Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona, ili tuendelee kumzalia matunda yaliyo mema.

Miongoni mwa vitu ambavyo unapaswa kujitoa haswa kwa kumaanisha, ni pamoja na kutenga muda wako kwa ajili ya kusoma NENO la MUNGU. Usitafute sababu ya kutosoma NENO la MUNGU, kuruhusu sababu utakuwa mtu wa kujiona kila siku huna muda wa kusoma NENO la MUNGU.

Tukiacha kusoma NENO la MUNGU, tutaendelea kuishi kama wakiwa wasiomjua baba yao kwa sababu ya kutojua ahadi za MUNGU juu ya maisha yetu. Mungu hulitazama agano lake alitimize kwetu, atalitimizaje ikiwa wahusika wenyewe hatuelewi chochote. Tuseme ataweza kutimiza maana tayari ameahidi katika NENO lake, hata akilitimza tutajuaje ikiwa hatuna NENO la MUNGU ndani yetu.

Hatuna sababu ya msingi sana kusingizia ili tuendelee kukaa bila kusoma NENO la MUNGU, kukaa na kujidanganya kuwa tutasomaga tu wakati miaka inazidi kusonga mbele, ni kujidanganya.

Tuelewe kusoma Neno la Mungu, ni kwa ajili ya faida yako binafsi, ikiwa hujui kama ni kwa ajili ya faida yako, imefika kipindi hata ukitaka kubeba biblia unajisikia aibu. Mtu anaona bora abebe notebook kuliko biblia, maana anaona biblia itamfanya asiwe huru.

Hili pia la kutotembea na biblia tumeliona jambo la kawaida kawaida, hii inaletwa na kutojua kilichopo ndani yake. Maana wote tukijua thamani inayopatikana ndani ya biblia, utatamani maandiko yote yanyonywe na bomba la sindano uingiziwe yote, ambapo ni kitu kisichowezekana.

Vitu vingine kama vile ufahamu wetu umefungwa ili tusipate kuelewa, ila ni mambo mhimu sana katika WOKOVU wetu. Hivi kama mtu umeokoka alafu hujisikii kusoma NENO la MUNGU, kama sio tatizo hili ni nini ndugu yangu katika Kristo YESU.

Mambo mengine yakukataa kabisa, NENO la MUNGU ambalo ndilo dira ya maisha yako, unaona kama kitu fulani kisicho na faida. Lazima ukae chini ujihoji kwanini unashindwa kuwa na muda wa kusoma NENO la MUNGU.

Hatuwezi kuwa watu wa visingizio vya kila siku vya kushindwa kusoma NENO la MUNGU, hakuna mtu anaweza kusingizia kuwa ametingwa sana, yaani ni sawa na tuseme, akifika muda wa kula chakula cha mwili anashindwa kabisa kutokana na ubize wake.

Kama yupo mtu ambaye huwa anakuwa bize kiasi kwamba anaona hata uvivu wa kula chakula siku 3 au tano, aniambie hapa. Hakuna kitu kama hicho ambacho tunaweza kukiweka kama tunavyofanya kujipa sababu za kutosoma Neno la Mungu.

Jambo hili la kujipa sababu nimekuja kulijua vizuri baada ya kukaa pamoja na watu tuliokubaliana nao tuwe tunajifunza NENO la MUNGU kila siku. Kisha yale tunayosoma tunapaswa kushirikishana ili kujua kama kweli mtu amesoma na amepata kitu.

Zoezi hili la kusoma NENO la MUNGU kwa pamoja, limekuwa na hamasa kwa wengi, ila hamasa yenyewe huwa inadumu ndani ya wiki moja mpaka mwezi. Yule mtu anapotelea mitini hutakaa umwone tena, ukimuuliza atakupa kila sababu ili uone kweli hawezi kushika biblia.

Kubali ukatae hili ni tatizo, kama umeokoka alafu hujisikii kabisa ndani yako kuchukua hatua za kusoma NENO la MUNGU. Fahamu huo ni ukuta wako unaokuzuia usione baraka zako, ambazo Mungu amekuahidia juu ya maisha yako ya kimwili na KIROHO.

Nitakuambia anza sasa kuchukua hatua za kusoma NENO la MUNGU, unaweza ukalichukulia kawaida kama ulivyozoea kulichukulia hili jambo kawaida.

Nitakuambia anza leo kusoma NENO la MUNGU, ukaanza kweli ila baada ya siku tatu utapotelea mitini. Akija mtu kukuuliza mbona husomi tena biblia, naamini utakuwa na sababu nyingi sana za kutetea uzembe wako.

Habari njema ni kwamba ili uone matunda ya hili zoezi la kujisomea biblia kila siku, utapaswa kuwa mvumilivu kwa kujua unachokisoma ndicho Mungu alikitumia kuumba dunia hii na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

Ulivyochagua kuachana na dhambi ukaamua kuokoka, na leo unaitwa mwana wa Mungu. Unaweza kuchagua leo kuwa msomaji wa NENO la MUNGU, nakwambia ukidhamiria na ukaweka nidhamu katika hili hutakaa ujute maisha yako yote.

Yupo rafiki anakuambia kusoma NENO la MUNGU haina haja, sikuambii sana hafai kuwa rafiki yako maana unaweza usinielewe, ila fahamu kwamba huyo ni mpinga Kristo.

Badilika sasa uwe msomaji mzuri wa NENO la MUNGU, anza leo kubeba biblia yako kila unapoenda kanisani, ulikuwa huna biblia chukua hatua leo kwenda duka la vitabu ununue biblia yako.

Leo tupo kitabu cha 1 Nyakati 28, hii ni kwa wale ambao tupo pamoja CHAPEO YA WOKOVU Wasap group, tunaenda kusoma sura hii na kushurikishana yale tuliyojifunza.

Nakukaribisha sana katika darasa hili la kusoma NENO la MUNGU kila siku, ambalo ukituliza mawazo yako vizuri, lazima uondoke na kitu cha kukusaidia katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.

Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.