Weka Utaratibu Mzuri Unaoeleweka Wa Kusoma Biblia.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele, siku nyingine tena Mungu wetu ametupa kibali cha kuiona. Tunasema ni kwa neema yake tu tumeweza kuiona leo, tunapaswa kuitumia vyema neema hii kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Wakati tunaendelea kukumbushana mambo ya msingi katika kusoma neno la Mungu, yapo mambo mengine yanazidi kujitokeza na tunapaswa kuelezana ili tuende pamoja katika hili. Usije ukaishia njiani katika usomaji wako wa Neno la Mungu, hili likatae kabisa siku zote za maisha yako ya wokovu.

Wengi wetu tunaona kusoma Neno la Mungu ni jambo la ziada sana, ambalo unaweza kulifanya ukijisikia au unaweza usilifanye kabisa usipojisikia. Ukawaida huu umewarudisha wengi nyuma kutokana na kutokuwa na mzigo wowote ndani yao.

Hatari kuufanya mwongozo wa maisha yako kawaida kama mwamini, hii inakupelekea kutokuwa na msisitizo wowote ndani yako. Ila ungejua thamani inayopatikana ndani ya Neno la Mungu, ungeweka kipaumbele hili jambo la kusoma neno la Mungu.

Tunalaumu hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu, kwa sababu hatujui tunachokipata ndani ya biblia. Hata tukipata huo muda wa kusoma Neno, tunalipua tu ili kutimiza wajibu. Ila ndani ya mioyo yetu hatuna kiu ya kutaka kujua Mungu anasema nini juu ya maisha yetu kupitia Neno lake.

Unapofanya jambo lolote bila kujua umhimu wake kwa undani wake, unaweza kuishia njiani. Usipoishia njiani utakuwa unafanya tu ili uonekane kwa wengine, ila ndani yako unaona hakuna chemichemi zozote za kutaka kujua kitu.

Hebu wewe mwenyewe fikiria una uwezo wa kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii zaidi ya masaa mawili, sio kana kwamba una shughuli kubwa unayoifanya la hasha. Ila unapofika kusoma Neno la Mungu unajiona upo bize sana, tena unajipa dakika 10 kwa haraka haraka kulipua, muda mwingine humalizi hata sura moja. Unaweza kufungua sura yenye mistari 40, ukasoma mistari 5 ukaishia hapo na kuona umesoma sura nzima.

Nazungumzia kufanya usomaji wa Neno la Mungu ni jambo la ziada, ziada hii ndio imetufanya tusione uzito wowote ndani yetu wa kutoa muda mzuri wa kutulia mbele za Mungu.

Naomba uelewe hili usije ukachanganya, unaweza kutoa muda wako wa ziada kufanya shughuli zako za ziada nje na ajira yako. Na kufanya hivyo kukakuletea mafanikio mazuri sana, mimi sizungumzii eneo hilo ninachozungumzia hapa ni kuliona suala la kusoma Neno la Mungu sio jambo la lazima sanaa.

Labda nikutolee mfano huu utanielewa zaidi, umewahi kuelewa kwanini kanisani unachelewa sana lakini huwezi kuchelewa kuingia kazini kwako, na huwezi kuchelewa kwenye vikundi vyenu vya vikoba. Huwezi kuchelewa na kutokwenda kazini kwa sababu unajua itakuweka kwenye hatari ya kufukuzwa, huwezi kuchelewa kwenye vikoba kwa sababu unajua kuna faini. Lakini kanisani unajua hakuna hayo mambo ya kufukuzwa wala kudaiwa faini.

Hili ndio kosa tunalofanya wengi wetu, tunayapa mambo mengine kipaombele sana, tunashindwa kujiwekea ratiba nzuri ya kutulia na biblia zetu tukisoma. Unafikiri kwa tabia hii itatuwezesha kulijua kusudi haswa ambalo Mungu ametuletea hapa duniani? unafikiri tunaweza kujua ahadi za Mungu juu ya maisha yetu? unafikiri tutaweza kuacha kutenda machafu pasipo Neno la Mungu kuwa kwa wingi ndani yetu?

Lazima kulipa Neno la Mungu mstari wa mbele, popote ulipo unapaswa kujua muda wako wa kusoma Neno la Mungu umefika. Kama kuna kitu ulikuwa unakifanya na kimeanza kula muda wako, unapaswa kulisimamisha hicho kitu.

Tukifika hatua za kulichukulia Neno la Mungu kwa uzito, tutaona mabadiliko makubwa sana juu ya maisha yetu ya kiroho na kimwili. Hakuna mtu atakuja kukushikia fimbo usome Neno, ni wewe kujipangia utaratibu wako.

Vinginevyo hili jambo la kusoma neno la Mungu litakuwa kero na makelele kwenye masikio yako. Elewa sikusisitizi hili kwa sababu mwisho wa mwezi nitapokea mshahara, nafanya hili bure kabisa kwa sababu ya msisitizo uliopo ndani yangu ni mkubwa. Inabaki kwako kuchukua hatua ya kusoma au usisome, ila mimi nitakuwa sina hatia kwako.

Bila shaka kupitia ujumbe huu umejifunza mengi ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu. Hakikisha unafanyia kazi uliyojifunza, nikiwa na maana hii, yaweke katika matendo yale uliyojifunza.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com