Kupenda Kufanya Jambo Fulani Toka Ndani Ya Moyo Wako Hakuondoi Udhaifu Wa Mwili Wako.
Haleluya, siku nyingine tena Bwana wetu Yesu Kristo ametupa kibali cha kuiona, sifa na utukufu tumrudishie yeye kwa wema wake mkuu. Hupaswi kujuta kuzaliwa kwa sababu ya changamoto ya jana, furahia uwepo wako kwa sababu Mungu ana kusudi jema na wewe.
Shughuli za kutwa nzima zinaweza kuwa sababu na chanzo cha sisi kujisikia wenye kuchoka sana, na kuona mambo mengine tunapaswa kuyasitisha. Kusitisha hayo mambo kunaweza kutuletea hasara kubwa zaidi, au kunaweza kuleta faida fulani kubwa na nzuri kwa kulipa jambo lingine nafasi zaidi.
Ikiwa kazi zako zinakubana kiasi kwamba huwezi kushika simu yako ya mkononi, na ukaingia mitandao ya kijamii. Mpaka unaingia saa ya kulala hujui kwenye magroup ya wasap wameandika nini. Na hujui marafiki zako wa facebook na instargram, na twiter, wameandika nini, hapo tunaweza kusema kweli upo bize. Ila kama unapata muda wa kuingia huko, huwezi kusema umebanwa na kazi kiasi kwamba huna muda wa kumpa Mungu katika kusoma Neno la Mungu.
Hatuwezi kukwepa uchovu wa miili yetu, inafika wakati umechoka kweli unaona hata kile ulichojiwekea utaratibu wa kukifanya. Unakiona hakina nafasi ya kukifanya kwa muda huo, hapo ndipo wengi tunaporudi nyuma kwa kile tulichokuwa tunakifanya.
Kuchoka kupo, ila hatuwezi kuruhusu kuchoka kule kutuzuia kabisa kutimiza ratiba zetu. Unachotakiwa kuangalia ni mambo yapi ya kuweka kipaumbele sana uyafanye kabla ya kuchoka. Na mambo yapi yawe ya mwisho ambayo unaweza kuyafanya wakati umechoka, bila kuathiri kitu chochote kwako.
Hatuwezi kuupa tu mwili nafasi ya kufanya kile unachotaka wenyewe, kuna vitu itakubidi ujilazimishe kufanya. Ukishajizalimisha kufanya sio kana kwamba utajisikia vibaya na kuchoka zaidi, ipo furaha ya ushindi utajisikia ndani yako. Hutojisikia kuhukumiwa ndani ya moyo wako kwa sababu ya kutekeleza kile ulichopanga kukifanya.
Wakati mwingine tunashindwa kuelewa kwamba, hata kama jambo linamletea Mungu sifa na utukufu. Kuna saa unajikuta mwili wako hujisikii kabisa kukifanya hicho kitu, zaidi sana unakusumwa kulala au kukaa tu. Hapa ndipo unahitaji nidhamu yako binafsi kuulazimisha mwili wako na akili zako kutulia kwenye eneo husika.
Kujipa sababu kila siku umechoka au umebanwa na kazi wakati haipiti lisaa limoja unachungulia kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii. Huo ni uzembe wa kiwango cha juu sana kuendelea kujifariji nao. Lazima ufike wakati ujue kupenda mambo ya Mungu hakukufanyi uache kujisikia kutokufanya, hizo hali zipo ila hatuwezi kuzikubali tu kirahisi.
Kusoma Neno la Mungu kunahitaji nidhamu ya juu sana ndani yako, japo ni kweli kuna siku zinakukuta kwenye hali fulani ambayo wewe mwenyewe unaona kabisa huwezi kushika biblia yako. Ila hali hiyo haiwezi kudumu siku zote, iwe sababu ya wewe kutokusoma kabisa neno la Mungu.
Tunapaswa kujishughulisha kwa bidii sana na kazi za mikono yetu, iwe umejiajiri au uwe umeajiriwa au uwe unasoma, unapaswa kujituma haswa kwa unachofanya. Ila kujituma kwako kusiondoe mpaka na nafasi ya kumpa Mungu muda wako wa kutulia mbele zake kusoma na kufakari Neno lake.
Labda unaweza kufikiri hizi jumbd ninazokuandikia kila siku, huwa ninaamka nina kiu sana ya kufanya hivyo la hasha! Muda mwingine nakuwa mchovu sana kutokana na hali tu ya mwili. Ila sikubaliani nao moja kwa moja, nitaulazimisha mpaka unakubali kufanya kile moyo wangu unataka kufanya.
Usikae eti unasubiri uje upate nafasi kubwa sana, nakwambia utasubiria miaka yako yote. Hiyo nafasi hutakaa uione ikitokea, maana kila siku kunaamka na habari zake tofauti kabisa kwenye maisha yako. Huenda leo unajiona huna nafasi ila kesho ukajiona ulikuwa unachezea muda wako mwingi sana, unaweza leo kujiona umechoka sana kesho ukajiona ulikuwa unajidekeza tu.
Usiufuatishe sana mwili wako unavyokutaka usifanye, usijionee huruma mpaka ukapitiliza kuwa uzembe/uvivu. Uwe na kiasi katika kujipa mapumziko ya mwili wako, isije ikakutokea uchovu wa siku moja ukakupelekea kuacha kabisa kujifunza Neno la Mungu.
Kila mmoja amepewa masaa hayohayo 24 unayotumia wewe, inabaki ni jinsi gani utayatumia hayo masaa 24 kukuletea faida mbele za Mungu. Kuchoka kupo ila isiwe ndio wimbo wako wa kila siku iendayo kwa Mungu.
Mungu akubariki sana kunipaa muda wako kusoma ujumbe huu, nichukue nafasi hii kukutakia siku njema kwako na familia yako.
Usiache kufuatilia masomo mazuri kupitia mtandao wetu,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com