Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliyeshinda kifo na mauti, na sasa yu hai, habari za leo ndugu yangu katika Kristo. Siku nyingine tena mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona, kuiona tu siku ya leo ni baraka tosha kwetu, maana wapo hawajapata nafasi hii pamoja na walitamani wawepo. Tunapo bahatika kupata nafasi kama hizi hebu tuzitumie vizuri kumletea Mungu sifa na utukufu kwa kuyatenda yaliyo mema, na kuachana na yale yanayomkosea Mungu.
Unapoamua kujifunza NENO la MUNGU, fahamu kwamba umechagua jambo ambalo wengi walianza kulifanya na wakajikuta wamerudi nyuma kwa kuona walivyoona wao. Kuzungukwa na walioshindwa wengi, inakuhitaji uwe na nidhamu ya hali ya juu sana, huwezi kusema neno juu ya usomaji biblia bila kupewa sababu ya wewe kushindwa kufanikiwa katika hilo.
Kila mmoja aliyewahi kugusa kidogo usomaji wa NENO la MUNGU ana sababu za kutosha, kukuambia hicho unachofanya na yeye aliwahi kufanya. Ukifuatilia sana kwanini aliacha na hakuendelea mbele, anaweza akawa na visingizio vya kutosha. Ila mwisho utagundua ni uvivu uliomfanya asiendelee mbele kulijua NENO la MUNGU.
Kukua na kufikia hatua tukaanza kufikiri kama watu waliokomaa KIROHO, haiji kwa kula sana ugali, na haiji kwa kuwa na miaka mingi. Inakuja kwa kujifunza NENO la MUNGU, na kujua linatuasa nini, na linatutaka tufanye nini, tufuate yale tunaelekezwa.
Kujua alafu usiende kama unavyoelekezwa, hiyo ni habari nyingine, ila kuenenda pasipo kujua unatenda yasiyompendeza Mungu, hilo linaweza kuwa tatizo lingine baya pia. Ambapo ungejua usingefanya au ungefanya kwa sababu unajua unachopaswa kutenda.
Kupenda NENO la MUNGU kwa mdomo bila matendo, ni sawa na bure kabisa, haina utofauti wowote na asiyependa. Yaani sawa na unasema umeokoka alafu matendo yako yanafanana na asiyeokoka, hapo huna tofauti kabisa na asiyeokoka, tena wewe uliyeokoka alafu unatenda maovu una hali mbaya kuliko asiyemjua na kumkiri Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake.
Kipi sasa kinatuonyesha sisi tumefuata na kuamini kile tumekikiri kwenye vinywa vitu, kipi kinatufanya tuonekane tunapenda kile tukisema kwenye midomo yetu. Matendo yetu ndio yanatutambulisha yale tumeyakiri kwenye ndimi zetu, matendo tu yanazungumza hata pasipo mtu mwenyewe kuzungumza kwa mdomo.
Matendo yako yana mchango mkubwa sana kukutambulisha mwenendo wa tabia yako, jinsi unavyotembea, na jinsi unavyozungumza. Matendo yako yatakuonyesha kabisa wewe ni mtu wa imani fulani.
Hebu zile hadithi za kuambiana nampenda Mungu alafu matendo yetu yanamchukiza Mungu tuziache, nimeseme huwezi kufuata kitu usichokijua, na huwezi kutenda jambo ipasavyo pasipo kulijua vizuri. Unaweza ukalijua lakini usijue uzito wake kwa undani wake, ndio maana unafanya kutimiza wajibu ila si kwa moyo wote.
Wote tunajua vizuri madhara ya kutokula chakula, haya madhara tunaona matokeo yake kwa wengine ambao walileta uzembe wa kula. Leo hii unasikia mtu ana vidonda vya tumbo, kwa kusababishwa na kutokula. Na madhara mengine tunajua kabisa mtu asipopata chakula kwa muda mrefu inampelekea kufa kabisa.
Hebu turudi kwenye chakula cha kiroho ambacho ni Neno la Mungu, unawezaje kuishi pasipo kusoma NENO la MUNGU? Hilo ni swali la kujiuliza, kwa maana nyingine tuna watu wana vidonda vya tumbo kiroho, na kuna watu wamekondeana kiroho na wengine kufa kabisa kiroho.
Sio maneno mazuri sana kukuambia ila huo ndio ukweli, unaweza kuwa na mbegu nzuri sana ukawa umeipanda bila kupata mvua au kumwagiliwa maji. Mbegu ile haitakuletea faida yeyote, zaidi itaendelea kukaa kwenye udongo mwisho wa siku itaharibika huko chini.
Tunaweza kuwa na biblia zetu za gharama kubwa sana, lakini kama hatutazisoma zitakuwa hazina matunda yeyote kwetu. Tunaweza kuwa tunapenda sana NENO la MUNGU, lakini kama hatulisoma na kuliishi, itakuwa hasara mbaya sana kwetu.
Fikiri vyema ili unapochukua hatua za kulisha moyo wako NENO la MUNGU, uwe na uhakika safari uliyoanza inakupeleka sehemu salama. Ila ndani ya safari yako ina changamoto kubwa sana, unaweza kuanza kusoma NENO lakini mume/mke wako asijue kile unafanya. Badala yake anageuka fimbo kwako, sasa kwa kuona hivyo usisumbuane naye, tenga muda tofauti yeye akiwa hayupo wewe SOMA.
Marafiki zako wanaweza kuwa kikwazo kwako kushingdwa kusoma NENO la MUNGU, kuwa peke yako wakati unaanza kusoma NENO, yaani usikubali eneo lolote likukwamishe wewe kushindwa kusoma NENO la MUNGU. Tafuta kila mbinu ya wewe kupata nafasi ya kujifunza NENO la MUNGU, kama unavyofanya bidii ya kutafuta kila njia upate chakula cha mwili ule.
Umakini wako wa kujifunza NENO la MUNGU, utakufungua vitu vingi sana ambavyo huenda uliyumbishwa sana hapo nyuma na mpaka sasa hujawahi kuelewa. Yapo mengine utayajua ambayo hukuwahi kuyajua hapo kabla na hata sasa, na ili ufanikiwe kujua mengine zaidi kwa ufasaha. Uwe umeokoka ndugu yangu, na Roho Mtakatifu awe ndani yako, yaani uwe na imani na ujazo wa Roho Mtakatifu. Vinginevyo biblia itakuwa afadhali ya gazeti maana hutoelewa kitu unachosoma.
Badala ya kupata ladha ya maneno ya Mungu, utakuwa unaona vitu havieleweki kabisa kwako, au unaweza kusoma kuanzia mwanzo mpaka ufunuo usione mguso wowote wa Mungu ndani yako. Tatizo lipo kwako, hujamua kujizamisha kwa Mungu, upo juu juu mara upagani mara wokovu.
Chukua hatua sasa, unatamani kufikia kile umekitamani siku nyingi ambacho ni kusoma NENO la MUNGU, anza sasa na kama uliacha unapaswa kurudia tena kwa nguvu mpya na si kwa ulegevu tena.
Unapenda kuzungukwa na marafiki wenye safari moja ya kujifunza NENO la MUNGU, na kushirikishana yale waliyojifunza katika sura husika ya kitabu. Unakaribishwa sana*CHAPEO YA WOKOVU wasap GROUP,kwa kuniandikia sms wasap+255759808081*, hakikisha umedhamiria kweli kusoma NENO la MUNGU kila siku.
Hatuna haja kuishi kama wanyonge wasio na uhakika na maisha yao, tumeamua wenyewe kumfuata YESU Kristo kwa kuacha matendo maovu. Hebu tukubali kuwa wanafunzi wanaopenda kumjua Baba yao amewaahidia nini baada ya kuamua kuyaacha ya dunia.
Leo tunaenda kujifunza katika kitabu cha 2 Nyakati 1. Kwa wale ambao tuenda pamoja katika kujifunza maandiko matakatifu ya Mungu. Tamani kuwa miongoni mwa watu wanaotenga muda wao kila siku kwa ajili ya kusoma NENO la MUNGU.
Usiwe mtu wa kuachwa nyuma kila siku, hebu kuwa mstari wa mbele kulisoma NENO la MUNGU, ondoa dhana potofu ya kwenda na biblia siku za ibada tu. Ifanye biblia yako ni rafiki yako hata ukiwa nyumbani, isiwe ya kuendea nayo kanisani ila hujui kilichopo ndani.
Inafurahisha sana unapopitishwa na mtumishi wa Mungu kwenye maandiko Matakatifu, alafu wewe ukawa umewahi kusoma hiyo habari. Unakuwa unaongezewa vitu zaidi ndani yako, kuliko yule ambaye ndio mara yake ya kwanza kusikia NENO lile analohubiriwa.
Nakuomba sana uondokane na tabia ya uvivu, tumia macho yako na masikio yako kulijua NENO la MUNGU. Uwe mwimbaji unapaswa kulijua neno, uwe mwalimu unapaswa kulijua neno, uwe mchungaji unapaswa kulijua neno, uwe mtume unapaswa kulijua neno, uwe nabii unapaswa kulijua neno, uwe shemasi unapaswa kulijua neno la Mungu.
Mungu afungue ufahamu wako zaidi uelewe umhimu wa kusoma NENO la MUNGU.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.