ANZA NA HATUA NDOGO ZITAKUFIKISHA HATUA KUBWA.
Haleluya mwana wa Mungu, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema sana ametupa kibali tena cha kuiona siku ya leo.
Kukua kiroho kuna hatua zake, hizo hatua zinaweza kuonekana ni ndogo sana na hazina matokeo mazuri ya mwanzo, ila zina faida kubwa sana kwa atakayekubali kuvumilia.
Uvumilivu wetu muda mwingine unaonekana unatuchelewesha kufikia eneo fulani, kuchelewa huku huanza kutushawishi tutafute njia ya mkato ili tufike haraka eneo tunalolihitaji kufika.
Bila kujua zipo safari huwezi kufika haraka haraka bila kukaa kwenye usafiri husika, unaweza kuteswa sana na hili jambo kwa sababu hujajua hatua za kufuata.
Najua umewahi kujihisi kuruka angani kama Mungu angekuwekea mbawa pale ulipokuwa una uhitaji mhimu mkoa/nchi nyingine. Lakini pamoja na haraka zako ulipaswa kwenda stand/uwanja wa ndege kukata tiketi ndipo upewe ratiba ya kuondoka gari/ndege husika.
Uwe ulikuwa na usafiri wako ambao hukuhitaji kwenda kukata tiketi, bado ulihitaji kuwa mvumilivu barabarani/angani masaa kadhaa ndipo uweze kufika mahali ulipohitaji kufika.
Huwezi kufika safari yeyote kwa mawazo yanavyokutuma ufike, utahitaji uchukue hatua ambazo zitaweza kukufikisha pale unataka kufika. Haijalishi utachagua usafiri gani, bado utahitajika kuwa mvumilivu kwenye chombo ulichopanda.
Huenda hujawahi kufikiri hili kutokana na taratibu ambazo zimewekwa, umeona ni jambo la kawaida kabisa kutulia saa na siku ifike uanze safari. Pia hujawahi kufikiri utahitaji tena masaa mengine ya kutulia ili ufikishwe eneo unalotaka.
Huenda mama mjamzito huwa hatumshangai sana kubeba ujazito miezi tisa kwa sababu tunajua ni utaratibu, ila tunashangaa na yeye pia atashtuka pale atakapozidisha miezi tisa au atakapopunguza miezi tisa.
Nazungumza na hatua za usomaji NENO, nazungumzia uvumilivu wa kuwa na muda wa kusoma NENO la MUNGU, wengi wetu tumeona tunachelewa kufika pale tunapoona safari imekuwa ngumu.
Tumesahau hatua moja inazalisha hatua ya pili, vivyo hivyo hatua ya pili itazalisha hatua ya tatu, yaani jana uliposoma sura moja ya biblia kesho hutasoma palepale utasoma sehem nyingine tena. Hutorudi pale pale kuna hatua utakuwa umesogea, haijalishi hatua hiyo ni ndogo sana, bado utajulikana umesogea.
Wengi wetu tunatamani kusoma biblia, ila tukianza hatufiki mbali tunapumzika, mapumziko yale yanakuwa ndio mwisho wa safari yetu. Hebu fikiri mtu aliyekuwa anatoka Mwanza anaenda Dar, alipofika Singida akashuka kwenye gari kwa sababu ya kuchoka. Alipolala Singida akaona aendelee kupumzika, huyu mtu atakuwa amepumzika kweli ila atakuwa ameongeza hasara ya vitu vingi, muda na fedha.
Zipo safari tunahitaji kuwa wavumilivu sana, haijalishi umechoka sana bado utaendelea kuvumilia kwenye chombo cha usafiri ndipo utafanikiwa kufika safari uliyoipanga ufike. Ndio maana unaona abiria wanalala kwenye siti zao lakini dereva aliyewachukua mkoa mmoja atawafikisha mkoa mwingine tena anaweza kuvuka mkoa zaidi ya mmoja bila kufumba macho.
Dereva wetu ni Yesu Kristo, huyu dereva hajawahi kusinzia hata kama sisi tumechoka, hatupaswi kukata tamaa njiani, tunapaswa kuambatana naye kile anapotuelekeza ili tufike safari yetu.
Ukianza kusoma leo kitabu cha Mwanzo au Mathayo, unaweza kuanza kwa kiu kubwa na hamasa kubwa sana, ila utakapofika wakati fulani utajikuta umechoka. Usipokuwa makini unaweza kuishia hapo na ukabaki kusema niliwahi kusoma biblia baadhi ya vitabu ila sikumaliza.
Unapoanza hatua moja endelea kuwa na bidii ufike hatua nyingine na nyingine, kidogo kidogo utajikuta upo mbali sana. Hii ni wewe kuamua wala huhitaji muujiza ukutokee sijui wapi, muujiza mkubwa unao mwenyewe ni kuchukua hatua za kuanza kutenga muda wako kila siku kusoma NENO la MUNGU.
Vizuri sana ukawa na muda wako maalum wa kujisomea biblia, hii itakupa nidhamu fulani kila inapofika muda huo. Utasitisha mambo mengine kwa ajili ya kipindi cha kujisomea NENO la MUNGU, usiwe mtu ambaye huelewiki yaani leo unasoma kesho unapumzika. Kuwa na mpango endelevu ambao utanzaa mazoea na mwisho utaona ni sehemu ya maisha yako.
Usikubali kuanza kusoma NENO la MUNGU alafu ukaishia njiani, najua hili linawakumba wengi sana, maana mimi ni mmoja wapo. Niliwahi kuanza kusoma biblia miaka ya nyuma kabla sijaanza utaratibu nilionao sasa. Nilianza vizuri, ila nilipofika katikati ya kitabu husika, nikasema kesho ikawa kesho mpaka ikazaa miezi, na mwisho nikasahau kabisa.
Naelewa sana ninachokueleza hapa, usiogope hatua ndogo wala usizidharau hizo hatua, kidogo kidogo utajikuta upo eneo zuri sana KIROHO. Wakati mwingine utaanza kufikiria na usielewe kwanini miaka yote ulikuwa hujui jinsi gani NENO la MUNGU lilivyo na mambo mengi kiasi kile.
Mpaka hapa utakuwa umeelewa kuwa hatua zile unazoona ni ndogo, ni za mhimu sana katika kujifunza kwako NENO la MUNGU. Basi nikuombe kama ulikuwa umeacha kusoma NENO la MUNGU, anza leo kusoma tena. Kama ulikuwa bado hujaanza kabisa kusoma NENO la MUNGU, anza leo, yaani leo na si kesho.
Ambao tupo pamojaCHAPEO YA WOKOVU wasap group,tunaenda kujifunza NENO la MUNGU katika kitabu cha1 Nyakati 27. Unakaribishwa sana kama umedhamiria kweli kujifunza NENO la MUNGU.
Mungu akubariki sana kwa kuamua kutoa muda wako, kwa ajili ya kujifunza maandiko Matakatifu yaletayo uzima.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.