuwa Neno la Mungu linaelekeza tofauti na wao, waliamua kubadili msimamo wao na kuifuata iliyo kweli.

Tumeona dini zingine pamoja na baadhi ya watu wake kufahamu kweli, bado wameendelea kushikilia msimamo wao. Hatuwezi kujua sana wana mashaka ya kuonekana walikosea ama vipi.

Tunapojifunza hapa Neno la Mungu, tunapata nafasi ya kuona kipi cha kutenda, na kipi cha kufuata. Neno la Mungu halina upendeleo kama ilivyo dhehebu/dini yako, lenyewe linaelekeza iliyo kweli bila kupindisha chochote.

Wakati mwingine tumekosa baraka za Mungu kwa kutojua Neno, mara nyingi dini zetu zimetuzuia kufanya yale yanayotuletea ushirika mzuri na Mungu wetu, kwa sababu ya mapokeo tuliyonayo.

Hatuwezi kusema dini ni mbaya, zinatusaidia sana kutuelekeza njia za kwenda mbinguni kuketi na Bwana siku moja baada ya tabu za dunia. Ubaya unakuja pale tunaposhindwa kuelewa Neno, kwa nguvu za dini zetu. Hapo tunakuwa tumeweka mioyoni mwetu dini zetu badala ya kumweka Yesu Kristo moyoni.

Unaposoma Neno la Mungu linakufungua baadhi ya mambo ambayo hapo nyuma uliona kama huwezi kuyafanya, na mengine utayaona ni mapya kabisa, kumbe ni haki yako kuyatenda.

Tunaweza kuhangaika kupigana vijembe kuwa akina fulani hawamwabudu Mungu wa kweli kutokana na jinsi wanavyoenenda. Na wao unaowaona hawapo sawa, wakabaki kuona na ninyi hampo sawa.

Kila mmoja anaweza kuvuta upande wake kuwa ni sahihi kwa manufaa yake binafsi, na wengine kwa ajili ya kutamani watu wamfuate Mungu katika njia iliyo sahihi.

Mivutano hii ya kidini/kidhehebu msemaji wao wa mwisho ni Neno la Mungu, tutaweza kupima watu hawa wanamwabudu Mungu wa kweli na watu hawa hawamwabudu Mungubwa kweli, kupitia Neno la Mungu.

Lione Neno la Mungu ni jambo la mhimu sana kwako, hivi hujiulizi kwanini vitabu vingine vimezidi ukubwa wa biblia lakini unasoma mpaka nukta ya mwisho? Hiyo ni vita inayokuzuia usiijui kweli, kuijua kweli itakufanya uondoke kwenye giza.

Ombi langu kwa Mungu ujue uthamani wa kusoma NENO LAKE, kuijua kweli hutomtenda Mungu dhambi, kuijua kweli utafanya yampendezayo Mungu, kuijua kweli itakufanya kuondoka katika mapokeo yaliyokuzuia kumwona Mungu akitenda mambo makubwa katika maisha yako.

Hatujuvunii kuwa na dini nzuri, tunajivunia kuwa na YESU Kristo mioyoni mwetu, tunajivunia kukombolewa kwenye dhambi na damu yenye thamani, si damu ya kuku, mbuzi wala ng’ombe, ni damu Yesu Kristo.

Kuanzia sasa jitoe katika kusoma NENO la MUNGU, kataa uvivu, kataa sababu za kukufanya uendelee kubaki hapohapo mwaka hadi mwaka. Anza kuonyesha vitendo, shika biblia yako na uanze kuisoma kwa bidii zako zote.

Usikubali kuendelea na hadithi za kujifariji uendelee kutosoma NENO, amua kuijua kweli uwe huru, kulijua Neno la Mungu ni kwa manufaa yako. Manufaa yale uliyoyapata wewe yatamsaidia na mwingine ambaye bado hajajua umhimu wa kusoma NENO.

Neno la Mungu ni mbegu ya maisha yako, unaweza kuanza kuipanda leo faida yake ukaja kuiona baadaye, baada ya kuanza kuvuna mavuno yake.

Ulikuwa unasoma NENO la MUNGU ila si kwa kila siku, na hukumbuki mara ya mwisho ulishika biblia lini, na unatamani kuungana na wenzako wanaosoma NENO kila siku. Unakaribishwa sana group la wasap kama umeamua haswa, hapa uwe umedhamiria kweli ndipo utaweza kuendana na hili kundi.

Umejiona upo tayari, tumia namba hizo chini kuwasiliana nasi kwa njia ya wasap sms, usitumie njia nyingine, tuma sms yenye majina yako mawili kwa njia ya wasap.

Kwa wale ambao tupo pamoja, leo tupo katika kitabu cha 1 Nyakati 22, tunaenda kusoma na kushirikishina yale tuliyojifunza.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.

+255759808081.