Bidii Yako Ya Kumtafuta Mungu Isije Ikawa Ni Kutaka Kuonekana Kwa Watu Ili Iwe Rahisi Kwako Kusaidiwa Jambo Lako
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku mpya inapofika kama leo tunapaswa kumshukuru Mungu kwa neema yake hii. Kumshukuru Mungu ni Njema sana inaonyesha ni jinsi gani unajua kupewa nafasi ya kuiona leo, ni Mungu yeye amefanya hivyo.
Karibu sana tushirikishane mambo machache mhimu ya kutusaidia sote katika safari yetu ya wokovu. Sio rahisi sana wengi kuupenda ukweli ila inapofika kipindi tunapaswa kuusema ili kuokoa yule ambaye yupo tayari kuokolewa.
Kumekuwa na tabia moja ya ajabu sana, sijajua sana ni mbinu ambayo mtu anakuwa anafundishwa au anakuwa nayo mtu ndani yake. Pale mtu anapoona ana jambo lake mbele anapaswa kupata msaada wa wengine, utamwona anaanza kuwa mstari wa mbele kuwa karibu na wandugu/watumishi.
Nimeshuhudia vijana wengi sana wakati wa kuoa na kuolewa, huwa wanakuwa karibu mno na watumishi wa Mungu, na washirika wengine. Bidii yao ya kuwa Karibu na watumishi sio kwa faida ya kiroho, bali ni kwa faida yao wenyewe ikifika siku ya tukio lao aweze kupata ushirikiano mkubwa.
Kama ni kanisani utamwona kila tukio, kwa haraka haraka utasema kwa kweli huyu kijana amebadilika, kwa kutokujua kwako utasema huyu baba/mama amekuwa na bidii sana kwa mambo ya Mungu. Ngoja sasa atimize jambo lake, hutokaa umwone tena kwenye vipindi vya katikati ya wiki. Ukiuliza unaambiwa yupo bize sana, huo ubize hukuwepo hapo nyuma ila umekuja baada ya kumaliza jambo lake.
Tumeona wengine wakitengeneza urafiki wa ghafla, na urafiki wao unakuwa urafiki haswa wa kubanana kiasi kwamba unaona kabisa huu sio urafiki wa kawaida. Urafiki ule kumbe unataka kitu kutoka kwako, na wasipokipata huwa wanageuka maadui wabaya sana.
Najua umewahi kuona urafiki wa mtu anayetaka kukukopa pesa yako, atajenga mahusiano mazuri sana ya karibu. Akishapata alichokuwa anakitafuta kwako, hata hilo deni hatalilipa kwa wakati au asikulipe kabisa. Ukimfuatilia sana atakuona wewe hufai kabisa, amesahau anakuona hufai kwenye kitu chako ulichompa.
Mtu wa kutaka kitu kwako atakupa kila sifa, unaweza kusifiwa kiasi kwamba wewe mwenyewe unaona huu sio usifiwaji kabisa wa kawaida. Maana vipo vitu unaona hukufanya vizuri ila unaona sifa kibao, kuna vitu unaona kabisa ni vya kawaida sana ila unavyomwagiwa maneno unabaki mdomo wazi.
Sikufundishi uache kutia moyo wengine, nataka kukuonyesha jambo kama ni kupona upone, kama ni kuepuka utapeli uepukane nao leo.
Hapa ndio utakutana na idadi kubwa ya watu, wanakuwa karibu zaidi na Mungu pale wanapokuwa kwenye kipindi kigumu. Pale mtu anapokuwa hana msaada wowote kwa ndugu wala jamaa zake, pale anapokuwa amebananishwa na nguvu za giza. Anakuwa mstari wa mbele sana kumtii Mungu, ila baada ya kupona na kupata msaada wa Mungu, anaacha ile bidii yake ya kumtegemea Mungu.
Haya maigizo tunayaona sana ndani ya kanisa, huenda mchungaji hakupata nafasi ya kukuambia ila mimi leo naomba nikupe ukweli. Ili kama ni kupona upone na kama kuendelea na upuuzi wako uendelee nao tu.
Kuna kaka mmoja alipokaribia kuoa, nilikuwa namwona sana kanisani yaani nilikuwa simjui mpaka nikamjua jina na alipozaliwa. Kama ni vurugu za kung’ang’ana na Mungu basi yeye alikuwa mstari wa mbele, kabla muda wa ibada kufika utamkuta yupo nje anasubiri geti kufungiliwa aingie. Kama siku sio za ibada humkosi maeneo ya kanisani, nafikiri alikuwa akimaliza kazi zake. Alifanya eneo lake la kupumzikia ni maeneo ya kanisani.
Baada ya kuoa sasa, sijawahi kumwona tena kwenye kipindi chochote zaidi ya jumapili tu, namaliza mwaka sasa. Hata kama anabanwa sana na kazi, hawezi kubanwa mwaka mzima kushindwa kuhudhuria ibada zote za katikati.
Yupo tena dada mmoja nilikuwa simjui kabisa, hata kwenye macho yangu alikuwa mgeni kabisa. Ila alijenga ukaribu mkubwa sana wa ghafla, nikajipa muda nisimhukumu haraka huenda alikuwa na nia nzuri. Haikuchukua muda akanipa kadi ya sendoff, baada ya kumaliza shughuli yake sikumwona tena alipopotelea.
Nikiendelea kukutajia watu wa namna hii ni wengi mno, na mpaka hapa nitakuwa nimekukumbusha idadi kubwa sana ya marafiki waliobuka kwako ghafla na kupotea.
Wengi wa hivi huwa hawashiriki matukio ya wengine mpaka wameona ya kwao yamekaribia ndio utamwona yupo mstari wa mbele. Kama ni mama siku zote alikuwa amejitenga na wamama wenzake, akishaona binti/kijana wake amekabiria kuoa/kuolewa. Utaanza kumwona akijihusisha na mambo ya akina mama wenzake ili tu apate ushirikiano siku ya tukio.
Kwanini nakueleza haya mambo, nasikia msukumo wa kukueleza haya kwa sababu kuna kundi kubwa wamebeba wake sio wao, na wapo wamebeba waume sio wao. Na wapo wameamini watu wakawapa pesa zao wakiwa na imani watarudishiwa, badala yake wametapeliwa na hao waliowaamini.
Wengi wanaanza kwa bidii kusoma Neno la Mungu, ukijua mpo pamoja na mwenzenu hasa hasa njia hii ya wasap. Kumbe mwenzetu hasomi Neno la Mungu akue kiroho, anasoma ili aonekane na wengine siku moja apate msaada. Ninao marafiki zangu kazaa katika hili, walikuwa na bidii sana kusoma Neno la Mungu kabla ya kuolewa. Baada ya kuolewa tu wakapotea, labda unaweza kusema majukum ya ndoa yamewabana sana.
Wapo wamama wanalea watoto, ila hawajaacha kutenga muda wao kusoma Neno la Mungu. Wapo wamama walizaa kwa operation, lakini walikuwa wanatenga muda wao wa kujifunza neno la Mungu. Binafsi nilikuwa nawashangaa mno ila ndio ulikuwa ukweli wenyewe.
Kila mmoja akimaanisha kumjua Mungu kupitia Neno lake, atamjua tena sana. Ila mtu akiingia kwa mgongo wa kumjua Mungu kutaka kupata kitu fulani kwenye kundi, hao watu huwa hawafiki popote.
Kuanzia sasa kama umeamua kujitoa kwa Mungu jitoe kwelikweli, usiwe na wokovu wa kutaka kutatuliwa shida yako. Usiwe na wokovu wa kutaka kusaidiwa, usiwe na wokovu wa kutaka kujulikana. Kuwa na wokovu unaomtafuta Mungu kwa bidii kujenga mizizi imara ya kukusaidia kusimama vizuri.
Vijana tuache wokovu wa maigizo, muda tunao mwingi sana wa kumtumikia Mungu katika roho na kweli. Kuruka ruka ili kutafuta idadi ya marafiki waje wakubebe kwenye jambo lako sio mbaya, ila ni mbaya sana wokovu wako kubebwa na kuhitaji msaada.
Bila shaka kuna jambo umejifunza, nia yangu uondoke kwenye utoto wa kiroho, maana hayo yote niliyokueleza ni uchanga wa mtu kiroho. Ndio unamfanya mtu kuwa hivyo.
Nashukuru sana kwa muda wako, nikutakie siku Njema.
Endelea kuwa nasi kwa kutembelea mtandao wetu kujifunza zaidi,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com