Milipuko ya ghafla na kupotea.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu katika Kristo YESU. Siku nyingine tena tumepewa na Bwana tupate kuitumia vyema katika kuleta faida ya uwepo wetu siku ya leo.
Kila mmoja anampenda Mungu, hakuna mkristo utakayemuuliza kuhusu habari za Mungu akakuambia hamtambui Mungu. Pamoja na kumpenda Mungu, wengi wetu tunapenda kufikia kiwango fulani KIROHO.
Kila mmoja utakayemuuliza ana mpango gani wa kuendelea kusogea hatua moja kwenda nyingine kiroho, atakupa mikakati mingi sana mizuri. Mihemko hii imetufanya wakristo wengi kubaki pale pale, kwa kuanzisha kitu kwa mbwembwe nyingi sana baada ya muda tunapoteana kabisa.
Wewe ni shahidi wa hili, umeshuhudia huduma ngapi za KIROHO zilivyoanza kwa kasi kubwa, leo zimepoa na zingine hazipo kabisa tena. Hii ni kwa sababu tunakuwa na maneno mengi kuliko kujua kuna gharama katika vitendo.
Mtu anakupa mikakati mikubwa ya mwaka, anakuambia mwaka huu nina mpango wa kujifunza NENO la MUNGU kwa juhudi kubwa sana. Kweli mtu huyu anaanza kusoma vizuri NENO la MUNGU kwa muda fulani, baada ya siku kadhaa mbele anazima kama moto wa karatasi na anasahau kabisa kama aliwahi kuahidi kitu kama hicho.
Hizi ni tabia fulani mbaya lazima kila mmoja amue kuzikataa, mtu anakujia na kukuambia nahitaji kusoma NENO la MUNGU, wapo wengine wananiomba niwaunge kwenye group la Wasap. Lakini ukishamuunga baada ya muda fulani anapoteana kabisa, na humsikii tena kama amewahi kukuambia hiyo habari.
Huwa napenda ukweli hata kama utamuuma mtu, napenda kuambiwa ukweli, na napenda kuusema ukweli. Tuache kujidanganya sisi wenyewe, tujifunze kuendeleza yale tuliyoanzisha.
Mnaweza kupanga kwa pamoja tutakuwa na maombi ya mfululizo kwa siku kadhaa, kila mmoja atahamasika na jambo hilo. Na wengine wataongea kwa mbwembwe kubwa, ila toa siku chache zijazo rudi uliza ni wangapi mpo pamoja. Utashangaa katika watu kumi mmebaki wawili tu.
Wote hawa huwa wanaenda wapi, jibu ni kwamba, hawa wote ni watu wa kulipuka tu siku mbili tatu wanapoteana kabisa kwenye ramani. Nakubaliana kweli huwa kuna changamoto zinatokea katikati ya makubaliano, kuna kuumwa, kuna kupatwa na msiba, kuna kubanwa sana na shughuli kiasi kwa unakosa jinsi. Ila pamoja na hayo yote huwezi kubanwa kila siku, wakati huohuo una uwezo wa kuzurura kwenye mitandao, wakati huohuo una uwezo wa kukaa na marafiki zako kupiga stori.
Kukua kiroho sio jambo la kulipuka siku moja na kupotea, unahitaji kujitoa kila wakati ili kufanikisha kile uliamua kufanya. Tukiwa watu wa kuanzisha kitu lakini baada ya muda tunapoteana na kusahaulika kabisa kama tuliwahi kufanya hicho kitu itakuwa aibu kwetu wenyewe.
Tunaelewa kwamba katika kujitafuta wewe ni nani na unaweza kufanya nini, huwa tunafanya mambo mengi sana mwisho wa siku tunajikuta tumesimama katika jambo moja. Hili linaeleweka wala halina ubishi, mimi ninachozungumzia ni yale mambo ya msingi ambayo yanamsaidia mkristo kuwa imara katika WOKOVU wake.
Suala la kusoma NENO la MUNGU, sio kipaji useme kwamba ni jambo la watu fulani tu. Hili kila mmoja anapaswa kutenga muda wake wa kusoma NENO la MUNGU. Dunia ya leo imeendelea kuturahishia zaidi, zipo audio bible ambazo unaweza kusikiliza sauti na ukaendelea kupata vitu vya kukujenga.
Shida yetu hatupendi kujibana kwa mambo ya msingi katika maisha yetu, tunapenda kubanwa na mambo mengine ambayo ukiangalia sana hayana faida katika maisha yetu kiroho.
Unaweza kuamua kuendelea kulipukalipuka na kupotea, mchezo huu unaweza kuufanya katika maisha yako yote ya ujana na uzee. Itafika kipindi utaona ulicheza vibaya, ila utakuwa umri umeenda sana na huna jinsi ya kuurudisha nyuma.
Neno la Mungu ni hazina ya mwenye safari ya kwenda mbinguni, hazina hii jinsi anavyozidi kuiwekeza ndani yake ndivyo anavyozidi kujiweka mbali na mazingira ya kumtenda Mungu dhambi. Ndivyo anavyozidi kujiweka mbali na mitego ya mwovu shetani, maana NENO la MUNGU lililo ndani yake linampa mwanga wa kujua mitego iliyotegwa kwa ajili ya kumrudisha nyuma.
Hebu kaa chini utafakari kama mtu mzima, unasoma NENO la MUNGU ili iweje, ili uweze kuwa mwimbaji mzuri, ili uwe mwalimu mzuri, ili uwe mchungaji mzuri, ili uwe mwinjilisti mzuri, ili watu wakujue kuwa wewe ni bingwa wa maandiko mengi au kujua ahadi za MUNGU juu ya maisha yako Baada ya kujua sababu ya wewe kusoma NENO la MUNGU, kaa chini upige hesabu za gharama zote za hatua unazoenda kuchukia, kisha jua kuna changamoto gani katika hayo uliyopanga.
Ukija kuanza kusoma neno la Mungu, hutoona tabu au mateso ya wewe kusoma biblia kila siku. Maana tayari ndani yako umepokea na kuona mbali zaidi kwa kile ulichoamua kukifanya.
Habari ya kulipuka siku mbili tatu na kupotea, achana nayo kabisa, amua kuikomesha kabisa kama kweli unataka kuijua kweli ya Mungu kupitia NENO lake.
Wale ambao tupo pamoja Chapeo Ya Wokovu wasap group, leo tunaenda kujifunza na kushirikishana yale tuliyojifunza katika kitabu cha 1 Nyakati 26. Unakaribishwa sana kwa wewe ambaye upo tayari kwenda pamoja nasi.
Mungu akubariki sana, nakutakia usomaji mwema wa biblia.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.