Usifanye Kwa Mkono Mlegevu Wapo Wanaokufuatilia Utawaumiza Kwa Uzembe Wako.
Haleluya mwana Mungu, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa fursa ya kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa wema wake mkuu namna hii, huenda hatukustahili sana kufikia leo. Ila kwa neema yake Mungu ametupa kuiona siku ya leo.
Huwa tunajitazama sisi kama sisi na kuona hata tusipofanya vizuri sana, hakuna anayetuona wala hakuna anayetujali sana. Tunasahau yupo mtu mmoja anakuamini na anajifunza vitu kutoka kwako bila kujali kiwango chako ulichonacho.
Tunajua kabisa tupaswa kujifunza kwa waliofanikiwa, na kwa unayeona hana cha kujifunza kwako unapaswa kuepukana naye. Unapothubutu kufanya jambo fulani elewa wapo watu eneo hilo ambao watakufuatilia sana jinsi unavyofanya, ili na wao wapate kujifunza kitu kupitia wewe.
Tunapokuwa kwenye nafasi fulani wale mashabiki/wafuasi wetu wanaopenda kuona tunafanya vizuri, tunakuwa tunawaumiza sana tunapokuwa tumefanya kwa uzembe. Huku moyoni mwako unaweza kubaki ukijipa faraja kuwa ulichoka au siku hiyo ulikuwa hujisikii kufanya.
Kila mmoja wetu ana nafasi ambayo kuna watu wanamtazama kama mwalimu wao au kama kocha wao. Katika hao wanaokufuatilia, wapo watu ambao watakuwa tayari kukukimbia kwa udhaifu unaorudia kila siku. Na wapo hawatakuwa tayari kukuacha kukufutilia, maana ndani yao hawaoni mtu mwingine wa kujifunza vizuri wakilinganisha na wewe wanakuelewa zaidi.
Unaweza kuona hili ninalokuambia haliwezekani kabisa kwako kutokana na hali uliyonayo, ila fahamu yupo mtu. Anaweza akawa mdogo wako, anaweze kuwa mtoto wako, anaweza kuwa mfanyakazi wako, anaweza kuwa jirani yako, na anaweza kuwa mshirika mwenzako kanisani. Inategemeana na nafasi uliyonayo katika jamii yako inayokuzunguka.
Yupo mtu anapenda unavyovaa, ukivaa mtindo fulani na yeye anaenda kutafuta nguo ile anavaa. Yupo mtu anapenda unavyoongea, yupo mtu anapenda unavyoweka nywele zako, yupo mtu anapenda jinsi unavyonyoa. Ukifanya jambo lisiloeleweka anajiona umemwebisha na yeye, huenda hamjawahi hata kukaa kiti kimoja mkaongea.
Ndio maana huwa napenda kuwaambia sana dada na kaka zangu kuwa na bidii katika mambo ya Mungu. Inaweza kumbadilisha na yule rafiki yake mwingine anayemwamini sana na kumsikiliza anachosema. Anaweza huyo mtu hamfahamu yeye kama yeye, ila kupitia yeye kubadilika inamvuta zaidi mtu huyo anayemfuatilia na yeye kubadilika.
Kama unaimba jua wapo watu wanakufuatilia uimbaji wako, haijalishi wewe unajiona kwa kiwango cha chini sana. Yupo mtu anafurahishwa sana na kiwango chako cha uimbaji, ukileta utani kwenye eneo hilo ukafanya vibaya anaumia sana.
Kama ni mtumishi wa Mungu unafundisha Neno la Mungu, ukafanya jambo linalomchukiza Mungu, jua kabisa hujamkosea tu Mungu. Umewaumiza wale wote wanaokuamini na kukufuatilia, sio wanakufuatilia tu vipo wanajifunza kutoka kwako.
Ndio maana ukisoma mstari huu unaweza kunielewa zaidi ukitafakari;
Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Marko 14 : 27 SUV.
Unaweza usiwe mchungaji kanisani, ukawa mchungaji wa watu fulani unaowachunga kwa matendo yako mema. Unapojigeuza kwa matendo mabaya yupo hana uwezo wa kupuuzia mabaya yale na kuyaacha, atakufuatisha vilevile unafanya wewe.
Kwanini nimekuandikia haya, ni ili uwe na bidii katika mambo ya Mungu. Vipo vitu tunafanya kwa uzembe mwingi sana tukijua hakuna anayetuona wala kutujali sana. Tumebaki na juhudi kwa yale mambo ya mwili tunayojua tusipofanya kwa bidii madhara yake yanatupata palepale.
Soma Neno la Mungu kwa bidii sana, haijalishi unajiona upo peke yako fanya kwa bidii. Bidii yako inampendeza Mungu na wale wanaokujua kwa sura na wasiokujua kwa sura. Bidii yako inawavuta watu wengi zaidi kujifunza kwako, unapofika muda unaanza kufanya kwa mkono mlegevu unawaumiza mioyo yao wengine.
Unafanya kwa ajili ya Mungu, na unafanya kuimarisha mahusiano yako na Mungu. Ila fahamu kwamba kufanya hivyo kwako Mungu anakupa mwanafunzi wa kujifunza kupitia wewe. Mchungaji unapoanza kupoteza mwelekeo, hutopotea wewe tu, lipo kundi kubwa nyuma yako unalipoteza.
Mjue sana MUNGU ufanikiwe katika mambo yako yote, kumjua kwako Mungu inakupasa kujifunza sana Neno lake kwa bidii.
Nakushuru sana kwa muda wako, nikutakie siku njema.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com