Anayetengeneza Sababu Nyingi Za Kushindwa Kuliko Za Kushinda Uwe Naye Makini Anaweza Kukuambukiza udhaifu wake.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa tukaitendee kazi siku ya leo, kwa kumzalia matunda yaliyo mema. Nakukumbusha sana hili jambo kila wakati, usikubali kuvunjwa moyo na jambo lolote hasi ukaamua kuachana kabisa, na lile lengo jema ulilolianzisha kulifanya. Utakuwa umetende kosa kubwa sana, huwezi kuzuia kuumizwa na mambo mbalimbali, ila una uwezo wa kutokubali kukata tamaa hata kama umefika wakati huoni njia vizuri.

Kila mmoja wetu ana mawazo yake ya kufikiri mambo na kuyachukulia kama anavyojua yeye kwa wakati huo. Mkusanyiko wa maarifa tuliyonayo, ndio yanatengeneza mitizamo tuliyonayo sasa, uwe mtizamo hasi au uwe mtizamo chanya. Jua hayo yote yanatokana na maarifa uliyojaza ndani yako, ukiona jambo haliwezekani alafu mwingine anaona linawezeka. Na akifanya likawezekana kwake kweli, na kwako ulipojaribu kufanya likashindikana kweli, ujue tofauti zenu zipo kwenye mtizamo.

Yupo mtu unaweza kukesha naye ukimweleza jambo fulani ukilifanya linawezekana, lakini akawa hayupo tayari kukubaliana na hilo jambo. Zaidi akawa anakushawishi namna ya kushindwa, na ukimpa namna ya kushinda, na ukamweleza jinsi wewe ulivyoweza kufanikiwa kupitia njia unayomweleza, anaweza asikuelewe kabisa.

Unaweza ukaanza kufikiri yapo mambo hayawezekani kabisa, japo wapo wengine wanaona yanawezekana. Upo sahihi kufikiri hayawezekani, ila mimi huko sipo, nipo kwa wawili hawa, mmoja anayeelewa vizuri kuhusu kufanikiwa hilo jambo na mwingine asiyeelewa vizuri ila anatengeneza sababu nyingi za kuendelea kushindwa.

Jiepushe sana na kauli za watu wenye kauli za mitazamo hasi, watu hawa unapaswa kuwambia inawezekana kwa vitendo na si maneno. Jinsi utakavyozidi kufanya na wakaona kufanikiwa kwako kwa kile walichosema hukiwezi, watakurudia tena kukuuliza siri ya mafanikio yako ni nini.

Nazungumza na wewe unayependa kujifunza Neno la Mungu, lakini umekutana na marafiki walioshindwa wakakujaza kila sababu ya wewe kushindwa. Ikiwa umekubali kuwasikiliza, utakuwa umeamua mwenyewe kujirudisha nyuma.

Ulipaswa kutumia muda mwingi kumsikiliza aliyeshinda na sio aliyeshindwa mwenzako, inaweza kuwa yupo alishindwa ila akawa anatafuta njia ya kuweza kushinda tena. Huyo mimi sina shida naye, tuna shinda na mtu aliyeshindwa alafu anataka na wengine washindwe kama yeye.

Hebu jiulize imekuwaje yeye aache kusoma NENO la MUNGU ghafla, wakati kuna mtu alimwonyesha njia nzuri ya yeye kusoma neno la Mungu kila siku. Alafu ukimuuliza kwanini ameacha, atakwambia unajua bwana …unajua bwana…yaani hana anachoweza kukueleza cha msingi. Ujue huyo rafiki alikuja kushindwa nguvu na marafiki wengine walioshindwa, na kuchanganya na ile hali yake ya nyuma ndio anapata mwanya wa kuacha.

Wapo watu hawapo tayari kubadilika kwa kuanza kufanya yale yenye manufaa kwao, kutokana na jinsi walivyoweka mitazamo hasi ndani yao. Kubadilika kwao mpaka waone wale waliojua hawawezi wameweza, hapo ndio wataanza kuona inawezekana, au wanaweza kutengeneza sababu nyingine hasi ya kuonekana mtu yule hajafanikiwa kihalali.

Ndivyo walivyo walioshindwa, lakini hapa hatupo kujifunza namna gani na sisi tutashindwa, kama kwa walioshindwa. Tupo hapa kujifunza kushinda, ni wewe kuamua kuondokana na mitazamo hasi na kuamini katika mtazamo chanya.

Tafuta sababu ya kwanini wengine walishindwa ili wewe utengeneze sababu nzuri ya kushinda, kwa kile unachojua kabisa kina manufaa kwako. Kile unaona kabisa ni msaada kwako katika maisha yako ya kimwili na kiroho, kifanye sasa.

Usisikilize waliorudi nyuma maana hawana kinachoweza kukufanya uwe mshindi, zaidi watakupa maneno mazuri na malaini ya kushindwa kwako. Ukiwauliza sababu ya wewe kushindwa kwenye jambo ambalo lina manufaa kwako na kwake, utakuja kugundua kuwa wanajitengenezea mazingira ya kuzidi kubaki na uvivu/uzembe wao. Sio kana kwamba hilo jambo wanaokuambia haliwezekani ni baya au halijulikani kuwa lina faida kwa wote.

Kama ulianza kusoma NENO la MUNGU, alafu umefika wakati unaona huna kiu tena ya kuendelea kujifunza Neno la Mungu. Jichunguze marafiki ulionao, utagundua idadi kubwa ya marafiki ulionao ni wale ukiwaeleza habari za kusoma NENO la MUNGU wanakuambia hilo waachie wachungaji wafanye. Wataenda mbali zaidi na kukuambia, walioenda chuo cha biblia, wenyewe biblia inawashinda ije iwe wewe ambaye hujui hata huo mlango chuo!!.

Ukishapewa hizo sababu nakwambia unaweza kujaribu kujitutumua kujitetea, na kuwaeleza kuwa inawezekana kujifunza Neno la Mungu. Ukishabaki peke yako utajiambia maneno uliyoambiwa ni kweli kabisa, hapo ujue umekwisha. Alafu ukute ulikuwa umebanwa kidogo na kazi unajumlisha na yale mawazo hasi, unabaki kuweka alama ya tiki.

Umechangua kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, lazima uwe na NENO la MUNGU la kutosha moyoni mwako. Vinginevyo utamtenda sana MUNGU dhambi na mataifa wasiomjua Mungu, watabaki kukushangaa na kusema, mkristo gani huyu anasema ameokoka alafu ana tabia chafu hivi.

Nimalize kwa kukumbusha kuwa, tupo katika kitabu cha 2 Nyakati 15, hapa ni kwa wale ambao tupo pamoja. Tunaenda kusoma sura hii na kushirikishana yale tuliyojifunza, hii inatufanya kuendelea kujimarisha zaidi katika tafakari zetu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com