Kufanikiwa Kwako Jambo Kunaweza Kuleta Chuki Kwa Wengine.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine mpya Bwana ametupa kibali cha kuiona. Vyema tukaitumia siku hii vizuri kumzalia Mungu wetu matunda mema kwa kuitenda kazi yake, kupitia nafasi zetu tulizonazo.
Tunaendelea kushirikishana mambo mbalimbali yanayoweza kukomaza fikira zako kadri unavyozidi kukua kiroho, isije ukafika hatua fulani katika ukuaji wako wa kiroho. Ukajikuta unaumizwa na jambo, na wakati mwingine kurudishwa nyuma na jambo dogo sana, ambapo ungelijua mapema lisingekupa shida.
Tunapambana kufanikiwa, tujue hili kila mmoja wetu anatamani sana kufikia hatua fulani katika maisha yake, iwe kiroho au kimwili, awe mvivu au mwenye juhudi. Kila mmoja anatamani kufika viwango fulani ambavyo anafikiri kila wakati atawezaje kufikia pale anapopataka.
Wale wanaochukua hatua za kuanza safari ya kufika pale wanapopataka, wanapoanza safari huonekana kama watu wasiojua wanachofanya. Na wakati mwingine wanaonekana hawataweza kufika pale ambapo kila mmoja anapatamani kufikia.
Vita inaanza pale mtu huyu anapofanikiwa kwa jambo ambalo amepambana nalo muda mrefu kulifikia, wale wale waliosema hawezi, ndio wale wale wakaoanza kusema anajiona sana ana uwezo. Sijui kama unanielewa vizuri hapa, yaani aliyekuambia hutoweza kufikia jambo fulani ndio yuleyule anageuza kibao cha maneno mengine tena ya kukuumiza.
Kama hukujipanga katika hili utaanza kuyumba, maana wanaweza kuinuka hata wale watu ambao unawaamini na kuheshimiana nao. Kuanza kukutupia maneno ambayo kwako yanakuwa kama yanakulenga vibaya na kukuzuia usiweze kuendelea mbele, na kile ulichofanikiwa.
Unahitaji ujasiri kupambana na kelele za watu hawa, huwezi kuzuia ila unaweza kuzichukulia kawaida kelele zao. Na kuzifanya kama moja ya mafunzo yako ya kuweza kukufikisha sehemu nzuri zaidi ya vile ulivyokuwa mwanzo.
Binafsi siwezi kukuambia hiyo changamoto itakuja kwa njia ipi, ila naweza kukuambia utakutana na hali kama hii ya kuchukiwa kwa sababu tu ya mafanikio yako kiroho. Ikiwezekana omba Mungu uwe na uwezo wa kukabiliana na mambo kama haya, ambayo yanakuja bila taarifa.
Linda sana moyo wako usitawaliwe na hasira za kipumbavu, maana ukiziruhusu tu hasira ulizojazwa na watu wasiokutakia mema. Utajikuta umerudi nyuma na kuona ulichokuwa unakifanya hakina tena maana, mpaka uje ushtuke kuwa maamzi uliyochukua sio sahihi, utakuwa umeharibu mengi sana kwa kucheleweshwa.
Usomaji wako wa Neno la Mungu una mafanikio, una matunda mazuri sana, na matokeo yake unayaona kabisa. Kuona kule mafanikio usifikiri utaacha kuguswaguswa na changamoto zinazokutaka ukwame. Bali wewe zifanye hizo changamoto kuwa darasa lako na daraja lako la kuvukia, kufikia hatua kubwa zaidi kiroho.
Usifikiri ukijiweka vizuri na Mungu utaacha kujaribiwa, bado upo duniani, dunia iliyojaa kila changamoto, kila hatua unayopiga utakutana na kikwazo chake cha namna yake. Lazima ulielewe hili ndugu yangu, kama umechagua kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo, uwe jasiri wa kumfuata Yesu na kumsikiliza anachokuelekeza. Vinginevyo utarudishwa nyuma na kitu kidogo sana ambacho ukija kukigundua hutoamini kama kilikukwamisha.
Endelea kuongeza juhudi zaidi za kusoma Neno la Mungu, unapoona upinzani unainuka juu yako, na wewe unaona unachokifanya kinampendeza Mungu, ujue njia uliyochagua ni sahihi. Ila njia hiyo imejaa changamoto nyingi za kukuzuia usiendelee mbele, kwa kuwa wewe umejua dawa yake ni kuzigeuza hizo changamoto kuwa darasa na daraja lako la kufikia malengo zaidi. Basi uwe mwaminifu katika kulinda nidhamu yako ya kusoma NENO la MUNGU isipotee.
Uzuri wake Neno la Mungu linakupa maarifa ya kuzitambua hila za mwovu shetani, huna haja ya kuacha kusoma NENO la MUNGU kwa kusababishwa na jambo fulani. Kitabu kinachoweza kukuelekeza cha kufanya ndicho hicho hicho cha NENO la MUNGU.
Usivunjwe moyo na wasiojua kesho yako, hao hao wanaokupiga vita leo, ndio haohao watakaohitaji msaada wako kesho. Ili uje uwasaidie unapaswa kujenga nidhamu kwa kile kinachokuunganisha moja kwa moja na Mungu wako.
Tunaendelea kujifunza NENO la MUNGU kwa pamoja kupitia Wasap group, ambapo leo tupo katika kitabu cha 2 Nyakati 10. Tunaenda kusoma na kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura hii, tunakukaribisha wewe ambaye ulikuwa bado hujaanza hili zoezi na unatamani kuwa miongoni mwa ndugu hawa wanaojifunza Neno la Mungu.
Naamini umejifunza mengi ya kukusaidia usonge mbele hata pale vita vilivyoinuka juu yako. Pia umeona ni jinsi gani jambo zuri ambavyo linaweza kusababisha maadui ili usiweze kuendelea nalo.
Nakushuru sana kwa muda wako, nikutakie wakati mwema.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.