Hesabu Gharama Na Muda Utakaotumia Kabla Ya Kuanza Jambo.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, siku nyingine tena tumepata kibali cha kuiona. Mungu hajakosea kabisa mimi na wewe tuwepo siku ya leo, lipo kusudi jema kabisa kuwepo siku ya leo, kila mmoja ajaribu kufikiri hili ili kuepuka kumaliza siku bila kumzalia Mungu matunda mema.
Kila mmoja wetu anapenda jambo fulani kulipata kama hakuwa nalo, na kama alikuwa nalo anapenda kuliona likiendelea kuwa lake. Shida inakuja ni namna gani kulipata hilo jambo kama alikuwa hana, na changamoto inakuja ni namna gani anaweza kulitunza lile jambo ambalo tayari alishakuwa nalo lisimponyeke.
Tunapokuwa tunajaribu ni namna gani tutapata kile ambacho tunakihitaji, huonyeshwa njia ya namna ya kukipata. Njia ile kweli inakuwa na jibu la hitaji letu ambalo mtu alikuwa anaumiza kichwa kulipata.
Njia ile inakuwa shida pale mtu anapoianza na kujikuta safari inakuwa ngumu, anasahau kabla ya kuanza safari ile alitakuwa kujipanga kifikra kuwa, kukutana na changamoto za njiani inaweza kutokea muda wowote. Ila hapaswi kuacha kuendelea kuendea kile ambacho alikuwa anakiendea, bali anapaswa kusonga mbele bila kuchoka wala bila kukata tamaa.
Tunajua sio kila ulichopanga kinaweza kuenda kama ulivyonga, ila kujua vizuri gharama ya kile ambacho unataka kukianza, inakupa nguvu ya kuendelea mbele pale unapojisikia kukwama ndani ya safari.
Kupiga hesabu ya gharama na muda utakaotumia, inakuandaa mapema kiufahamu mwenye safari ili usije ukavunjika moyo. Ambapo unakuwa na uelewa mzuri wa safari yako.
Tuseme labda unahitaji kujenga nyumba, kabla ya kuanza unapaswa kujua ni jinsi gani utaanza kujenga nyumba ile. Ukishajua njia gani itatumika kupata pesa ya vifaa vya kukamilisha nyumba yako, haitakurudisha nyuma pale utakapoanza kutajiwa bei za vifaa vya ujenzi na fundi.
Ujenzi wako unaweza kuupigia hesabu fulani ambapo unajua ukifika sehem fulani utaiacha kwanza nyumba yako, ili kujiongeza nguvu tena kutokana na nguvu yako ya pesa uliyonayo.
Hizo gharama za kujua wakati unaanza kujenga nyumba, yapo mambo mengine ya KIROHO unapaswa kuyaelewa vizuri kabla hujaanza kuyafanya. Unapaswa kuhesabu gharama ya huduma yeyote unayotaka kuanza kuifanya.
Unaweza kweli umeokoka lakini ukaanza huduma fulani, baada ya muda fulani unapoteana kabisa. Bila shaka hili umejionea mwenyewe kwako ama umeliona kwa marafiki zako. Ambapo mtu alianza huduma ya uimbaji akaifanya kwa muda mfupi, ila baada ya hapo hakujulikana tena yupo wapi.
Ukimfuatilia sana atakueleza sababu ambayo huenda angejua mapema kabla ya kuanza huduma ile ingemsaidia. Hapa ndipo wengi wanapoitika pale wanaposikia mioyoni mwao kumtumikia Mungu eneo fulani. Ila baada ya kukutana na changamoto wanaacha huduma zao na kuingia mitini.
Kujua gharama ya kile unachokifanya au unachotaka kuanza kukifanya, inakusaidia sana wewe kujipanga vizuri namna ya kwenda kukabiliana na yaliyo mbele yako. Ukijua gari lako linatumia lita 50 kukufikisha mkoa mwingine, hutoweka lita 20 kwa kujitoa fahamu kwamba zitakufikisha salama. Lazima utakwama njiani, lakini ukijua vizuri itakusaidia kutokwama njiani.
Najaribu kukuonyesha mambo mbalimbali jinsi yanavyoweza kumrudisha mtu nyuma kwa kutojua vitu vya msingi kabla ya kuanza safari. Usije ukafikiri mtu kuacha alichokuwa anafanya, atakuwa ameasi imani yake la hasha wengine wanashindwa kwa sababu ya kuparamia safari bila kujitoa katika roho na kweli.
Unaweza kuona pia mtu anaokoka vizuri na anaanza kwa kasi nzuri kabisa katika wokovu wake, ila baada ya muda anaona wokovu ni mateso bora arudie maisha yake ya awali. Mtu huyu hakujua safari aliyoanza ina milima na mabonde, ilimpasa kuwa mvumilivu kwa hali zote atakazokutana nazo.
Nataka kusema nini hapa kwako, wengi wanaanza vizuri kusoma NENO la MUNGU, ila baada ya muda fulani wanarudia maisha yao yaleyale ya kutokusoma NENO la MUNGU. Hii si kwamba ameacha wokovu, bali ameshindwa kujua gharama ya kusoma biblia inahitaji uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu sana, ndipo mtu aweze kufanikiwa.
Kama unahitaji jambo fulani ndio liwe sehem ya maisha yako, piga hesabu kwanza kabla ya kulianza, vinginevyo utaanza na utarudi kulekule ulipotoka. Elewa sababu ya wewe kusoma NENO la MUNGU, labda naweza kukusaidia sababu moja wapo ni wewe kujua ahadi za Mungu juu ya maisha yako ya sasa, na ya baadaye.
Usiwe mtu wa kulipuka kwa kila jambo, mambo mengine hayahitaji mlipuko bali yanahitaji kuyaishi na kuyatenda kama sehemu ya maisha yako. Ukielewa hili utafanikiwa sana maisha yako ya kimwili na kiroho.
Neno la Mungu linakupa dira ya maisha yako yote, sasa unaposoma siku mbili tatu unapotea, hiyo ni kujidanganya. Kuwa na utaratibu mzuri ambao utakufanya siku isipite bila kushika biblia yako usome.
Unapenda kuwa karibu na watu wanaojifunza NENO la MUNGU kila siku kwa kusoma sura moja ya kitabu, na kupata muda wa kutafakari kwa pamoja. Jibu lako lipo CHAPEO YA WOKOVU wasap group, cha kufanya ni wewe kuniandikia ujumbe wako wenye majina yako kamili kwenda namba +255759808081. Hakikisha unatumia wasap kunitumia ujumbe, na hakikisha una nia ya kweli ya kusoma biblia.
Wale ambao tupo pamoja katika hili, leo tupo katika kitabu cha 2 Nyakati 2, unakaribishwa sana ndugu yangu.
Nakutakia siku njema, uwe na wakati mwema wa kutafakari haya niliyokueleza hapa.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.