Uwe Makini Na Uvivu Hutengeneza Sheria Za Kulea Uzembe.
Haleluya mwana wa Mungu, nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai. Siku nyingine tena ya baraka mbele za Mungu, ametupa kibali cha kuiona tena leo, lipo kusudi la kila mmoja wetu aliyepata kibali cha kuiona leo. Wapo wanapaswa kuendelea kulitimiza kusudi la Mungu, na wapo wamepewa nafasi ya kuyaacha mabaya na kumrudia Mungu.
Zipo tabia ambazo unaweza kuzitengeneza wewe binafsi zikawa kama sehemu ya maisha yako, na zipo tabia unaweza usizitengeneze ukawa unaishi tu kwa kelele za watu wengine wanavyotaka wao uishi.
Marafiki wanaweza wakuelekeza njia nzuri ya kukufikisha kwenye malengo yako, na wakawa sehemu ya kukuhamasisha kufanya vizuri zaidi katika safari yako. Na wapo marafiki wanaweza kuwa sehemu ya wewe kupotea njia sahihi na wakakuelekeza njia isiyo sahihi.
Kila mtu ana mchango wake katika maisha yako, inategemeana na wewe unahitaji kundi gani la watu wa kuwa nao wakati huo. Ubaya wa marafiki unakuja pale unapotaka wakuelekeze njia ambayo wao hawaijui na kama wanaijua basi walijaribu wakashindwa.
Aliyeshindwa ana sababu nyingi zaidi za zile zilizomkwamisha, zinaweza zikawa za msingi na vilevile zinaweza kuwa asilimia kubwa zikawa zimeongezewa chumvi nyingi sana. Nikiwa na maana yapo mambo ambayo yalikuwa hayana nafasi kupewa kibali cha mtu kushindwa.
Ukiambatana sana na marafiki wavivu wasio na malengo yeyote, na ukijaribu kuwashirikisha ndoto zako wanakuzima kwa maneno ya kukatisha tamaa. Jinsi unavyoendelea kuambatana nao kila mara na ukawa unawasikiliza sana, bila wewe kujijua utajikuta umekuwa kama wao.
Marafiki wale wale wavivu, usipokubaliana na maneno yao ya kushindwa, ukaendelea kuishi yale unayoamini kufanikiwa. Wataongea mengi sana, na wakati mwingine watakupa muda wa wewe kuanguka kwa kile ambacho uliwaeleza.
Ukiwa na moyo wa ujasiri, ukafika wakati ukafanikiwa watabadilisha kauli zao. Na unaweza ukawa sehemu ya wao kuona kumbe inawezekana kufanya jambo hili likafanikiwa kabisa.
Shida ipo kwako kama muda mwingi utaumia kuwa na marafiki wenye maneno/mazungumzo mabaya wanayoongea muda mwingi bila kujizuia. Kadri unavyozidi kusikia mazungumzo yao mabaya ndipo unavyozidi kuyaweka maneno yao moyoni mwako, na mwisho wake unaweza kujishangaa na wewe umekuwa miongoni mwao mwa yale matendo mabaya.
Uvivu wa mtu unasababishwa na mambo mengi sana moja wapo ni hayo niliyokueleza ya kuambatana na marafiki hasi. Pia uvivu unakuja pale mtu anapochoka mwili alafu akakosa ule msukumo wa ndani kwa kile alichokuwa anakifanya. Anapokosa msukumo wa ndani hataweza kuendelea kufanya anachofanya hata kama atapata muda wa kupumzika, badala yake ataanza kusogeza siku za kufanya kile kitu.
Siku zikisogea mbele sana kwa ahadi ya nitafanya kesho, kesho ile huzaa kuacha kabisa kile ambacho ulikianzisha/ulikikusudia kukifanya. Hili ndio jambo ambalo limewafanya wengi kushindwa kudumu katika kusoma NENO la MUNGU.
Tumezungukwa na idadi kubwa sana ya marafiki zetu ambao biblia kwao ni hadithi, ukimweleza habari za kusoma NENO la MUNGU. Anaweza kuhamasika kwa maneno ila kimatendo hayupo kabisa, sio kana kwamba hajaokoka la hasha ni mwamini mzuri sana ila NENO hataki kulisoma.
Tunapokuwa tumezungukwa na idadi hii kubwa, tunahitaji nidhamu ya hali ya juu sana ili wasije wakatuambikiza uvivu wao wa kutosoma NENO la MUNGU. Lazima tulijue hili ili kuweza kuondokana na changamoto ya kufuga uzembe ambao hukupaswa kuwa ndani yetu.
Tunaweza kuona kutokuwa na kiu ya kusoma NENO la MUNGU ni kawaida, ila nakwambia ukawaida huu umeletwa na marafiki wavivu wanaotupa faraja ambazo zinatufanya tuendelee kudumaa kifikra.
Ninapokuambia kuwa makini unapojisikia kuchoka na ukaona unaanza kujisikiauvivu wa kutofanya kile ulichokipanga, uwe makini kweli sio utani. Maana utakapojaribu kufanya hivyo utaruhusu uvivu ule ukutengenezee sheria nzuri kabisa ambazo zitakufanya uone upo salama kumbe unaangamia.
Kusoma Neno la Mungu ni wajibu wa kila mwamini, aliyelikiri jina la Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Unapaswa kulijua NENO ili uwe na maelekezo sahihi ya njia ya kufuata pasipo kutangatanga.
Nakukumbusha tena uvivu usikupelekee kutengeneza sheria/kanuni za kuendelea kuwa mvivu. Utakuwa mwimbaji mzuri sana wa hizi nyimbo za NITASOMA NENO KESHO, NITAANZA TU KUSOMA NENO. Mwisho wake unachoka kuimba nyimbo hizo kila siku, unaamua kuacha na kubadilisha staili nyingine ambayo itakupa faraja.
Tenga saa yako moja tu kila siku usome NENO sura moja tu, kisha utafakari yale uliyojifunza ili yakusaidia katika maisha yako ya wokovu. Binafsi napenda uwe na utaratibu wa kusoma sura moja tu ya biblia, alafu baada ya kusoma uwe na muda wa kutulia kutafakari yale uliyosoma.
Utaona mabadiliko makubwa sanasana katika maisha yako ya KIROHO na KIMWILI. Sikuambii hadithi za uongo, nakueleza habari za kweli kabisa.
Huna marafiki mnaoweza kujifunza NENO la MUNGU pamoja? Nakushauri uambatane na marafiki hawa wanaosoma NENO la MUNGU kila siku, na kushirikishana yale waliyojifunza katika sura husika ya kitabu. Marafiki hao wapoCHAPEO YA WOKOVUwasap GROUP, ili uungane nao tuma sms yenye jina lako kamili kwenda wasap +255759808081. Tumia wasap tu kunitumia ujumbe, pia hakikisha umedhamiria kweli kusoma NENO la MUNGU.
Leo tupo katika *kitabu cha2 Nyakati 3*,kwa wale ambao tupo pamoja katika safari hii tuliyoichagua maisha yetu yote tukiwa duniani.
Nashukuru sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Facebook; Chapeo Ya Wokovu.
Email; chapeo@chapeotz.com
WhatsApp; +255759808081.