Kuna Tabia Mbaya Za Asili Haziondoki Haraka Ndani Ya Mtu Aliyeokoka Mpaka Atakavyozidi Kumjua Mungu Zaidi
Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu katika Kristo. Siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuiona, sifa na utukufu tunamrudishia Bwana.
Karibu tushirikishane mambo ya msingi ya kutusaidia katika safari yetu ya wokovu, naamini utakaondoka na kitu cha muhimu kukusaidia kusonga mbele zaidi.
Zipo tabia ambazo mtu anakuwa nazo kabla ya kuokoka, baada ya kuokoka wengi huwa tunategemea hizo tabia zitamwondoka mtu huyo. Ila utashangaa bado zinamng’ang’ania mpaka akiwa ndani ya wokovu, unashindwa kuelewa sana mbona inakuwa hivyo.
Tabia zile mbaya mtu anaweza kuwa hazipendi yeye binafsi, ila kwa kuwa hajui atafanyaje, na hajui atawezaje kuzikwepa. Anajikuta amefanya kosa ambalo linamuumiza moyo wake kiasi kwamba anaona wokovu unakuwa mgumu kwake.
Unakuta mtu alikuwa mlevi, akaamua kuokoka sasa akitegemea ile hali itamwondoka kabisa. Kweli ile kiu ya pombe itakatwa, ila inategemeana na mtu mwenyewe jinsi atakavyokuwa anajibidiisha katika mambo ya Mungu. Na kuepukana na makundi mabaya yanayomshawishi kunywa pombe. Badala yake anajikuta anarudia kunywa pombe kama awali ila kwa siri siri.
Unakuta mtu kabla hajaokoka alikuwa amejaa matusi mdomoni kiasi kwamba hawezi kuongea kitu bila kuunganisha sentensi na tusi. Alivyokoka tunategemea wote hali ile ingemwondoka kabisa, ila unaweza kushangaa bado anaendelea kutukana.
Unaweza kuona watu mbalimbali waliokoka na bado wana tabia fulani za ajabu hujawahi kufikiri kama mtu aliyemjua Kristo anaweza kuwa hivyo. Usishangae kumwona dada akiendelea kuvaa mavazi ya kikahaba bila wasiwasi wowote, na wakati watu walitengemea kumwona tofauti.
Usishangae kumwona mama anaendelea kuwa mchonganishi na mmbea, wakati walio ndani ya nyumba ya Kristo hawana tabia hiyo. Utasema nyumba ipi hiyo mbona wapo watu wengi wamejaa tabia za ajabu ajabu makanisani, rejea maneno yangu ya mwanzo hasa kichwa cha somo utakumbuka vizuri ninachokisema.
Vipo vitabia vingi sana mtu anaweza kuwa navyo ndani yake, vingine mtu anaweza kuwa anapambana navyo vimwondoke. Na vingine vinaweza kuwa mtu anavyo ila hajui kama ni vibaya kwake.
Ipo habari njema sana kwako ndugu yangu katika Kristo, habari hii inaweza kuwa njia yako ya kukuongoza kufika vile viwango unavyohitaji kufikia.Haijalishi unaona ngumu mtu kuacha kabisa uzinzi/uasherati, haijalishi unaona mtu hawezi kabisa kuacha kuvuta singira, haijalishi unaona haiwezeakani kabisa mtu kuacha tabia za udokozi. Hii labda kwa sababu umeona wengi wakijaribu kuacha alafu wanajikuta wakirudi kule kule.
Dawa ya kuondoa vitabia hivi vibaya vya asili, ni kujitoa kuutafuta uso wa Mungu kwa kumaanisha kweli. Unapaswa kutafuta kila njia ya kuweza kusikia maneno ya Mungu, unapaswa kutafuta kila njia ya kupata marafiki wanaompenda Mungu haswa.
Sio jambo la kuchukulia kawaida, kila kundi linalokushawishi usiwe na bidii ya kumtafuta Mungu wako. Hilo kundi hakufai kabisa kwako, kundi linalokuambia kuomba ni ushamba au kusoma Neno la Mungu ni kupoteza muda, au kuhudhuria ibada za kila siku ni kutumia muda wako vibaya. Wakati huo huo muda wanaokuambia unatumia vibaya, wanautumia muda wao vijiweni kuongelea mambo yasiyofaa.
Jinsi unavyozidi kuongeza bidii yako ya kumjua Mungu kupitia Neno lake, kuna vitabia vya asili vinazidi kunyonywa taratibu na kuondolewa kabisa ndani yako. Hiyo ni kufanywa upya ndani mwa mtu kila siku, tabia mbaya uliyokuwa nayo jana unaweza usiwe nayo leo mpaka unaondoka hapa duniani.
Vile vitabia vibaya vya siri siri ulivyokuwa unavifanya, hofu ya Mungu ikishakukamata vizuri kwa kushiba NENO LA MUNGU. Hutoona tabu tena kuviacha hivyo vitabia, maana utakuwa una jibu la namna ya kuachana na hivyo vitabia.
Vipo vitabia unavifanya ambavyo unavijua mwenyewe havimpendezi Mungu, na una uhakika kabisa hakuna mtu anayevijua isipokuwa wewe na Mungu wako. Vinawezekana kuondoka kabisa ukiwa na bidii ya kumtafuta Mungu.
Kujifariji hakuna anayekuona kwa hicho unachokifanya, bado haiwezi kukufanya ukampendeza Mungu. Bado utafanana na mwingine yeyote ambaye anatenda maovu.
Lakini unapojitoa kulisoma Neno la Mungu kila siku, kuna vitu vibaya vitaondoka kabisa, unaweza usielewe sana uliachaje kitu fulani. Ila nakwambia Mungu ni Mungu tu, ndio maana Yesu Kristo akatuhimiza tuendelee kuwa wanafunzi. Tabia ya mwanafunzi ni kujifunza kila siku, hakuna siku utasema umejua kila kitu.
Unapenda kufikia viwango fulani vya KiMungu, unapenda kuwa na hekima ya kiwango fulani katika maisha yako, unapenda huduma yako iwe na nguvu zaidi. Penda kusoma Neno la Mungu na kulitafakari, neno la Mungu linakuelekeza kila kitu cha kufanya ili uwe vile unataka kuwa. Unahitaji kuwa mwombaji mzuri utaipata ndani ya biblia, unahitaji kuwa mwimbaji mzuri utaipata ndani ya biblia.
Ile tabia ya kushindwa kusamehe utakutana nayo kwenye Neno la Mungu, ile tabia ya kuzungumza ovyo ovyo utaipata ndani ya neno la Mungu. Ile tabia ya kushindwa kumtii mume wako kama kichwa cha familia utaipata, ile tabia ya kushindwa kumpenda mke wako na kumtunza utaipata ndani ya biblia.
Tabia zote ambazo unazijua unazo na usizozijua kama unazo, silaha yake kuu ya kuzimaliza ni Neno la Mungu. Unaona ni jinsi gani Neno la Mungu lilivyo na uwanja mpana katika maisha yako, kujua hivi inakupa picha kubwa na umhimu wa hili jambo.
Bila shaka hupendi vitabia fulani katika maisha yako ya wokovu, ila huwa unajikuta umefanya. Hebu kuanzia sasa weka bidii katika mambo ya Mungu, utabadilika mwenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote. Haijalishi watu wamekuonyeshea vidole kiasi gani, kupitia wewe watasema hakika huyu ndugu sio yule wa mwezi uliopita. Amebadilika na amekuwa mtu wa tofauti kabisa anayempenda Mungu sana sivyo kama zamani.
Kubadilika kwako utawasaidia wengi sana kubadilika, hata kama usipowaambia badilikeni, watakavyokutazama wewe watapata msukumo wa kubadilika. Una kitu hukipendi kwako kipeleke kwenye juhudi za kumtafuta Mungu kwa bidii, hata kama huelewi elewi vizuri.
Nilikuahidi hutaondoka kwenye ujumbe huu bila kujifunza kitu cha kukusaidia, napata ujasiri wa kusema kipo kitu umejifunza. Usibaki kusema kweli, chukua hatua sasa, ongeza umakini wako zaidi kwenye mambo ya Mungu.
Mungu akubariki sana Kwa Muda wako, nikutakie wakati mwema.
Usiache kutembelea mtandao wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com