Nyundo Pekee Inayoweza Kuvunjavunja Ngome Za Shetani Ni Neno la Mungu.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa ili tukaendelee kumzalia matunda yaliyo mema. Ni nafasi ya pekee sana kwetu kuitumia vyema siku ya leo, kuweka alama njema mbele za Mungu.
Leo tunaenda kushirikishana mambo ya msingi sana ili tuweze kuitumia hii silaha, ukiijua silaha uliyobeba na ukaelewa matumizi yake, na ukawa na uwezo wa kuitumia silaha hiyo. Bila shaka utaweza kuitumia vizuri na utakuwa na ujasiri wa kuitumia pale inapobidi kufanya hivyo.
Tukijua umhimu wa kujaza Neno la Mungu ndani ya mioyo yetu, hakuna mtu atatusukuma kuwa na utaratibu huu wa kujisomea Neno la Mungu. Tunaweza kuwa tunajua umhimu wa Neno la Mungu lakini tusichukue hatua, hii bado tunaiita ni kutojua.
Neno la Mungu linaongeza imani zetu, jinsi tunavyozidi kusoma Neno la Mungu tunazidi kuimarisha silaha za kutumia katika maisha yetu. Silaha hii tunaweza kuitumia kwa imani pale tunapoona vita vinainuka juu ya maisha yetu.
Tunapokuwa na Neno la Mungu, tunakuwa na uwezo wa kushinda majaribu/changamoto mbalimbali zinazotuvuta turudi nyuma. Badala ya changamoto kukurudisha nyuma inakuwa daraja lako la kufika mbali zaidi kimafanikio.
Tunapokuwa na shida ambayo kibinadamu inaonekana hakuna majibu yake, Neno la Mungu linatupa majibu sahihi ya maswali yaliyokosa majibu yake.
Neno la Mungu unaweza kulitumia kama moto wa kuteketeza kila hila ambazo zinakuzuia usisonge mbele. Linaondoa kila hila na ngome mbaya za shetani zilizojikita ndani ya fikra zako.
Neno la Mungu linatupa ujasiri wa kutamka jambo ambalo kibinadamu linaonekana haliwezekani, Neno la Mungu linatupa uhakika wa kupokea jambo/kitu ambacho kwa wengine wamefika kipindi wamekata tamaa.
Neno la Mungu linatupa ujasiri wa kulisimamisha jina la Yesu Kristo eneo lolote lile, ambalo kwa mazingira ya kibinadamu panaonekana kuna ugumu wa kulitaja jina la Yesu.
Neno la Mungu ni kutupa uhakika wa kile tunachofanya sisi watenda kazi katika Bwana, tuna ujasiri wa kuwaambia wanaoabudu miungu mingine kuwa Mungu wetu anaweza kutenda makuu zaidi ya miungu yao, kwa sababu tuna uhakika ulioletwa na NENO la MUNGU ndani yetu.
Rejea; Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? YER. 23:29 SUV.
Umeona hilo andiko? Hapo anasema Bwana na si mtume/nabii/mchugaji/askofu, anasema Mungu mwenyewe Neno lake ni MOTO na NYUNDO. Kuna mahali utalitumia kama moto na kuna mahali unaweza kulitumia kama nyundo katika ulimwengu wa roho.
Nyundo unaweza kuitumia kujenga, vilevile unaweza kuitumia kuvunja kuta ambazo huzitaki, hii inaletwa na kujua matumizi sahihi ya kifaa ulichonacho. Labda unaweza kujiuliza nyundo inawezaje kujenga? Moja wapo ni kugongelea misumari kwenye bati/mbao.
Kiwango chako cha kulijua Neno la Mungu, kinakupa nafasi kubwa sana mbele za Mungu kudai kile unachoona kinakustahili. Utakuwa na uwezo wa kuliita jina la Yesu Kristo nyakati zozote zile unazoona zinamhitaji yeye mwenyewe. Kwanini tusitumie nafasi hii kuibeba nyundo ambayo itatusaidia, kwanini tusitumie moto kujifua kama dhahabu kwa kuondoa kila kilicho kichafu.
Tunapaswa kulitendea kazi hili, tutazame kwa namna ya tofauti sana kuhusu Neno la Mungu, tusilichukulie kawaidakawaida. Tuone ni silaha ya pekee sana inayoweza kutumiwa mahali popote pale na kwa mazingira yeyote yale.
Mungu akubariki sana kwa muda wako, nikutakie utendaji mwema katika siku ya leo.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com