Kutafakari Neno La Mungu Inakupa Uwezo Wa Kuelewa Zaidi Na Kuwa Na Kumbukumbu Nzuri.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona tena leo. Tunapaswa kutengeneza pale tulipokosea, na kuendelea kumzalia Mungu matunda mema kwa kila mmoja wetu aliopo kwenye nafasi yake.

Leo napenda kukushirikisha jambo hili ambalo nimeliona likitenda kazi sana ndani yangu, unaweza ukaona ni jambo la kawaida ila ukilichukulia kwa kumaanisha linaenda kuzaa matunda mema sana ndani yako.

Tumekuwa tukipata muda mzuri wa kusoma NENO la MUNGU, na kupata muda mwingine mzuri wa kushirikishana tafakari zetu, kwa jinsi mtu alivyoelewa. Jambo hili limezaa matunda mema sana kwa wengi na limeongeza uwezo mkubwa wa kuhifadhi Neno la Mungu moyoni, na kupanuka uelewa zaidi ya vile mtu alivyokuwa mwanzo.

Tunaelewa sio kila kitu utakachokisoma unaweza kukielewa palepale, lakini mnavyosoma Neno la Mungu pamoja, na kila mmoja akashiriki kutoa mchango wake kwa kile alichokielewa, unakuta unapata uelewa zaidi.

Kusoma biblia yako alafu ukapata muda wa kutulia na kutafakari, ni sawa na mtu aliyejifunza darasani alafu anaenda kufanyia mazoezi ya vitendo kwa kile alichojifunza. Vitendo vile vinamfanya mwanafunzi huyu aelewe zaidi kwa kile alichojifunza darasani.

Zipo njia nyingine ambazo zimetumika sana darasani, kusoma kwa makundi makundi, katika makundi wapo watu wenye uwezo mkubwa wa kumwelewa mwalimu pale pale alichofundisha. Na wapo hawawezi kumwelewa mwalimu pale pale mpaka atakapopata nafasi nyingine kuelezewa. Mwalimu anapotoa zoezi la kufanya kwa makundi, unakutana na mawazo tofauti yenye majibu tofauti yenye kukufanya kuelewa kwa urahisi, unajikuta kama hukumwelewa mwalimu vizuri unapata wakati mzuri wa kuelewa yale ambayo hukuelewa.

Kujadiliana kwa makundi haikufanyi tu kuelewa zaidi yale uliyofundishwa, inakufanya uwe na uwezo mkubwa wa kuelewa mambo uliyojifunza. Kuliko ungesoma tu kile ulichofundishwa ukaishia hapo bila kupata muda wa kutafakari.

Nimetumia mfano huo wa darasani ili unielewe vizuri hichi ninachokueleza hapa, kufakari kwa njia ya kujadiliana kuna faida nyingi sana. Ikiwepo hiyo ya kuelewa zaidi kile ulichojifunza, na kukufanya kuwa imara zaidi wa kuweza kuelewa, na sio kukariri vitu ambavyo ukiambiwa uelezee unakuwa unashindwa.

Jenga utaratibu huu mzuri sana wa kusoma Neno la Mungu kisha upate muda mwingine wa kutafakari yale uliyojifunza, una uwezekano wa kuwa pamoja na wenzako ambao mnaweza kusoma Neno la Mungu kila mmoja kivyake. Alafu mkapata muda wa kushirikishana kile mlichojifunza, itapendeza sana na utakuwa zaidi ya vile ulivyokuwa peke yako.

Mnaweza kutumia makundi yenu ya kanisani, badala ya kuhubiriana kwenye vipindi vyenu vya katikati ya wiki, mnaweza kutenga siku moja kwa ajili ya kusoma sura fulani kwa pamoja. Na kushirikishana kila mmoja kile alichokielewa vizuri, kwa kufuata utaratibu wenu mzuri atakaoweka kiongozi wenu.

Njia hii inawezekana kabisa kama utaelewa vizuri maana yake, unaweza kujiuliza mbona kanisani kwetu huwa hatuna utaratibu huu. Na ukiangalia jinsi mazingira yalivyo unaona kuna ugumu fulani, basi mnaweza kutengeneza kikundi chenu cha marafiki nje na kanisani, mkawa mnakutana kila jioni eneo mliochagua kwa ajili ya zoezi hili.

Mkiona njia ya kukutana nayo inaleta ugumu kwenu kutokana na majukum ya kila siku, mnaweza kutumia magroup yenu ya wasap. Badala ya kuchati tu, mnaweza kukubaliana mwe na utaratibu wa kusoma NENO la MUNGU, na kushirikishana yale mliyojifunza.

Hapa mnahitaji nidhamu ya hali juu sana, na kiongozi wenu anapaswa kujitoa haswa kwa moyo wake wa kupenda. Maana mnaweza mkaanza vizuri mkafika njiani mkaacha, kama mlikuwa kumi mtashangaa mmebaki wawili. Na mkishafika wawili mtaona haina maana tena kuendelea na hilo zoezi.

Kama hilo nalo ni changamoto kwa magroup uliyopo, unakaribishwa sana CHAPEO YA WOKOVU wasap group kwa namba 0759808081. Hapa tumeweza kuwa pamoja kwa muda mrefu katika kusoma NENO na kushirikishana TAFAKARI zetu. Hapa unahitaji nidhamu yako ya kutoa muda wako kila siku kwa ajili ya kusoma na kutoa tafakari yako.

Njia hii imetufanya tuelewe zaidi yale tunayosoma, sisemi haya ili kukuvutia la hasha! nasema haya kwa kumaanisha kile kinachovunwa na wengi. Juhudi yako na nidhamu yako, ndio inakupa kile unachokihitaji.

Kama una utaratibu wa kujisomea Neno la MUNGU mwenyewe hilo nalo halina shida, endelea na utaratibu wako ila kumbuka kutenga muda wa kutafakari yale uliyojifunza. Ni mhimu sana maana inakujengea uwezo wa kuelewa zaidi kile umekisoma, na Roho Mtakatifu atakusaidia katika hilo.

Bila shaka umenielewa na kupata kitu cha kurekebisha, na kufanyia kazi yale maeneo uliyoona yana upungufu. Nakusisitiza ufanyie kazi uliyojifunza usiishie kufurahi ama kujilaumu.

Leo tupo katika kitabu cha2 Nyakati 11, unakaribishwa sana katika tafakari ya leo. Tenga muda wako kwa ajili ya Bwana, ni sadaka nzuri sana kwa Bwana kumpa muda wako.

Nakushuru sana kwa muda wako, nikutakie wakati mwema.

Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.