Unapovuka Hatua Moja KirohoTamani Kuvuka Na Hatua Ya Pili.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana wetu ametupa kibali watoto wake kuiona ili tukaitende kazi yake, na tukamzalie matunda yaliyo mema. Vizuri ukaitumia siku ya leo vyema kuweka alama njema mbela Mungu.
Unapojitoa kusoma neno la Mungu kila siku, kuna hatua unasogea kiroho, unapofika hatua fulani kiroho usijione umemjua sana MUNGU huhitaji tena kujifunza Neno lake. Kujifunza uwe ni utaratibu wa maisha yako yote ukiwa hapa duniani, upovuka hatua moja tamani kuvuka ya pili, tamani zaidi na ya tatu, na ya nne, na ya tano.
Wengi wamefeli eneo hili, walipofikia viwango fulani kiroho walijiona hawahitaji tena kujifunza Neno la Mungu. Badala kuimarishwa zaidi kiroho, wamezidi kupoa zaidi kiroho, na kushuka zaidi. Maana waliona mambo ya Mungu ni yale yale hawahitaji tena kujifunza, wakati tunaambiwa Neno la Mungu ni jipya kila siku.
Omba Mungu akusaidie usifike hatua hii ya kufanya mambo ya Mungu kwa mazoea, usifike wakati unajiona huna haja tena ya kujifunza zaidi. Huwezi kujiuliza kwanini unapopata kiasi fulani cha pesa, unatamani kupata zaidi, hujawahi kujiuliza unapofika hatua fulani kielimu unatamani kusogea zaidi ya pale.
Ikiwa maisha ya mwili tunatamani kusogea zaidi hatua ya kile tulichokipata, iweje mambo ya Mungu hatuoni ni zaidi ya hayo. Lazima ulijue hili kwa undani zaidi, ulivyokuwa jana usiendelee kuwa hivyo kila mwezi/mwaka, tamani kusogea hatua nyingine katika kumjua Mungu.
Ndio maana tunaaswa tusiwe kama watoto wachanga, maana yake upo uwezekano wa kuendelea kuwa mchanga kiroho hata kama umri wako umeenda sana. Na inamaanisha uwezekano upo wa kusogea hatua moja kwenda nyingine kiroho.
Hebu fikiri una mtoto wako, tangu mtoto azaliwe mpaka leo anafikisha miaka miwili hakuna dalili ya kuota jino hata moja. Lakini anaendelea kurefuka tu, hapo utafurahia ile hali aliyonayo au utaanza kujiuliza mwanangu ana tatizo gani. Maana anapoelekea ataenda kupewa jina la kibogoyo, maana yake mtu asiye na meno.
Kila hatua unayopiga ina ukomo wake na inapaswa kusogea hatua ya pili, hii inayonyesha mabadiliko ya ukuaji wako kiroho kwa mwamini. Kama ulikuwa huna uwezo wa kutoa tafakari yako vizuri mbele za watu, basi uwe na uwezo zaidi kutoa tafakari yako kadiri siku zinavyozidi kwenda. Ukiwa pale pale kila siku, utaonekana mtu asiyekua, kwa maana nyingine umedumaa kiroho.
Unapaswa kujimarisha kila siku, hata mtu aliyekuona mwaka jana katika huduma, akikutana na wewe leo abaki na mshangao maana anayoyaona ni mabadiliko makubwa sana juu yako. Utashangaa anakuuliza ndugu hebu nipe siri ya mafanikio yako ni nini, ujue hapo kuna vitu anaviona sivyo alivyovizoea kwako.
Hatufanyi haya kwa mashindano ya watu fulani kuwaonyesha kuwa sisi ni sisi, tunafanya haya kwa ajili ya kumletea Mungu sifa na utukufu. Wanavyozidi kushangaa watu jinsi unavyozidi kuwa imara katika wokovu, wakija kuuliza hakuna cha kuwajibu zaidi ya kuwaambia ni Yesu tu amefanya.
Endelea kumwomba Mungu akusogeze eneo lingine zaidi kiroho, kuwa na kiu zaidi kujiona unasogea, ukijiangalia ulivyokuwa Mwezi December mwaka jana ujiona haupo vilevile. Utajishuhudia mwenyewe nakwambia, watu wanaweza kuwa walikuona upo vizuri kipindi hicho ila wewe kujilinganisha ulivyo leo na kipindi cha nyuma, unaona tofauti kubwa mno.
Huo ndio tunaosema ukuaji wa mtu kiroho, sio tunaimba tukue kiroho lakini unasoma Neno la Mungu hubadiliki. Upo vilevile kila siku, hapo tutasema kuna ukuta umekuzuia, uzuri wa mambo ya kiroho yanahitaji ujitoe kwa Mungu. Huwezi kusema sina pesa kumlipa Mungu aniinue, ni utayari wa moyo wako kuumimina mbele zake katika roho na kweli.
Narudia tena tamani kusogea hatua zaidi kiroho, kama leo upo hatua ya kwanza, tamani ya pili, ya tatu, ya nne, na ya tano, ukiweza nenda mpaka ya kumi. Kikubwa uone mabadiliko ya kiroho ndani yako.
Mpaka hapo naamini kuna kitu chema umekipata cha kukusogeza hatua fulani kiroho, naamini ulipo hujaridhika na kujisahau sana, kama ulijisahau sana naamini kupitia ujumbe huu kuna eneo umevuka. Usibaki kusema mdomoni na kutikisa kichwa kuonyesha ni kweli, peleka yale uliyojifunza katika matendo.
Leo tupo katika kitabu cha 2 Nyakati 18, tunaenda kusoma sura hii mpya na kushirikishana yale tuliyojifunza. Naamini kila mmoja anayeenda pamoja nasi katika hili zoezi, anaona mabadiliko katika wokovu wake. Usirudi nyuma, ongeza bidii zaidi ya ulivyokuwa jana.
Mungu akubariki sana kwa muda wako, nakutakia siku njema iliyojaa baraka za Mungu kwako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com