Usifungwe Na Mawazo Yako Binafsi Amini Neno La Mungu.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona. Sio kwa ujanjaujanja wetu, bali ni neema yake imetufikisha leo, tunapaswa kumshukuru Mungu na kumzalia matunda yaliyo mema siku ya leo.

Wengi wetu tumekuwa na tabia ya kufuata mawazo yetu kwa kuyaona yanafaa sana kuliko Neno la Mungu. Hii imeletwa sana na jinsi tunavyoona wengine wakiishi maisha fulani na kuona yafaa kuishi vile kama wao.

Tumesahau mawazo yetu hayawezi kubadilisha Neno la Mungu liwe kama wao wanavyotaka liwe, haijalishi mawazo yale ni mazuri sana. Kama yapo kinyume na Neno la Mungu ujue unatenda dhambi.

Vipo vitu tumejihalalishia na kuona vipo sawa kutokana na kuamini mawazo yetu, ila ukija kwenye Neno la Mungu linakataa kabisa hayo mawazo yetu.

Tunaweza kufundishana na kupeana mbinu mbalimbali za maisha, kama ndani mwetu hakuna Neno La Mungu tujue tunapotea kabisa. Kupotea kwetu ni mbaya zaidi kwa sababu tunajiona tupo sahihi kumbe hatupo sahihi.

Unaweza kuiga mitindo fulani mibaya ya dunia kwa kuona haina shida yeyote. Lakini baadaye jinsi unavyozidi kufanya hayo yasiyofaa, unazidi kuwambukiza na wengine wakijua wapo sahihi kumbe wanakosea na wao. Ila kwa kuwa wanakuamini wanakuwa wanafanya vile walikuona wewe wakijua wapo katika msingi wa Neno la Mungu.

Mungu ametupa akili nyingi sana, na kila mmoja amejaliwa uwezo wa kufanya makubwa zaidi kwa kadri atakavyojibidiisha kwa kile anachokifanya. Ndani ya kufanya kule kunaibua mambo mengi, ndio maana tunaona tunaona leo tupo ulimwengu wa smartphone na mitandao ya kijamii. Haya yalitabiriwa tangu agano la kale kuwa maarifa yataongezeka.

Hatuwezi kupigana na mabadiliko ya dunia yanavyoenda, huenda zamani watumishi wa Mungu walikuwa wanahubiri injili kwa kutumia nguvu nyingi sana bila kipaza sauti. Lakini leo vipaza sauti vipo na vinasaidia injili kusonga mbele kwa urahisi zaidi.

Ukirudi nyuma ulikuwa huwezi kumwona mtumishi wa Mungu akihubiri live mpaka kwa wale walio eneo husika. Ila leo hii tunaweza kutumia mitandao kuona ibada live kila kinachoendelea kwenye semina/mkutano wa Neno la Mungu.

Hayo yote niliyokutolea mfano ni mabadiliko ya dunia inavyoenda, mabadiliko haya yanayotokea sio jambo geni bali ni yale ambayo yalishatabiriwa siku nyingi. Imebaki sasa kutimia kwa unabii ule.

Shida ipo pale tunapolikataa Neno La Mungu, na kuona mawazo yetu ni bora zaidi ya neno la Mungu. Ndio hapo unakuta watu wanaanza kujihalalishia uovu na dhambi kwa kulidharau Neno la Mungu.

Mila na desturi pia zinaweza kuonekana ni bora zaidi kuliko Neno la Mungu, ambapo ni kosa mila na desturi kutulazimisha kuabudu miungu mingine wakati Neno La Mungu limekataza kabisa kufanya hivyo. Mawazo yetu ni bora sana kama yatakuwa na hayapingani na Neno la Mungu.

Lazima tuelewe hili itatusaidia maeneo mengi katika maisha yetu, usifuate mapokeo yako ukapingana na Neno la Mungu. Haijalishi hilo jambo unalofanya linakupa manufaa kiasi gani, haijalishi hilo jambo unalofanya halijawahi kukupa madhara yeyote. Ikiwa linapingana na Neno la Mungu, ujue unafuata mawazo yako potofu ambayo yanakuelekeza pabaya.

Dira ya maisha yetu iwe inaongozwa na Neno la Mungu, kama Mungu amekukataza jambo fulani usilifanye, usilifanye kweli. Isiwe kwa sababu umeona mwingine analifanya halijamletea madhara na wewe ukaona ufanye tu.

Nasema hivi, usione rafiki yako alienda kwa waganga wa kienyeji akapewa vya kupewa. Akafanikiwa sana kwa jambo lililomshinda siku nyingi na bado mpo naye kanisani, ukaona hilo jambo la kwenda kwa waganga linafaa sana. Nakwambia hayo mawazo yatakupoteza vibaya sana, hakuna Neno la Mungu linaloruhusu kuchanganya miungu mingine na Mungu wa kweli.

Simamia Neno la Mungu linavyokuelekeza, usisimamie mawazo yako potofu ambayo mwisho wake ni jehanamu. Fahamu Neno la Mungu linasemaje, jambo sio kila kinachoonekana kimeandikwa, ila tunaye msaidizi anayetusaidia hayo yote. Ambaye ni Roho Mtakatifu, huyu hutupa mwelekeo na amani ndani ya mioyo yetu kufanya yale yanayompendeza Mungu.

Weka bidii na nidhamu katika kulijua neno la Mungu na kuliishi jinsi linavyokuelekeza, vinginevyo utajianzishia mambo yako ya ovyo. Mwisho wako ukawa mbaya sana, maana utakuwa umeruhusu uharibifu mkubwa ndani yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, naamini lipo jambo umelipata katika ujumbe huu la kutendea kazi.

Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com